Msimamizi wa mradi wa uchimbaji wa visima vya maji katika Shule ya Msingi Mbagala majimatitu kutoka DAWASA Muhandisi Abel Chibelela akiangalia maendeleo ya kisima kimoja kati ya viwili vinavyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) katika shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 24.5.
Wataalam kutoka Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) wakiendelea kuchimba kisima chenye urefu wa mita 130 katika shule ya Msingi Mbagala majimatitu, Temeke jijini Dar es salaam.
Msimamizi wa mradi wa uchimbaji wa visima vya maji katika Shule ya Msingi Mbagala majimatitu kutoka DAWASA Muhandisi Abel Chibelela na Mhandisi Elizabeth Kingu, Katibu Tawala Msaidizi Huduma za Maji (kushoto) wakiangalia maendeleo ya moja ya kisima kinavyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) katika shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 24.5.
Na. Aron Msigwa –Dar es salaam.
Walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbagala Majimatitu iliyoko Temeke jijini Dar es salaam watanufaika na huduma ya maji safi kufuatia Serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 24.5 kwa lengo la kufanikisha mradi wa uchimbaji wa visima viwili kwa lengo la kuboresha taaluma na mazingira ya shule hiyo.
Akizungumzia uchimbaji wa visima hivyo leo jijini Dar es salaam msimamizi wa mradi huo kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) Muhandisi Abel Chibelela amesema kuwa kuchimbwa kwa visima hivyo ni utekelezaji wa agizo la Serikali kuitaka DAWASA kutafuta vyanzo vya maji katika shule hiyo ili kuwaondolea adha ya uhaba wa Maji.
Amesema shule hiyo imekuwa na tatizo hilo kufuatia kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wapatao 6000 inayozidi uwezo wa miundombinu iliyopo sasa ikiwemo kisima kinachotumiwa na wanafunzi hao kinachozalisha lita 8000 kwa siku wakati mahitaji halisi ya maji ni Lita 40,000 kwa siku.
Amesema Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kupitia Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa ( DDCA) ilipewa jukumu la kuchimba visima viwili vya shule hiyo kwa thamani ya shilingi milioni 24.5 zikiwa ni gharama za uchimbaji, usafishaji wa visima hivyo na gharama za vipimo vya maabara ili kuangalia ubora wa maji hayo.
No comments:
Post a Comment