
MAAZIMIO YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA CHAMA KATIKA KIKAO CHAKE CHA TAREHE 2 – 3 APRILI, 2016 KILICHOFANYIKA MAZSONS HOTEL, MJINI ZANZIBAR
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) limefanya kikao chake cha kawaida kwa siku mbili, tarehe 2 hadi 3 Aprili, 2016 mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama, Mheshimiwa Twaha Taslima.
Ajenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni Hali ya Kisiasa Zanzibar na mwelekeo wa CUF baada ya kufanyika kile kilichoitwa uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016.
Baada ya kupokea na kujadili kwa kina ajenda hiyo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:
1. Linawapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa ujasiri, uzalendo na ari kubwa walioionesha kwa kuitikia kwa kiasi kikubwa wito wa chama chao cha CUF wa kuwataka wasishiriki katika uhuni na ubakaji wa demokrasia uliopewa jina la uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016.
Baraza Kuu la Uongozi limefurahishwa kuona zaidi ya asilimia 80 ya wapiga kura wa Zanzibar hawakujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo haramu na batili, na hivyo kuudhihirishia ulimwengu kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina ridhaa ya wapiga kura hao.
2. Linawapongeza waliokuwa wagombea wa CUF kwa nafasi zote za Urais, Uwakilishi na Udiwani kwa kuheshimu maamuzi ya Chama na kutoshiriki uchaguzi haramu na batili wa marudio licha ya njama nyingi zilizokuwa zikifanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, za kulazimisha ushiriki wao. Msimamo wa wagombea hao umewadhihirishia na kuwathibitishia CCM kwamba tofauti na wao, viongozi wa CUF hawajali nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka ni kuleta mabadiliko ya kweli kwa maslahi ya watu wote wa Zanzibar.
3. Linawapongeza kwa namna ya pekee wagombea Urais, Uwakilishi na Udiwani wa vyama vyengine vya upinzani ambavyo ni UMD, JAHAZI ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP, na ACT-WAZALENDO, na vile vinavyoshirikiana kupitia UKAWA ambavyo ni CHADEMA, NCCR na NLD vilivyoungana na wananchi wa Zanzibar kususia uchaguzi haramu na batili wa marudio na kusimamia maamuzi halali ya wapiga kura waliyoyafanya kupitia uchaguzi mkuu halali wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
4. Linazishukuru na kuzipongeza jumuiya na taasisi zote za kitaifa na kimataifa pamoja na nchi rafiki za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zilikataa kuleta waangalizi wa uchaguzi katika uchaguzi huo haramu na batili na hivyo kuungana na Wazanzibari katika kutetea maamuzi yao halali waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu halali uliokuwa huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
5. Linavishukuru na kuvipongeza vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi pamoja na waandishi wa habari na wapiga picha kwa jinsi vilivyosaidia kuonesha ulimwengu uchaguzi mkuu uliokuwa halali, huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia kwa jinsi vilivyoanika uchafuzi wa tarehe 20 Machi, 2016 hasa kule kuonesha vituo vya kupigia kura vikiwa havina watu na hivyo kuwasaidia Watanzania na ulimwengu kuujua ukweli ambao CCM na Tume yao ya Uchaguzi walikuwa wakijaribu kuuficha.
6. Linalaani tabia na mwenendo wa uongo, uzushi, na uvunjwaji wa Katiba, Sheria na Maadili wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, dhidi ya matakwa na maamuzi halali ya Wazanzibari waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kitendo chake cha kuiingiza Zanzibar katika dimbwi la chuki, uhasama, uvunjifu wa haki za binadamu na udhalilishaji wa raia kwa sababu tu ya kukiridhisha chama chake cha CCM ambacho kimekataliwa na Wazanzibari.
Vitendo vya Jecha Salim Jecha vimeishushia hadhi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na kuichafulia jina Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbele ya jumuiya ya kimataifa na kuonekana haiko tofauti na nchi nyengine za Afrika zisizoheshimu matakwa na maamuzi ya wananchi katika uchaguzi.
7. Linalaani hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli kuleta nguvu kubwa ya vikosi vya ulinzi na usalama kuja kubaka demokrasia Zanzibar.
Baraza Kuu linalaani vikali nguvu kubwa iliyotumiwa na vyombo vya dola dhidi ya raia wasio na hatia kwa lengo na madhumuni ya kuwatisha na kuwazuia wasitumie haki zao za msingi kama ibada kwa kuwalazimisha kutotoka nje ya nyumba zao kuanzia saa 2 usiku wakati muda huo ni muda wa ibada ya sala kwa Waislamu ambao ni asilimia 99 ya wananchi wote wa Zanzibar.
Baraza Kuu pia linalaani mwenendo wa viongozi wa juu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa kutumika waziwazi kisiasa kwa kuegemea upande wa CCM na kuwakandimiza viongozi na wanachama wa CUF kinyume na maadili ya kazi zao.
8. Linalaani vitendo vya Serikali kuunda makundi ya kiharamia ambayo yamekuwa yakiwahujumu raia wasio na hatia yakitumia silaha za moto na silaha za kienyeji huku yakitumia gari za Idara Maalum za SMZ.
Baraza Kuu linalaani Jeshi la Polisi ambalo limekuwa likiyalinda makundi haya na kutochukua hatua zozote dhidi yao licha ya wananchi wanaohujumiwa kutoa taarifa kwa jeshi hilo.
Badala yake, katika matukio mengi Polisi imewageuzia kibao wananchi waliohujumiwa kwa kuwakamata na kuwaweka ndani.
Baraza Kuu linawataka Wakuu wa Jeshi la Polisi kujirudi, kutekeleza majukumu yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao na na kufuata maadili yao na kuwacha kujifanya ni Idara ya Polisi ya CCM.
9. Haliyatambui matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani.
Baraza Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa na watu hao.
CUF haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu.
Kwa vyovyote vile, Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo inaeleza kwa uwazi kabisa namna ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
10. Linawataka wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.
11. Linaendelea kuutambua uchaguzi mkuu uliokuwa halali, huru, wa haki na uliofanyika katika hali ya amani na utulivu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia linayatambua matokeo yake ambayo yalionesha wazi kwamba chaguo la Wazanzibari ni CUF na Maalim Seif Sharif Hamad kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Kitendo cha zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari kususia uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016 kimezidi kuyapa nguvu maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba, 2015 mbele ya macho ya Watanzania na dunia.
12. Linaendelea kuwataka Wazanzibari kuwa watulivu na kulinda amani iliyopo na linawahakikishia kwamba CUF inaendelea na juhudi zake za kutafuta haki yao na kusimamia maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa njia za amani na za kidemokrasia. Njia hizo za amani zimefanikiwa na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa ambayo imeanza kuchukua hatua dhidi ya ubakwaji wa demokrasia uliofanyika.
13. Linazishukuru na kuzipongeza nchi washirika wa maendeleo kwa kuchukua maamuzi ya kuzifutia misaada Serikali za kidikteta za CCM ambazo zimebaka demokrasia na kukanyaga haki za wananchi wa Zanzibar.
Baraza Kuu linatoa wito kwa nchi hizo washirika wa maendeleo na jumuiya za kimataifa kuchukua hatua zaidi dhidi ya Serikali za CCM na madikteta wake walioshiriki katika ubakaji wa demokrasia Zanzibar zikiwemo hatua makhsusi dhidi ya watu makhsusi waliohusika na ubakaji huo wa demokrasia na uvunjaji wa haki za binadamu katika kipindi hiki.
MWISHO, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawahakikishia wanachama wake wote na Watanzania kwa ujumla kwamba chama chao kiko imara na hakitoyumba wala kuyumbishwa katika kutetea na kupigania haki zao hadi tutakapofanikisha ujenzi wa taifa imara linalosimamia na kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu, demokrasia na utu wa watu wote.
Baraza Kuu linawataka viongozi wa Chama wa ngazi zote watekeleze majukumu yao ya kichama katika nafasi zao na pia Wabunge na Wawakilishi waliopewa ridhaa na Wazanzibari tarehe 25 Oktoba, 2015 kuwatumikia wananchi wote katika kutatua matatizo yao kadiri hali na uwezo wao unavyoruhusu.
Mbali na maazimio haya, Maalim Seif Sharif Hamad atazungumza na wananchi katika siku chache zijazo ili kuwaeleza kwa kina mwelekeo wa hali ya kisiasa ya Zanzibar na hatua zinazochukuliwa na CUF kuhakikisha maamuzi halali ya kidemokrasia ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 yanaheshimiwa.
HAKI SAWA KWA WOTE
Limetolewa na:
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITEDN FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)
ZANZIBAR
3 APRILI, 2016
6 comments:
Kama CUF inayo lengo la kuwaletea maendeleo Wazanzibari, basi kwa nini wanafurahia vitendo vya Mataifa ambayo yamekata misaada ya maendeleo? Watakaoteseka ni hiyo asilimia 80% ya Wazanzibari ambayo bwana Maalim na vibaraka wake wanawasifia kwa kutojitokeza kupiga kura ya marudio. Bwana Maalim ni mtu mwenye tamaa ya madaraka, lengo lake siyo kuwainua Wazanzibari. Tunajua ni kibaraka wa hawa Wakoloni wanaomlipa kuleta vurugu, lakini atashindwa tuu, hatutamruhusu kuleta vurugu kamwe.
Acha kuwapotosha walala njaa.kama kweli yanakutoka moyoni bwaga manyanga. Sema sasa, mimi siasa basi. Walishakuona tangu zama zileee....lakini yaonekana wewe na mzee wa Rhodesia hampishani.
Anonymous 1 na 2 hapo juu yaonekana wewe ni mtu mmoja ambaye umetumwa na hao Miungu watu ambao wameamua kubaka demokrasia na kutawala visiwa vya Unguja kwa nguvu na ubabe.Tusiwe wepesi wa kukimbilia kulaumu ukoloni au wakoloni (wazungu) eti wana haja ya kuleta vurugu!Ili iweje?? Kitu muhimu kinachoendelea huko Zanzibar ni watu wachache ambao wameamua kwamba watatawala visiwa hivyo kwa nguvu! Hawa ndio wakoloni halisi waliovaa ngozi nyuesi. Jana na juzi hao unaaowaita wakoloni walikuwa watu wazuri wahisani wa kutusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo. Leo hii tunavuruga uchaguzi na kufanya madudu ambayo hata mtoto mdogo anaona ni upuuzi kuita kilichotendeka Machi 20 kama ni uchaguzi, halafu tunatoka mapovu midomoni na tunakimbilia kuporomosha matusi makubwa makubwa. Maalim hakuiba kura na wala hakuvuruga uchaguzi. Waliovuruga mambo wanajulikana na kama kutakuwa na vurugu haoa ndio wakubebeshwa lawama. Tuachane na siasa za jikoni, zilipitwa na wakati kwenye miaka ya 60 hadi 70. Tusijidanganye, katika ulimwengu wa leo, Zanzibar haiwezi kusimama yenyewe kipekee bila ya kushirikiana na nchi au mataifa mengine. Zanzibar inahitaji kujenga uchumi wake na moja ya nguzo za uchumi huo ni utalii. Hata kama yatapatikana mafuta bado utahitaji kushirikiana na mataifa mengine kiteknolojia na kibiashara katika kukuza na kuendeleza sekta hiyo. Zanzibar siyo mali ya CCM au viongozi wake, tuamke na kutambua kwamba hizi ni zama mpya ambazo unatakiwa uwepo muafaka mpya wa jinsi ya kujenga demokrasia, umoja wakitaifa na kulinda maslahi ya Wanainchi wote wa visiwa vya Unguja na Pemba. Bila hivyo historia itawahukumu vibaya sana watawala walioko madarakani hivi sasa.
Seif bado anapata presidential service kutoka ndani ya serikali ya CCM. Matibabu,malazi, mahitaji yake yote ana yapata kwa asilimia 100% vipi atahofia Zanzibar au Tanzania kukatiwa misaada. Kunyimwa misaada kwa nchi masikini kama Tanzania wanaoasirika zaidi ni wananchi wanyonge. Nasisi wananchi masikini ambao ndio tulio wengi licha ya umasikini wa hali,umasikini wa akili ndio balaa linalotusumbua zaidi. Kwani hasira za pweza kwenye mkaa wa moto zinazompelekea kujikunyata pamoja kwa uchungu huku akizidi kujikusanyia moto karibu. Tumekosa uchaguzi na tunakosa misaada nani anaesirika zaidi? Zanzibar imepata uhuru wake kwa njia ya mapinduzi. Raisi wa kwanza baada ya mapinduzi hayo kauliwa kinyama licha ya upotoshwaji juu ya kifo chake yakuwa akina nani walihusika juu ya tendo hilo ovu katika historia ya Zanzibar, wareketwa wa mapinduzi na vizazi vyao wana ukweli wote juu ya wale waliohusika. CUF wanatamka hadharani yakwamba hawayatambui mapinduzi ya Zanzibar wakati muasisi wa mapinduzi hayo kauwawa kinyama sababu ya mapinduzi sasa hapo wafuasi wake watakuwa wanapata tafsiri gani kutoka kwa hao wanaopinga mapinduzi? CCM Zanzibar wameapa bila ya CUF kuyatambua mapinduzi ya Zanzibar basi wapo tayari kwa lolote lakini si kwa CUF kuchukua hatamu ya utawala kuviongoza visiwa vya Zanzibar. Ni busara pekee ndio inayoweza kuinusuru Zanzibar. Nguvu kubwa kuliko hata ya kunyima misaada zimetumika Libya, Iraq,Syria,Yemen na hata Zimbabwe na hakuna kilichobadilika zaidi ya maafa na zaidi walioasirika ni wananchi wanyonge. Na kiongozi anaesifia kukatwa kwa misaada kutoka kwa wahisani anaonekana shujaa kutokana na kitendo chake cha kuwakaribishia matatizo sasa hapo utaona jinsi gani faida ya umasikini wa akili inavyofanya kazi.
wadanganyika hamuwezi kuelewa msimamo wa maalim si rahisi wenu huyu;huyu ni raisi wa wazanzibari.wachiyeni wenyewe wazanzibari kipenzi chao;mtasema mwisho usiku mtalala.
maalim angekuwa mpenda madaraka si angeyapapatikia.ccm ingeshinda kihalali si mngeona .ccm imeshindwa mnawazibiti sasa kwa majeshi yenu;raisi shein si raisi wa wazanzibari ni wa wabara.raisi wa wazanziari ni maalim
na misaada mtanyimwa kweli maana mnatawali kimabafu.wenye uchu wa madaraka nyinyi si maalim ndo maana mpaka sasa anakubalika.
nasema tena wadanganyika shughulikeni na yenu kama raisi wenu alivyo kata kuingilia mgogoro.
wachiyeni wenyewe wazanzibari na nchi yao wanataka kupumuwa wamechoka kutawaliwa na mkoloni mweusi wa tanganyika
watu wengi hapa nyumbani hawawaelewi Wazungu na mabepari kwa ujumla wao! Mimi naweza kusema nauelewa kwa kiasi fulani mfumo wa Kibepari klk Mtanzania wa kawaida!
Na ninaweza nikawakikishia kwamba hayo yote tunayoyashuhudia leo hii kuhusu MCC au sijui nchi za Ulaya kusitisha hiyo inayoitwa misaada haina uhusiano wowote ule na sababu zilizotolewa!
Wazungu/Mabepari siku zote huongea au huwasiliana kinyume kinyume yaani wanachokwambia sicho wanachomaanisha, mimi ninavyohisi kuna uhusiano mkubwa sana kati ya maamuzi ya Serikali ya raisi Magufuli na maamuzi ya Wazungu kumbukeni ishu ya Mabenki, Serikali kukataza taasisi zake kuweka fedha Benki bali fedha zote ziwekwe Benki kuu, kumbukeni kwamba kuna Mabenki mengi makubwa hapa TanZania ambayo wewe huwezi kwenda tu kufungua akaunti kama vile City Bank haya yanafanya biashara na Serikali sasa Magufuli ameliminya hilo, vile vile kuna uamuzi wa Serikali kusitisha kukodisha mashine za kuwashia umeme ktk kwa Watu binafsi bali tujenge za kwetu ikumbukwe hapa Dowans na Symbion ni project ya Marekani chini ya Power Afrika ambayo ndiyo iliyowaleta H.Clinton na Obama TanZania, na hii ni fedha ndefu sana kwa Makampuni ya Kibepari sasa kusitishwa na Serikali ina maana mirija imezibwa!
Hivyo wengi mnaweza kufikiri kwamba sababu ni Zanzibar lkn hicho ni kisingizo tu sababu ni Uchumi hasa hilo la fedha, ambapo Serikali ilikuwa inafanya biashara na fedha zake yenyewe hapo ndipo ilipouma!
Wazungu huwa kwa mfano wako tayari kuzusha ugonjwa kama vile ebola au Zika ili tu kuweza kupata fedha, kwa mfano kuna makampuni ya pharmaceuticals yanahitaji fedha kudevelop baadhi ya dawa lkn hawana fedha hivyo hutumia ishu kama Ebola pmj na WHO halafu kesho utasikia zimechangwa kiasi kadhaa kwa ajili ya kutengeneza vaccine lkn ukweli ni kwamba hizo fedha ni kwa ajili ya makampuni ya Kibepari!
Hivyo mnaoshangilia kuhusu hili swala kuweni waangalifu sana kesho mkisikia MCC wametoa fedha mara mbili yake na hakuna cha Zanzibar wala Mitandao iliyoongelewa sijui mtaweka wapi sura zenu!"
Post a Comment