Mjumbe wa Kuteuliwa wa Baraza la Wawakilishi, Hamad Rashid (ADC) ametaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutobabaishwa na nchi washirika wa maendeleo kwa kususa misaada yao kwa kile alichosema, nafasi ipo ya kutumia rasilimali ziliopo kikamilifu.
Rashid, ambaye alikuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ADC katika uchaguzi wa marudio, alisema hayo wakati akichangia hotuba ya rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein aliyoitoa katika uzinduzi wa baraza la wawakilishi.
Mwakilishi huyo alionya nchi hizo akitaka zisitumie uwezo wao kwa ajili ya kulazimisha matakwa yao na kupinda sheria za nchi zinazotokana na demokrasia iliopo.
Alisema Tanzania bado inao uwezo mkubwa wa kutumia rasilimali zake zinazotokana na utajiri mkubwa kwa ajili ya kujenga nchi na kupambana na umasikini lakini viongozi walikuwa wakibweteka kutokana na kuwepo kwa misaada ya nchi matajiri.
“Tusibabaishwe na wahisani kwa tishio lao la kusitisha misaada ya maendeleo...wakati umefika wa kufanya kazi na kutumia rasilimali zetu kikamilifu ikiwemo kukusanya mapato na kupambana na viongozi wazembe na wabadhirifu."
Rashid mwanasiasa mkongwe ambaye aliwahi kuwa naibu waziri wa fedha na uchumi wa Serikali ya Muungano katika miaka ya 1987, alisema huu ni wakati wa kuiga mfano wa nchi ya Kenya wahisani walizuia misaada kwa asilimia 80 lakini walitumia walichonacho kwa ajili ya matumizi ya ndani.
Mapema Rashid alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohmed Shein kwa kumteua kuwa mwakilishi, hatua ambayo imetimiza ndoto zake za kuunda serikali itakayovishirikisha vyama vya siasa nchini kinyume ma matarajio ya wapinzani.
“Hii siyo serikali ya umoja wa kitaifa lakini ni serikali iliyowajumuisha wananchi na vyama vyote vya siasa na sasa tupo tayari kufanya kazi kwa ajili ya kuleta na kusimamia maendeleo kwa faida ya wananchi wote kwa sababu uchaguzi umekwisha,’’alisema
No comments:
Post a Comment