ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 6, 2016

DARAJA LA KIMATAIFA LA RUSUMO NA KITUO CHA HUDUMA KWA PAMOJA VYAZINDULIWA RASMI


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA

Coat of Arms

Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

               20 KIVUKONI FRONT,
                          P.O. BOX 9000,
                 11466 DAR ES SALAAM,  
                                   Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo Aprili 6, 2016 amezindua daraja la kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo.  
Zoezi hilo la uzinduzi lililofanywa na Mhe. Rais Magufuli wa Tanzania na Mhe. Rais Paul Kagame wa Rwanda, limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wa Serikali kutoka nchi zote mbili, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi mbambali za Kitaifa na Kimataifa.
Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha huduma kwa Pamoja Mpakani ni kiungo muhimu katika Ukanda wa Kati (Central Corridor) unaounganisha barabara kuu ya Dar es Salaam -  Chalinze – Morogoro – Dodoma – Singida – Nzega – Tinde – Isaka – Lusahunga na Rusumo kupitia Kibingo Nakayonza hadi Kigali nchini Rwanda. Mtandao huu wa barabara utakuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi kati ya Tanzania na Rwanda.

Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa mradi huo, Mhe. Dkt. Magufuli aliwahimiza wananchi kutumia fursa ya uwepo wa Daraja la Rusumo na Kituo cha huduma kwa Pamoja Mpakani Rusumo kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Aidha Rais Magufuli amewaasa wananchi kulinda miundombinu dhidi ya wezi wanaodiriki kuiba alama za barabarani, vyuma vya madaraja na kuharibu taa za barabarani kwa baadhi ya miji. Ameagiza vyombo vya usalama kuhakikisha wanalinda miundombinu hiyo na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaokamatwa wakifanya uharibifu huo.
Aidha licha ya mradi huo kurahisisha usafairishaji wa bidhaa na watu kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga alieleza faida kadhaa za mradi huo zikiwemo; kuwa ni kiungo muhimu cha Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya nyingine za Kikanda kama vile  SADC na COMESA, kurahisisha mawasiliano ya kijamii baina ya watu wa Tanzania na Rwanda, pamoja na kuimarisha uhusiano na kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili na nyingine za Maziwa Makuu.
Ujenzi wa Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha huduma Pamoja Mpakani Rusumo ni moja ya miradi inayotekelezwa kwa msaada kutoka Serikali ya Japan kwa nchi za Tanzania na Rwanda kupitia shirika lake la maendeleo la JICA. Mradi huu kwa upande wa Tanzania umegharimu takribani kiasi cha TShs. 33,206,508,072.07 hadi kukamilika. Miradi mingine inayotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia JICA ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Arusha – Namanga, Iringa – Dodoma, Namtumbo – Kilimasera – Matemanga – Tunduru pamoja na barabara ya Masasi - Mangaka.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dar es Salaam
06 Aprili, 2016

No comments: