Shahidi wa sita katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, ameieleza mahakama jinsi alivyosafirisha bunduki, risasi mbili, bahasha yenye alama za vidole na picha ya gari alivyochukua kwenye eneo yalipotokea mauaji hayo.
Kauli hiyo aliitoa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, wakati akitoa ushahidi mbele ya Jaji Sirilius Matupa wa mahakama hiyo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Ajuaye Bilishanga, shahidi huyo, ambaye ni Ofisa Upelelezi wa Polisi, Salama Ally (36) alidai kuwa kabla ya kutuma vielelezo hivyo, alipiga picha gari na kuchukua alama za vidole kwa kutumia unga maalumu kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Sehemu ya mahojiano kati ya shahidi huyo katika kesi ya mauaji namba 192 ya mwaka 2014 inayowakabili watuhumiwa saba chini ya kifungu 196 na 197 cha sheria ya kanuni za adhabu na Wakili wa Serikali Bilishanga yalikuwa kama ifuatavyo:-
Shahidi: Nilipigiwa simu na RCO Tono, mwezi mmoja zaidi kwamba nijiandae kwa ajili ya kusafirisha ushahidi ule kuupeleka makao makuu ya upelelzi Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi.
Wakili: Unaweza kukumbuka ilikuwa lini ulipoitwa ofisini kusafirisha ushahidi huo.
Shahidi: Ndiyo nakumbuka
Wakili: Hebu iambie mahakama ilikuwa tarehe ngapi.
Shahidi: Ilikuwa Desemba 6, 2012
Wakili: Ulisafirisha ushahidi gani?
Shahidi: Nilisafirisha bunduki moja, risasi mbili, picha za gari na alama za vidole nilizochukua (dusting powder).
Wakili: Tuambie uliusafirishaje ushahidi huo.
Shahidi: Nilisindikizwa na gari la polisi likiwa na maaskari kadhaa mpaka Uwanja wa Ndege wa Mwanza, waliponifikisha walirudi nami nilipanda ndege na kuondoka kuelekea Dar es S alaam. Niliposhuka Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam nilipokelewa na polisi wengine tukaenda hadi makao makuu ya uchunguzi nikakabidhi ushahidi huo mimi nikarudi Mwanza.
Wakili: Baada ya kurudi Mwanza nini kiliendelea?
Shahidi: Niliendelea na kazi zangu kama kawaida.
Wakili: Hata siku moja hukuwahi kufuatilia ujumbe uliokuwa umeupeleka makao makuu Dar es Salaam
Shahidi: Mimi mwenyewe sikufuatilia, ila haikuchukua muda mrefu kabla ya kujulishwa kwamba natakiwa kufuata majibu ya ushahidi niliopoleka.
Wakili: Ulipoleta hayo matokeo ya ushahidi ulimkabidhi nani?
Shahidi: Nilimkabidhi RCO Tono,
Wakili: Umetwambia kuwa wewe ndiye ulipiga picha ile gari na kuchukua alama za vidole, kwani wewe umeyasomea mambo ya picha?
Shahidi: Ndiyo, nilichukua takribani miezi mitatu kusomea mambo ya upigaji picha katika chuo kimoja huko visiwani Zanzibar.
Wakili: Hapo chuoni mlifundishwa aina hiyo ya poda (dusting powder) na mbinu zinazotumika kuchunguza alama za vidole.
Shahidi: Hapana sikuisomea chuoni bali nimeisomea nikiwa mafunzo ya Kipolisi husani nilipohamia kitengo cha upelelezi.
Shahidi wa saba katika shauri hilo, Lameck Mgeta (20), mkazi wa mtaa wa Lumumba jijini Mwanza aliieleza mahakama hiyo jinsi alivyomshuhudia mshtakiwa wa kwanza akifika kituoni kwa ajili ya kumuwekea dhamana ndugu yake.
Sehemu ya mahojiano kati ya wakili Bilishanga yalikuwa kama ifuatavyo:-
Wakili: Elezea mahakama Oktoba 13, 2012 ulienda polisi kufanya nini?
Shahidi: Nilienda kumdhamini mdogo wangu alikuwa amekamatwa, yuko pale polisi mjini kati.
Wakili: Ulipofika polisi ulikuta kitu gani kinaendelea?
Shahidi: Niliwakuta watu wengi wakiwa kwenye foleni.
Wakili: Wewe ulipofika uliambiwa ufanye nini?
Shahidi: Niliambiwa nipange mstari kusubiri watu wapungue
Wakili: Katika watu hao, humu ndani yupo mtu uliyemuona siku hiyo kwenye foleni siku hiyo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Unaweza kuionyesha mahakama hii mtu huyo?
Shahidi: Ndiyo naweza (aliamka kwenda kumgusa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Muganyizi Peter).
No comments:
Post a Comment