ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 12, 2016

MWANAMAPINDUZI YA ZANZIBAR, MZEE IBRAHIM AMAN AZIKWA LEO KATIKA KIJIJI CHA KWALE.

 Viongozi wa Kitaifa waliohudhuria mazishi ya  Marehemu Mzee Ibrahim Amaan wakikamilisha hitma ya kumuombea kiongozi huyo Mwanamapinduzi ya Zanzibar huko Kijijini kwake Nymanzi Wilaya ya Magharibi “B”.
 Baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislamu wakisubiri ibada ya sala ya Maiti kwa ajili ya kumuombea Dua zee Ibrahim Amaan kwenye Msikiti wa Ijumaa aliokuwa mioingoni mwa watu waliouanzisha Kijijini kwake Nyamanzi.
Waumini wa Dini ya Kiislamu wakiongozwa na Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Ngwali walimsalia Mzee Ibrahim kwenye msikiti wa Kijiji hicho.
Picha na – OMPR – ZNZ.
                                   
MWANAMAPINDUZI ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ambae pia ni mwanzilishi wa Chama cha Mapinduzi Mzee Ibrahim Aman aliyefariki Dunia jana mchana amezikwa leo Kijijini kwake Nyamanzi Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mzee Ibrahim aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya baridi pamoja na Uzee alilazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja akipatiwa matibabu kutokana na afya yake.

Mamia ya Wananchi, waumini wa dini  pamoja na Viongozi wa Kitaifa walihudhuria mazishi hayo yaliyojumuisha pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Rais Mstaafu wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi pamoja na Makamu wa Rais Mstaafu wa SMT  Dr. Mohammed Gharib Bilal.

Mzee Ibrahim Amaan alizaliwa mwaka 1930 katika Kijiji cha Nyamazi na alipofikia umri wa kusoma Wazazi wake wakampelekea kupata elimu ya Quran iliyoambatana na ile ya Dunia katika ngazi ya Msingi.

Wakati wa ujana wake marehemu Mzee Ibrahim Amaan alijishughulisha na kazi za ukulima na uvuvi ili kujipatia kipato kilichomuezesha kuanza kujitegemea katika maisha yake ya kawaida.

Mwaka 1957 Mzee Ibrahim alijiunga na Chama cha Afro Shirazy Party ambapo  kutokana na uzalendo pamoja na umakini wake alifanikiwa kuwa muanzilishi wa Umoja wa Vijana wa ASP  Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika Uhai wake marehemu Mzee Ibrahim aliwahi kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri ya Chama cha Afro Shirazy Party na kushiriki kuuangusha Utawala wa kisultani Mwaka 1964 na baadaye kujiunga na Jeshi la Ukombozi la Unguja akifikia cheo cha Kanal.

Akisoma Risala ya wakfu wa Marehemu Mzee Ibrahim Makungu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Ikulu na Utawala Bora Dr. Miwinyihaji Makame alisema Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zimepokea kwa masikitiko kifo cha Mwanamapinduzi huyo aliyejitolea muda wake wa maisha kulitumikia Taifa hili.

Dr. Mwinyihaji alisema Ushujaa wa Mzee Ibrahim ulimpelekea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kumtunukia Nishani ya Ushujaa wa Mapinduzi kwenye sherehe hizo za mwaka 2014.

Alisema Mzee Ibrahim miongoni mwa majukumu yake  kwa Taifa aliwahi pia kuwa Mbunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu wa  CCM Idara ya Umma Afisi kuu ya CCM Kisiwandui pamoja na Mwenyekiti wa kazi za njia na nnguvu za umeme.

Dr. Mwinyihaji alifafanua zaidi kwamba Mzee Ibrahim alikuwa Mjumbe wa Baraza la Wazee la Chama cha Mapinduzi wadhifa ambao aliendelea nao hadi mauti yalipomfika.

Mzee Ibrahim  Amaan aliyezaliwa mwaka 1930 na kufikisha umri wa Miaka 86 ameacha kizuka Mmoja na Watoto Thalathini.
Yarabi aiweke roho ya Marehemu Mzee Ibrahim Amaan mahali pema Peponi amin.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/3/2016.


No comments: