Dar es Salaam. Jopo la madaktari 33 kutoka Israel, wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto 34, kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Upasuaji huo ulifanyika baada ya kitengo hicho kupokea msaada wa Sh222 milioni wiki mbili zilizopita, kutoka kampuni ya BAPS Charity ili kusaidia upasuaji wa watoto 101 kati ya 500 wanaohitaji huduma hiyo.
Akizungumza jana na waandishi wa habari daktari bingwa wa utambuzi wa magonjwa ya moyo kwa watoto, Assa Sagi kutoka Israel, alisema baadhi ya watoto hao wamefanyiwa upasuaji mdogo ili kuchunguzwa na iwapo watabainika kuwa na tatizo watafanyiwa upasuaji mkubwa.
“Wapo tuliobaini kwamba matundu yao yanaweza kupona baada ya kuingiza vipimo vinavyobaini ukubwa wa tundu husika, na tumebaini kwamba kwa wao si lazima wafanyiwe upasuaji, bali tumerekebisha matundu hayo,” alisema Dk Sagi.
Akizungumzia mafanikio ya upasuaji huo, Mkuu wa Kitengo cha Moyo, Profesa Mohamed Janabi alisema mpaka sasa watoto 34 wamefanyiwa upasuaji huo. Wengine 67 waliobaki watafanyiwa awamu ijayo.
Profesa Janabi alisema walibaini watoto wengi wenye matatizo ya moyo hucheleweshewa huduma na tatizo kukua.
Upasuaji huo ulioanza kufanyika Machi 7, ulihusisha madaktari bingwa 10 kutoka Hospitali ya Muhimbili na madaktari hao wa Israel waliopiga kambi ya siku tatu kufanya upasuaji huo.
Naye Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kambi za upasuaji zimesaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje na kuokoa gharama za Serikali, kwa sababu idadi ya wagonjwa waliopata rufaa imepungua kutoka 198 hadi 89 kati ya mwaka 2013 na Novemba 2015.
No comments:
Post a Comment