Thursday, March 3, 2016

Watu saba wa familia moja wafa maji Ziwa Victoria

By Twalad Sulum, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Misungwi. Watu saba wa familia moja wamekufa maji na wengine wanne kunusurika baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama Ziwa Victoria wilayani hapa Mkoa wa Mwanza.

Familia hiyo ya watu 11 ilikuwa ikisafiri kutoka Kijiji cha Lubili wilayani Misungwi kwenda kwenye kikao mkoani Geita.

Mmoja wa walionusurika kwenye ajali hiyo, Juma Maguta (50), alisema ajali hiyo ilitokea Jumanne wiki hii baada ya mtumbwi huo kupigwa na dhoruba.

“Hali ya hewa Ziwa Victoria ilikuwa shwari, tulipofika katikati upepo mkali ulizuka na mtumbwi kupigwa na mawimbi mawili na kuzama,” alisema Maguta.

Alisema baada ya mtumbwi huo kuzama, watu wanne kati yao, walipiga mbizi na kufanikiwa kujiokoa, huku wengine wakizama na kufa.

Maguta alisema yeye na wenzake watatu waliokolewa na boti ya wavuvi iliyokuwa ikitokea Geita. Aliwataja wengine walionusurika kuwa ni Silvanus Charles (39), Ngabo Ngalu (39) na Vena Ramadhani (40), wakazi wa Lubili.

Waliokufa ni pamoja na mtoto wa miaka mitatu, Elizabeth Kasanga, mama yake, Kahabi Maguta (28), Agnes Ngalaba (20) na mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Lubili, Leary Masalu (31).

Wengine ni Juliuss Masalu (40), Hai Dotto (30) na Machibya Masanyiwa (45).

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mwajuma Nyiruka alifika nyumbani kwa wafiwa kuwafariji na kupiga marufuku vyombo vya usafiri majini visivyokaguliwa na kuthibitishwa na mamlaka husika kusafirisha abiria.

Aliwaagiza viongozi wa kata na vijiji wilayani hapa kusimamia utekelezaji wa amri hiyo ili kunusuru maisha ya watu wanaosafiri katika ziwa hilo.

No comments: