Matukio ya uchomaji makazi ya watu yameendelea kutikisa visiwani hapa siku chache kabla ya uchaguzi wa marudio baada ya watu wasiofahamika kulipua nyumba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame iliyopo Kijichi, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Hili ni tukio la tatu kuwekwa bayana ndani ya wiki mbili baada ya watu wasiofahamika kuchoma moto Maskani ya Kisonge iliyopo Michenzani, Unguja Machi 3 na wengine kuchoma nyumba 11, maskani tatu na kituo cha afya siku nne zilizopita.
Matukio hayo yametokea wakati hali ikiwa tete visiwani hapa baada ya Tume ya Uchaguzi (ZEC) kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu na kutangaza Machi 30 kuwa siku ya kurudia kupiga kura, huku chama kikuu cha upinzani CUF kikitangaza kutokubaliana na uamuzi huo.
Akizungumza na wanahabari kwenye ofisi za makao makuu ya polisi yaliyopo Ziwani kisiwani Unguja, Kamishna Makame alisema mlipuko huo ulitokea juzi saa 5:00 usiku.
“Kwa hili lazima tuchukue hatua hata kama watu watasema sana na kulaani. Hata kama ni kiongozi, hatuwezi kuiacha hali hii iendelee,” alisema Makame.
Alisema kumekuwapo na matukio mengi yanayojitokeza katika uchaguzi huo wa marudio na kutoa onyo kali kwa wale wanaohusika kufanya vitendo hivyo kuwa hawatavumiliwa na lazima wachukuliwe hatua kabla nchi haijaingia katika hatari zaidi.
Makame alisema uchunguzi wa uchomaji Maskani ya Kisonge pia unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahalifu wote waliofanya kitendo hicho na kuahidi kuwa katika kipindi kifupi kijacho watatiwa mbaroni na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Kamishna Makame alisema upande wa Pemba wanawashikilia watu 31 kwa mahojiano.
Polisi waongeza nguvu
Kuhusu suala la usalama kuelekea uchaguzi wa marudio Jumapili hii, Makame alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limeamua kuongeza nguvu ya ulinzi katika maeneo yote ya nchi kwa kufanya doria, kuongeza kasi ya ukusanyaji wa taarifa za kiintelejinsia na kufanya misako katika maeneo yanayotiliwa shaka.
“Uchaguzi utafanyika kwa hali ya amani na yeyote atakayethubutu kuanzisha ishara ya kuleta uvunjifu wa amani, atapambana na mkono wa dola na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema kamishna huyo.
Wakati huo huo, watuhumiwa 21 wa kesi ya kuchoma moto nyumba za makazi, kituo cha afya pamoja na maskani za CCM katika Mkoa wa Kaskazini Pemba wamerejeshwa mahabusu baada ya kesi inayowakabili kushindwa kufunguliwa kutokana na mkinzano wa taratibu za kisheria.
Upande wa mashitaka ulisema hautafungua kesi hiyo mpaka upelelezi ukamilike.
Watuhumia hao walikamatwa Machi 14, wakituhumiwa kuhusika na matukio hayo ya kuchoma moto ambayo yalitokea maeneo tofauti kwa wakati mmoja.
Mwanasheria wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba, Alibagher Yakuti alisema: “Sisi hatuwezi kufungua kesi ambayo ushahidi wake haujakamilika, halafu baadaye kesi hiyo iondolewe baada ya kukosa ushahidi, hivyo tumeirejesha kwa Polisi ili wafanye haraka upelelezi nasi tuweze kuifungua na kuanza taratibu za kusikilizwa.”
Kwa upande wake Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Kaskazini Pemba, Issa Juma Suleiman alikiri kupokea agizo hilo kutoka kwa ofisi ya DPP na kueleza tayari wapelelezi wameshaanza kuingia mitaani kukusanya ushahidi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment