ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 14, 2016

VIGOGO WA RAHACO WAFIKISHWA MAHAKAMANI


Waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), wakielekea chumba cha wazi cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo walipofikishwa kwa tuhuma za makosa ya kutumia vibaya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shs. Bilioni 6. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa (RAHCO), Mhandisi Benhard Tito, Kanji Mwinyijuma na Emmanuel Masawe. (Picha na Francis Dande) 
Mkurugenzi Mkuu wa (RAHCO), Mhandisi Benhard Tito akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi wakati akiingia mahakamani.
Afande akimuelekeza mtuhumiwa.....
Waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo, walipofikishwa kwa tuhuma za makosa ya kutumia vibaya madaraka na kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya shs. Bilioni 6. Kutika kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa (RAHCO), Mhandisi Benhard Tito, Kanji Mwinyijuma na Emmanuel Masawe. (Picha na Francis Dande) 

Na Mwandishi Wetu

VIGOGO wa tatu waliowai kutumbuliwa ‘majipu’ na Rais John Magufuli kutoka Kampuni ya Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), wamepandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka nane likiwemo la kusababisha hasara ya dola za kimarekani 527, 540.

Vigogo hao waliotumbuliwa mwishoni mwa mwaka 2015 walifikishwa mahakamani hapo jana wakiwa chini ya ulinzi mkali, kwa ajili ya kusomewa mashtaka yao nane yanayowakabili.

Vigogo hao ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya (RAHCO), Mhandisi Benhard Tito, Raia wa Kenya anayedaiwa kuwa dalali wa zabuni, Kanji Myinyijuma na Emmanuel Massawe ambaye yupo ndani ya bodi hiyo. Washtakiwa hao kwa pamoja walisomewa mashtaka yao leo mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba, ambapo

Wakili wa Serikali Thimos Vitalis alidai kuwa shauri hilo ni jipya. Alidai kuwa shtaka la kwanza la kula njama kwa ajili ya kutenda kosa linawakabili washtakiwa wote, ambapo inadaiwa kati ya Septemba mosi 2014 na Septemba 30, 2015 katika jiji la Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa kinyume cha sheria ya rushwa ya mwaka 2007.

Kosa la pili linalomkabili mshtakiwa wa kwanza Tito ni matumizi mabaya ya madaraka. Mwanasheria Vitalis alidai kuwa kosa hilo lilitendwa Februari 27, 2015 katika ofisi za RAHCO zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam baada ya kuhidhinisha Kampuni ya

Rothschild (South Africa) Property kuwa mshauri katika mpango wa ujenzi wa reli ya kati bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya Kmapuni hiyo. Mbali na hilo, shtaka la tatu linamkabili Tito na Massawe ya kutumia madaraka yao vibaya wakati wakiwa wanaitumikia Rahco.

Inadaiwa kwa pamoja Machi 12, 2015 katika ofisi za Rahco Ilala jijini Dar es Salaam akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni na Katibu wa Rahco walisaini barua ya kuhalalisha Kampuni ya Rothschild (South Africa) Property katika mchakato wa kutoa huduma ya ushauri wa kifedha katika ujenzi wa reli hiyo ya Kati bila kuidhinishwa na bodi.

Pia washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la nne, ambapo inadaiwa Kati ya Machi 12 na Mei 20, 2015 wakiwa ofisini kwao Ilala Dar es Salaam waliacha majukumu yao kwa kushindwa kuwasilisha mkataba wa Kampuni ya Rothschild kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Pia wanakabiliwa na shtaka la tano, ambapo inadaiwa Mei 20, 2015 katika ofisi zao hizo zilizopo Ilala, walishindwa kutekeleza majukumu yao na kutumia vibaya madaraka kwa kusaini mkataba na kuingia makubariano na kampuni hiyo katika masuala ya ushauri.

Katika shtaka la sita Wakili Vitalis alidai kuwa, pia washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.Inadaiwa kwa pamoja Katik ya Mei 20 na June 20, 2015 katika ofisi ao zilizopo Ilala walishindwa kuwasilisha ‘Copy’ za mkataba wa makubaliano wa kampuni hiyo na Kampuni ya Reli kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkaguzi wa ndani na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mbali na hilo, shtaka la saba linawakabili washtakiwa wote ambapo inadaiwa kusababisha hasara, kosa hilo wanadaiwa kulitenda Kati ya Machi mosi na Septemba 30, 2015 katika ofisi zao zilizopo Ilala Dar es Salaam. Inadaiwa kuwa wakiwa na mwakilishi wa kampuni hiyo na Katibu wa Rahco kwa pamoja walikubalianakuidhinisha makubaliano ya kampuni hiyo katika masuala ya kiushauri na kuisababisha hasara ya dola za Kimarekani 527, 540 Kampuni ya Hodhi ya Reli Tanzania ambazo zilishalipiwa kiwango cha awali benki.

Shtaka la mwisho linamkabili mshtakiwa wa kwanza, Tito kwa matumizi mabaya ya madaraka kinyume na sheria ya kupambana na rrushwa, ambapo inadaiwa Agosti 18, 2015 katika ofisi za Rahco Ilala alitumia nafasi yake vibaya kwa kutoa zabuni ya upendeleo kwa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya China Construction Corporatio.

Inadaiwa katika zabuni hiyo kampuni ilipewe ujenzi wa reli ya Kilometa 2 yenye kiwango cha kisasa kuanzia Soga ikiwa na thamani ya dola za kimarekani 2, 312, 229.39 bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya Reli.Baada ya kueleza hayo, Wakili Vitalis aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo anaomba kupangiwa tarehe kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo, jambo lililoibua mvutano wa kisheria kutoka upende wa utetezi. Kutokana na kuibuka kwa mvutano wa kisheria, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadio Machi 18, mwaka huu kwa ajili ya kutoa maamuzi kama washtakiwa watapewa dhamana ama la.

No comments: