ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 6, 2016

Dk Shein ateua wagombea urais watatu uwakilishi

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ametangaza kuwa hatamteua Makamu wa Kwanza wa Rais wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), huku akiwateuwa wajumbe saba wa Baraza la Wawakilishi wakiwamo watatu waliokuwa wagombea urais kupitia vyama vya upinzani.

Wagombea urais wa upinzani walioteuliwa jana ni Hamad Rashid Mohamed (ADC) aliyepata kura 9,734 sawa na asilimia 3.0, Juma Ali Khatibu (Ada-Tadea) kura 1,562 sawa na asilimia 0.5 na Said Soud Said (AFP) aliyepata kura 1,303 sawa na asilimia 0.4.

Kwa upande wa CCM walioteuliwa ni Balozi Amina Salum Ali aliyewania kuteuliwa kugombea urais wa Jamuhuri, Balozi Ali Karume, Mohamed Aboud Mohamed ambaye aliwahi kuwa waziri kwenye Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Moudline Castico mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM.

Awali wakati akizindua Baraza la tisa la Wawakilishi (BLW), Dk Shein alisema hayo yametokea kwakuwa wananchi waliipa CCM ushindi wa kishindo kwa kumpa kura 299,982 sawa asilimia 91.4 ya kura zote za urais, na kudhihirisha kuwa hakukuwa na sababu ya kuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais.

Alisema kati ya vyama 14 vilivyoshiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, zaidi ya CCM, hakuna chama kingine kilichoweza kupata kura za urais zaidi ya asilimia 10 wala kilichopata viti vingi vya uwakilishi zaidi ya chama hicho tawala.

“Kwa msingi huo na kuzingatia masharti ya kifungu cha 39(3) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 hakuna chama kinachokidhi vigezo vya kutoa makamu wa kwanza wa rais ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Dk Shein huku akishangiliwa.

“Huu ni uamuzi wa wananchi wa kukipa ushindi mkubwa CCM na hawakutoa nafasi ya kumchagua makamu wa kwanza wa rais. Huo ni uamuzi wao wa kidemokrasia.”

Maneno hayo ya Dk Shein yanakuja ikiwa ni siku moja tu baada ya CUF kutangaza kutomtambua kiongozi huyo na Serikali yake kwa madai kuwa alipatikana kwa uchaguzi uliovunja Katiba na Sheria.

CUF na vyama vingine tisa vilisusia uchaguzi wa marudio baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kwa sababu za kukiukwa kwa taratibu na sheria za uchaguzi.

Dk Shein pia alitupilia mbali madai ya wakosoaji wake kuwa alimteua Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi akieleza kuwa alifanya hivyo kikatiba kupitia kifungu cha 39(6) kutokana na kukosekana mgombea anayestahiki kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Muda mfupi baada ya Dk Shein kueleza kuwa hatoteua Makamu wa Kwanza wa Rais kuunda SUK, wanasheria nchini wamesema uamuzi huo ni mwendelezo wa kuvunja Katiba ya Zanzibar.

Wamesema uamuzi huo wa Dk Shein haukidhi matakwa ya kikatiba kwa maelezo kuwa anatakiwa kutumia Ibara ya 9(3) ya Katiba ya Zanzibar, ambayo inasema muundo wa SMZ utakuwa na SUK na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja na lengo la kufikia demokrasia.

Wakizungumzia utata huo, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Abubakar Khamis Bakar alisema kinachotokea Zanzibar ni zaidi ya maajabu, “Uundwaji huu wa Serikali anaousema Dk Shein ni uvunjaji wa Katiba.”

Bakar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF aligusia Ibara ya 42 (2) ya Katiba ya Zanzibar inayozungumzia uteuzi wa mawaziri na kusisitiza kuwa katika Katiba hiyo hakuna sehemu inayoeleza muundo wa Serikali ya chama kimoja.

Bakar alisema kutokana na Katiba kutokuwa na majibu juu ya muundo wa Serikali inayotokana na chama kimoja, hilo linadhihirisha wazi kuwa Serikali hiyo ni batili.

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stola alisema ,”Nadhani unatakiwa ufanyike muafaka kwanza kisha Katiba ya Zanzibar ibadilishwe ili kuendana na hali halisi.”

“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema Zanzibar kuna Waziri Kiongozi wakati Katiba ya Zanzibar imeondoa wadhifa huo na kuweka ule wa Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais.”

Stola alisema ili waweze kuwa na makamu wa kwanza wa Rais ni lazima Katiba ifanyiwe marekebisho kwa kuondoa masharti yaliyomo katika Katiba hiyo juu ya kumpata kiongozi huyo.

“Lazima CCM na CUF wafikie muafaka kwanza ambao utazaa marekebisho ya Katiba ya Zanzibar. Katiba hiyo ikiachwa kama ilivyo haitekelezeki kabisa katika uundwaji wa Serikali,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema kinachofanyika Zanzibar hakielezeki wala hakina mfano wa kisheria wa kukifananisha huku akishauri iundwe Serikali ya mpito ili kutoa nafasi ya kuondoa ukakasi wa kisheria na kikatiba uliovikumba visiwa hivyo, “Tusidanganyane pale hakuna Serikali.”

Akizungumzia hotuba ya Dk Shein, Katibu Mwenezi wa chama cha Ada-Tadea, Rashid Yusuph Nchenga alisema kuwa uamuzi wa Rais kutounda SUK umefuata katiba na kwamba kiongozi yeyote makini duniani angefanya uamuzi huo.

Hata hivyo, alisikitishwa na kitendo cha BLW kutokuwa na wajumbe kutoka upinzani akieleza kuwa “hilo ni suala la ajabu” kwa kuwa Zanzibar imerudi nyuma kuwa na baraza la chama kimoja cha CCM.

Mwakilishi wa jimbo la Tumbatu, Haji Omar Kheir alisema kauli ya Dk Shein wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana alisema kuwa CUF ingekufa mwaka 2015 imejidhihirisha baada ya “wananchi kuichagua CCM kwa kishindo.”


Imeandikiwa na Nuzulack Dausen, Fidelis Butahe na Elizabeth Edward.

No comments: