ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 24, 2016

BALAA! MAITI NYINGINE YAZIKWA, YAFUKULIWA

Maiti ya Mariki Kimario juzi ilifukuliwa na baadaye kuzikwa upya sehemu nyingine katika tukio jingine la kuchukua kimakosa maiti hospitalini.
Tukio kama hilo lililotokea takribani wiki mbili zilizopita kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), wakati ndugu walipochukua mwili kimakosa na kwenda kuuzika Usangi mkoani Kilimanjaro kabla ya watu wengine kupewa maiti ambayo si yao walipoifuata hospitalini hapo na kuibua tukio hilo.
Kutokana na tukio hilo MNH ililazimika kulipa gharama za mazishi kwa familia ambayo mwili wa ndugu yao ulizikwa na familia nyingine. Tukio hilo la juzi lilitokea mkoani Arusha ambako Jeshi la Polisi lililazimika kusimamia kufukuliwa kwa mwili huo kwenye Kijiji cha Elkisongo kilicho Kata ya Kidinga wilayani Arumeru. Katika tukio hilo, ndugu walioenda kuchukua maiti ya Leshai Ngoisaye, walipewa maiti ya Kimario na kwenda kuizika takriban kilomita 50 kutoka Arusha mjini.
Miili hiyo ilikuwa imehifadhiwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru. Wakizungumza na Mwananchi jana, baadhi ya ndugu wa Kimario walisema tukio hilo limesababishwa na kutokuwapo umakini kwa wafiwa na wahudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti. John Lesian, mmoja wa ndugu wa marehemu, alisema walikwenda kuchukua mwili wa ndugu yao juzi, lakini walipofika walionyeshwa mwili wa mtu mwingine.
Hali hiyo ilisababisha kuzuka kwa malumbano baina ya ndugu wa Kimario na wahudumu wa chumba hicho cha maiti.
“Maandalizi yote ya kuchukua mwili na kwenda kuzika Rombo yalikuwa tayari,” alisema ndugu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jeremiah Shirima.
“Baada ya hali hii ndugu walitoa taarifa polisi na ikajulikana mwili tayari ulishachukuliwa na kuzikwa na hivyo waliomba kwenda kuufukua.”
Muhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti wa hospitali hiyo, ambaye aliomba kutotajwa jina, aliwalaumu ndugu wa marehemu kuwa hawakuwa makini.
“Mimi si msemaji ila tukio limetokea na tayari mwili wa Kimario umefukuliwa na kurejeshwa na mwili wa Leshai Ngoisaye umechukuliwa na kuzikwa,” alisema
Mwenyekiti wa Kijiji cha Elkisongo alichokuwa anaishi Ngosaye, Lesiyoni Sikita alisema tayari wamefanya mazishi mengine baada ya kuzika kimakosa mwili wa Kimario.
Mkazi wa Kijiji cha Elkisongo, Samweli Ngalabali aliomba serikali kufanya tafiti kubaini sababu za kuongezeka kwa matukio hayo.
“Huu ni uzembe lazima serikali ichukuwe hatua,” alisema.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema ni kweli kuwa tukio hilo limetokea na wameanza kufanya uchunguzi kujua nini kilichosababisha maiti hizo kuchanganywa. Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Justin Urio alisema licha ya kuwa mochwari hiyo ilibinafsishwa na sasa inafanya kazi kwa zabuni lakini uongozi wa Hospitali nao unafanya uchunguzi kujua nini kilichotokea, hadi kupelekea maiti hizo kuchanganywa.

No comments: