Wednesday, March 2, 2016

Polisi, Ukawa jino kwa jino

By Waandishi Wetu, Mwananchi; mwananchipapers@mwananchi.co.tz


Dar/mikoani. Jeshi la Polisi limeendelea na kamatakamata ya wapinzani wa vyama vinavyounda Ukawa katika maeneo mbalimbali likieleza sababu tofauti za kijinai zinazohusishwa na masuala ya kisiasa.

Katika matukio ya karibuni, wabunge wa upinzani; Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga) na Peter Lijualikali (Kilombero), wote wa Chadema na baadhi ya madiwani wa chama hicho katika Jiji la Dar es Salaam walikamatwa.

Pia, baadhi ya wanasiasa wa CUF Zanzibar wamekamatwa na kuhojiwa kwa madai ya kuwatusi viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Vilevile, imeelezwa kuwa Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alikuwa anatafutwa kuunguanishwa na wenzake.

Tukio la Mdee

Mdee alikamatwa juzi baada ya polisi kuizingira nyumba yake na kuondoka naye hadi Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam ambako alikataliwa dhamana na kulala rumande akihusishwa na vurugu zilizotokea Jumamosi katika mkutano wa uchaguzi wa Meya wa Jiji ulioahirishwa kwa amri batili ya Mahakama.

Katika tukio hilo ambalo pia madiwani watatu wa chama hicho walikamatwa, limeelezwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa ni mkakati unaolenga kuwaweka ndani madiwani wa Ukawa ili baada ya hapo uitishwe uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam na kuiwezesha CCM kushinda nafasi hiyo kwa bao la mkono.

Jana, polisi walikwenda nyumbani kwa Mdee wakiongozana naye na kupekua nyumbani kwake na baadaye kwenye ofisi yake, Kinondoni ikielezwa walikuwa wanatafuta nyaraka za Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam zilizopotea wakati wa vurugu.

Baada ya upekuzi huo, polisi walimrejesha mbunge huyo Kituo Kikuu cha Polisi ambako pia Waitara alikuwa anashikiliwa, huku taarifa zikisema dhamana ilikuwa imezuiliwa hivyo wangelala rumande. Mpaka tunakwenda mitamboni wabunge hao walikuwa bado polisi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala tukio hilo lilikotokea, Lucas Mkondya alipoulizwa alimtupia mpira Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro ambaye hata hivyo, alipopigiwa simu mara tatu alijibu yuko kwenye kikao.

‘Figisufigisu’ Kilombero

Wakati hayo yakiendelea jana, ‘figisufigisu’ nyingine ilikuwa inaendelea Kilombero, ambako polisi walimkamata mbunge wa jimbo hilo (Chadema), Peter Lijualikali kwa madai ya kutaka kuingia katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kuapisha na kuchagua mwenyekiti na makamu wake wakati si mpigakura.

Lijualikali alikamatwa nje ya ukumbi wa halmashauri na polisi na kuswekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Kilombero saa 3.48 asubuhi wakati akiingia kwenye ukumbi huo kama mmoja wa mashuhuda.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilombero, Shabaan Mikongolo alisema mbunge huyo hakutendewa haki na polisi kwa kuwa alifika eneo hilo kushuhudia matukio ya kuapishwa kwa madiwani.

“Ni kama kuna maelekezo yalitolewa kwa polisi kuwazuia wabunge, Lijualikali na Devotha Minja (Viti Maalumu – Chadema) na mwakilishi wa Katibu Mkuu Chadema kutoingia ukumbini lakini viongozi wengine wa Serikali ngazi ya mkoa na wilaya waliruhusiwa.

Pia, polisi walizuia waandishi wa habari wakiwamo wa Mwananchi na kutaka kuwanyang’anya kamera kwa sababu ambazo hazijawekwa bayana. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro hakupatikana kueleza sababu za hatua hizo.

Mazrui, wengine 34 wasakwa

Matukio mengine ya polisi kuwakamata wapinzani yameripotiwa Zanzibar na jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui aliitwa na Polisi Zanzibar, ikielezwa kuna mambo yanamhusu.

Hii ni mara ya pili kwa Mazrui kuitwa polisi tangu kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, huku CUF ikidai kuwa huo ni mwendelezo wa mkakati maalumu dhidi ya viongozi wa chama hicho.

Jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Maalim Hamad Masoud Hamad alidai kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya kisiasa ya kutaka kumkamata kila kiongozi wa juu wa CUF kuelekea uchaguzi wa marudio.

“Kwa viongozi wa CUF hili halishangazi, nahisi ingelikuwa ni hatua ya kushangaza sana iwapo wanaoitwa kuhojiwa na polisi ni viongozi wa vyama vingine. Sisi upande wetu hili ni jambo la kawaida mno na watu wasishangae,” alisema.

Mazrui ambaye pia alikuwa Waziri wa Biashara na Uwekezaji, ametakiwa kuripoti Makao Makuu ya Polisi, Ofisi ya Upelelezi Ziwani mjini hapa kesho saa 2.00 asubuhi na kuonana na mkurugenzi wa makosa ya jinai Zanzibar.

Polisi Zanzibar imethibitisha kuwapo wito huo ikisema kuna mambo muhimu yanayomhusu mwanasiasa huyo.

Viongozi wengine wa CUF waliowahi pia kuhojiwa na polisi katika kipindi hicho ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Ali Shehe na Kiongozi wa Mkakati wa Ushindi, Mohamed Sultan Mugheir ‘Eddy Riyami’ ambaye yuko nje kwa dhamana.

Juzi, gazeti hili liliripoti taarifa ya polisi visiwani humo kuwasaka watu 34 kwa tuhuma za kuwakashifu viongozi wakuu wa SMZ.

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi alisema kundi hilo limekuwa linatumia mitandao ya kijamii kuandika maneno na kutoa ‘clip’ za sauti za matusi dhidi ya viongozi hao.

Alisema tayari mtu mmoja, ‘Eddy Riyami’ alikamatwa na kuhojiwa kisha kuachiwa kwa dhamana.

Imeandikwa na Hassan Ali, Suzan Mwillo na Juma Mtanda.

No comments: