Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuondoa majina ya watumishi hewa wanaolipwa mishahara na taasisi hiyo nyeti ya fedha, Gavana wake, Profesa Benno Ndulu amesema anahitaji kujiridhisha kabla ya kutekeleza agizo hilo.
Rais Magufuli alifanya ziara hiyo juzi ambapo alikutana na viongozi waandamizi wa benki hiyo na kuwapa maagizo kadhaa ambayo alitaka yafanyiwe kazi mara moja, ili kuongeza ufanisi wa chombo hicho cha umma katika masuala ya fedha na uchumi.
Pamoja na maagizo mengine aliyotoa kwa watendaji hao wa BoT, Rais Magufuli alitaka kuhakikiwa kwa watumishi wa taasisi hiyo ambao jumla yao kwa sasa ni 1,391 suala ambalo alilieleza kuwa haliwezekani kuwa na uhalisia kwa utekelezaji wa majukumu ya kila siku kwa ofisi hiyo.
Kufuatia agizo hilo, Profesa Ndulu alisema analazimika kukutana na watendaji wenzake ili kujadili kwa mapana na kuyabaini majina yote ambayo Rais aliyazungumzia, kabla utekelezaji wa agizo lake haujafanywa.
“Wiki ijayo nitakuwa na kikao cha kujiridhisha. Rais hajatuachia nakala ya watumishi hewa aliowazungumzia, hivyo ni lazima tuwatafute kutoka kwenye kanzidata yetu. Tukishawapata ndipo tutajua namna sahihi ya kutekeleza agizo hilo,” alisema Profesa Ndulu jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili.
Gavana huyo alifafanua kuwa kutokana na wigo wa maagizo ya Rais, utekelezaji wake unapaswa kufanywa kwa hatua ili kufikia lengo lililokusudiwa, bila kusababisha madhara yasiyotarajiwa.
Alibainisha: “Maagizo yake ameyatoa kwa taasisi mbalimbali zinazohusiana na BoT hivyo ni lazima tujipange kuyatekeleza kwa umakini. Kila kitu kitafanyiwa kazi kwa wakati ndani ya muda unaostahili.”
Wakati akitoa maelekezo hayo kwa wahusika, Rais Magufuli alitahadharisha kuwa kama utaratibu huo wa kuwalipa watu wasio na majukumu yoyote ndani ya benki hiyo uliwezekana kabla yake, mwisho umefika wa kila mmoja kula kutokana na kazi za mikono yake.
Licha ya suala la watumishi, Rais Magufuli aliagiza kusitisha kulipa malimbikizo ya malipo ambayo tayari yalishaidhinishwa (Ex-Checker) na badala yake yarejeshwe Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uhakiki. Alisisitiza kuwa lengo si kuzuia bali kuwalipa wale tu wanaostahili.
Alitoa agizo hilo ikiwa tayari BoT imeshaidhinisha Sh925.6 bilioni baada ya kupata kibali cha wizara husika.
Vilevile aliagiza kitengo cha madeni ya nje ambacho awali kilikuwa BoT kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Fedha, kirejeshwe Benki Kuu mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa fedha hizo ambazo mara nyingi huelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Tangu aingie madarakani Novemba 5 mwaka jana, Rais aliweka msisitizo kwenye ukusanyaji wa mapato huku akidhibiti matumizi yasiyo ya lazima ili kuboresha huduma za umma.
Kutokana na nia hiyo, utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umeongezeka kwa mwezi, tofauti na ilivyokuwa hapo awali huku mabilioni ya shilingi yakiokolewa na kuelekezwa kwenye huduma za jamii kama afya na elimu.
3 comments:
Ningemshauri Prof arudi World Bank ambapo alikuwa anafanya kazi kabla ya kuwa Gavana.Aachane na hao maCCM na mfumo wao mmbovu. Wakati wa kampeni CCM walimlazimisha Prof kuidhinisha mabilion ya fedha kwenda kwenye kampeni zao ili Maguful achaguliwe mpaka wakaikausha hazina ya nchi, LEO hii wanajifanya wanashangaa eti kuna majipu BOT. MaCCM inatakiwa warudishe kwanza zile fedha walizochukua kwa ajili ya Kampeni maana hilo ndiyo JIPU namba moja kama kweli wanamapenzi na nchi na siyo kumzunguka Prof wakati wao na watoto wao ndiyo chanzo kizima cha matatizo BOT....
Kwa msingi huo unakinzana na kauli ya Rais na hujiulizi muda wote ulikuwa wapi kufuatilia hayo, sisi wananchi tunaelewa wazi kabisa uajiri wa ofisi hiyo na nyinginezo uanavyofanyika kwa wenye sauti tuu. Hapo kuna madudu mengi na utayatambua kama ulikuwa hujui?! Vinginevyo subiria utumbuliwe wewe kwanza.
Yaani unabishana na mkubwa wako wa kazi hujajua kama wewe ni mojawapo ya majipu ya tangu enzi za utawala uliopita na umekali majipu ndani ya ofisi yako, Au unasubili tukutajie mmoja mmoja>> Huu uajiri wa kuletewa vikaratasi na kuajiri inabidi ufee!!! Undugu-Nization!!
Post a Comment