ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 12, 2016

SERIKALI YA TANZANIA NA NORWAY ZASAINI MAKUBALIANO KUWEZESHA WAHANDISI WANAWAKE WANAOHITIMU VYUO VIKUU

Mwenyekiti wa Bodi ya Wahandisi nchini Prof. Ninatubu Lema (kulia) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Tone Skogen (kushoto) wakisaini Makubaliano ya Awali ya Programu ya kuwasaidia na kuwaendeleza Wahandisi wanawake walioko vyuoni yenye lengo la kuongeza idadi ya Wahandisi waliosajiliwa kwa ngazi ya Ushauri.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wahandisi nchini Prof. Ninatubu Lema (kulia) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Tone Skogen (kushoto) wakibadilishana Hati za Makubaliano ya Awali ya Programu ya kuwasaidia na kuwaendeleza Wahandisi wanawake walioko vyuoni yenye lengo la kuongeza idadi ya Wahandisi waliosajiliwa kwa ngazi ya Ushauri leo jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Tone Skogen (Katikati) kuhusu Mafanikio wanayoyapata Wahandisi Wanawake wa Tanzania kutokana na msaada wa Mafunzo ya kuwasaidia na kuwaendeleza Wahandisi wanawake walioko vyuoni kutoka Serikali ya Norway.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akijadiliana jambo na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne –Marie Kaarstad wakati wa kusaini Makubaliano ya Awali ya Programu ya kuwasaidia na kuwaendeleza Wahandisi wanawake walioko vyuoni yenye lengo la kuongeza idadi ya Wahandisi waliosajiliwa kwa ngazi ya Ushauri leo jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wahandisi Nchini (ERB) Prof. Ninatubu Lema akieleza mafanikio ya uhusiano mwema kati ya Tanzania na Norway katika kusaidia Wahandisi Wanawake walioko nchini.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Tone Skogen (katikati), akiwa na baadhi ya Wahandisi Wanawake walionufaika na Programu ya kuwasaidia na kuwaendeleza Wahandisi wanawake walioko vyuoni na baadhi ya Viongozi wa ERB.
Msajili wa Wahandisi (ERB) Eng. Steven Mlote akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa Ushirikiano katika masuala ya Uhandisi kati ya ERB na Serikali ya Norway.

Serikali ya Tanzania na Norway zimesaini makubaliano yatakayowawezesha Wahandisi wanawake wanaohitimu na kufaulu masomo yao katika vyuo vikuu nchini kujengewa uwezo kupitia mafunzo kwa vitendo katika makampuni mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo katika fani hiyo.

Pia makubaliano hayo yatawawezesha wahitimu hao kusajiliwa na na Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), kupata ajira kwenye makampuni na taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na ujenzi pamoja na kujengewa uwezo wa kuanzisha makampuni yao wenyewe.

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa Makubaliano hayo jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani ameishukuru Serikali ya Norway kwa kuonyesha njia kwa kuwa msaada utakaotolewa na Serikali hiyo utasaidia kuboresha maisha ya wanawake wahandisi wanaohitimu vyuo vikuu kote nchini.

Amesema kupitia makubaliano hayo Norway itatoa fedha za awamu ya pili ili kuwezesha Programu hiyo kutekelezwa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutoa kiwango cha gharama halisi itakayotolewa na Serikali hiyo kufuatia mchanganuo utakaotolewa na watalaam.

"Leo tumesaini makubaliano ya awali kati ya Serikali ya Norway na Tanzania kupitia Bodi ya Usajili wa wahandisi kuwasaidia wanafunzi wa kike wanaomaliza vyuo vikuu hapa nchini katika Fani ya Uhandisi ili waweze mafunzo kwa vitendo ili kuwawezesha kupata Usajili wa Bodi hiyo", Ameeleza Eng.Ngonyani.

Amesema programu hiyo imejirudia baada ya ile ya kwanza kukamilika ambayo Norway ambapo Serikali hiyo ilitoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 2 kusaidia mpango huo na kuongeza kuwa fedha zilizotolewa zimewanufaisha wahandisi wanawake wapatao 297 hivyo kuchangia kukuza ajira nchini.

Aidha, amesema kupitia mfumo huo ERB huwatafutia nafasi za mafunzo kwa vitendo wahitimu hao kwa waajiri mbalimbali wenye makampuni yaliyosajiliwa yenye wahandisi washauri ambao hupewa jukumu la kuwasimamia hadi wanapohitimu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Tone Skogen akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo amesema kuwa Serikali ya Norway imeridhishwa na kufurahishwa na juhudi za kuongeza Wahandisi wanawake inayofanywa na Serikali kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB).

Amesema hatua hiyo ya Serikali ya Tanzania kutoa udahili kwa wanafunzi Wahandisi Wanawake wengi ni moja ya juhudi za kuimarisha jamii na uchumi wenye nguvu kama ilivyofanyika nchini Norway kuanzia mwaka 1970.

Bi. Skogen amebainisha kuwa kupitia mafanikio yaliyooneshwa na Serikali ya Tanzania Norway itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania ( ERB) kuhakikisha kuwa Wahandisi Wanawake Tanzania wanachangia kukuza uchumi wa Tanzania.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Prof.Ninatubu Lema akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo ameishukuru Serikali ya Norway kwa ushirikiano inaouonyesha wa kuwasaidia Wanawake wanaosomea na kuhitimu fani ya Uhandisi.

Amesema kupitia Programu hiyo Wahandisi wanawake Tanzania ambao wako vyuoni na wale wanaohitimu mafunzo wanapata hamasa ya kuendelea kufanya vizuri zaidi kutokana na mchango wao kutambuliwa na kuthaminiwa katika jamii tofauti na miaka iliyopita.

"Ninakumbuka mwaka 1970 wakati Chuo Kikuu cha Dar es salaam kilipoanzisha kitivo cha Uhandisi kulikua kulikua na akina mama wachache sana kikiwa na wahandisi wanawake 2 tu mwaka 1978, sasa hivi hali hii imebadilika, sasa kuna mwamko mkubwa huu ni ushahidi tosha wa maendeleo ya fani ya uhandisi nchini" Amebainisha Prof. Lema.

Amesema programu hiyo imesaidia kuwahamasisha wanafunzi wanawake walio vyuoni na shule za sekondari kufanya vizuri kwa kuwa mara baada ya kuhitimu masomo ya Uhandisi na kufanya vizuri hupewa ufadhili kupitia programu hiyo ili waweze kutambuliwa na kusajiliwa.

Amesema kwa sasa Tanzania inahitaji Wahandisi wengi kwa kuwa mkakati uliopo ni kuifanya Tanzania iwe nchi ya uchumi wa Kati ambayo uchumi wake utategemea uanzishwaji wa viwanda ambavyo ufanisi na uendeshaji wake utategemea Wahandisi waliopo nchini.

Aidha, amesisitiza kuwa suala la usawa wa kinjinsia katika udahili wa Wahandisi wanawake kwenye mafunzo linapewa kipaumbele na Bodi hiyo kwa kutoakana na matunda mazuri yanayoonyeshwa na Wahandisi wanawake kupitia kazi wanazopewa kwa kuwa huzifanya kwa ubora na viwango.

No comments: