Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku uingizaji wa mifugo kutoka nje ya nchi kutafuta malisho katika ranchi za ndani kwa sababu ni chanzo cha migogoro ya ardhi kwa wananchi waishio mipakani.
Waziri Mkuu alimtaja Ofisa Mifugo wa Kata ya Kakunyu, mkoani hapa, Eric Kagoro kuwa anahusika na uingizwaji wa mifugo hiyo ya nje nchini.
Katika sakata hilo, Waziri Majaliwa aligundua kuwa kuna ng’ombe zaidi ya 291, wanaotoka mikoa ya jirani wanalishwa kwenye ranchi ya mifugo ya Misenyi.
Alibaini kuwa ng’ombe 291 waliokamatwa katika ranchi ya Misenyi ni wa rafiki yake na ofisa huyo na ndiye aliyetoa kibali cha mifugo hiyo kulishwa.
“Nimeambiwa wale ng’ombe waliokamatwa ni wa rafiki yako na wewe ndiye ulitoa kibali waje kulishwa kwenye ranchi hii. Siyo kazi yako kuruhusu mifugo ya nje ije kulishwa hapa kwenye ranchi,” alisema na kuongeza:
“Leo Nimekusamehe. Kazi yako ni kuhakikisha mifugo ya kwenye kata hii iko salama. Kazi yako ni kuwasaidia wafugaji wa kata hii wafuge vizuri.”
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa watendaji wa kata na vijiji kutotumia nafasi zao kusababisha migogoro baina ya watu wa nje na wanaowaongoza.
Aliwataka pia maofisa uhamiaji wawe makini na vyeti vya kuandikisha uraia wanavyovitoa kwa wananchi wanaoishi mipakani, kwani imekuwa ni mianya ya kuleta migogoro ya ardhi.
Alitoa agizo kuwa watafutwe watu wote walioingia nchini kwa mgongo wa vyeti hivyo, wakamatwe na kurejeshwa kwao.
Alibaini kuwa raia wa kigeni wanaoomba uraia, pia huleta wenzao kununua ardhi kwa kutumia vyeti vyao.
“Kuna watu wamekuja hapa nchini wakaomba vyeti, lakini wakikaa wanaleta wenzao waje kununua ardhi kwa kutumia mgongo wa vyeti hivyo,” alisema.
Kadhalika Waziri Mkuu alionya kuwa tatizo kama la Misenyi lipo pia Karagwe na kuwataka wahusika wajiandae kuchujwa na kuchukuliwa ardhi zao kama watakuwa hawajaendeleza ili wapewe Watanzania wenye uhitaji wa kulima na kufuga.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment