Katibu huyo atatangazwa katika viwanja vya hadhara vya Furahisha, jijini hapa, kwenye mkutano wa hadhara utakaofanyika keshokutwa na kuhutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema jina hilo litapatikana kesho, Baraza Kuu la chama linalotarajiwa kufanyika kesho.
Baraza hilo, pamoja na mambo mengine, litatathmini kwa kina mwenendo wa chama hicho baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
“Katibu Mkuu mpya wa chama chetu atajulikana katika mkutano wa hadhara utakaofanyika keshokutwa, baada ya jina lake kupenya katika mkutano mkuu wa chama utakaofanyika jijini Mwanza,” alisema Makene.
Makene aliongeza kuwa Dk. Slaa hawezi kipimo au kigezo cha kumpata katibu mkuu mpya kwa kuwa Chadema ni taasisi yenye vigezo vyake, hivyo hawapeani vyeo bali wanakabidhiana majukumu ndani ya chama.
“Tunao watu wenye uwezo na vigezo wengi wenye kuweza kuhimili nafasi hiyo ya katibu mkuu,” alisema.
Aidha, Makene alikanusha taarifa za kuwapo makundi ndani ya chama hicho kutokana na upinzani mkali wa nafasi hiyo kwa kuwa wapo wanaohofia mwenyekiti Mbowe, anaweza kupendekeza jina la rafiki yake hali ambayo alisema Mbowe ni rafiki wa kila mtu na pia ni mlezi wa chama.
Makene alisema suala la kumpata katibu mkuu si la upendeleo wala kampeni, bali ni kanuni zinazompa mamlaka mwenyekiti kikatiba, kupendekeza majina mawili au moja litakalopitishwa na Baraza Kuu.
Hata hivyo, alisema mpaka sasa majina mawili ya watu wanaotarajiwa kupendekezwa, hayajajulikana kwa kuwa ni siri ya mwenyekiti, ambaye atayawasilisha mbele ya mkutano mkuu wa chama.
Nafasi ya katibu mkuu wa chama hicho, hivi sasa inakaimiwa na Salum Mwalimu tangu kujiengua kwa Dk. Slaa, kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment