Advertisements

Friday, April 29, 2016

NAIBU SPIKA ACHAFUA HALI YA HEWA BUNGENI BAADA YA KUMWITA MBUNGE BWEGE

Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye katika vikao vya Bunge anatakiwa kusimamia mijadala kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, jana alizua kizaazaa baada ya kumuelezea mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Said Bungara kuwa ni bwege, akimtaka aache kuonyesha hali hiyo.

Kwa mujibu wa toleo la pili la Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford) la mwaka 2004, neno bwege linamaanisha “mtu mjinga, mpumbavu, bozi, fala gulagula”.

Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo kilisababisha wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu aliyefunguliwa mashtaka mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John Magufuli kuwa ni bwege.
Bila ya kuruhusiwa, mmoja alifungua kipaza sauti na kusema: “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.”

Hata hivyo, wabunge hao wa upinzani hawakushinikiza Dk Tulia kufuta kauliz yake, lakini baadaye wakiwa nje ya ukumbi waliponda kitendo hicho cha kiongozi huyo wa Bunge ambaye aligombea uspika kwa tiketi ya CCM kabla ya kujitoa na muda mfupi baadaye kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na hivyo kupata sifa ya kugombea nafasi hiyo ya naibu spika.

Dk Ackson aliamsha tafrani hiyo saa 5:48 asubuhi baada ya Bungara, ambaye ni maarufu kwa jina la Bwege, kusimama bila kufuata kanuni za Bunge, kupinga maelezo ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye juu ya uamuzi wa Serikali kusitisha shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni nchini.

“Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,” alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo asiendelee kuzungumza wakati mjadala ukianza kuwa mkali.

Mjadala huo uliendelea bila ya wapinzani kuhamaki, lakini baada ya Nape kutoa taarifa akieleza kuwa uamuzi wa kuanzisha studio za Bunge ulifanywa na Bunge la Kumi ambalo yeye hakuwamo, ndipo wapinzani walipokumbusha kauli hiyo ya naibu spika.

“Bunge linaonyeshwa asubuhi na kurudiwa kuonyeshwa usiku na kuna wanahabari hapa Dodoma wana kamera zao na wanaripoti bunge hili. Tusitumie bunge hili kupotosha,” alisema Nape kabla ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kuingilia kati.

Msigwa: Hii ni taarifa au hotuba? 
Spika: Msigwa jifunze kusikiliza kwanza, unaipokea taarifa yake ama vipi?

Msigwa: Taarifa yake naikataa kwa sababu anasema uongo. Leo na wewe umemuita mtu bwege. Kuna mtu kule Arusha alimuita Rais Magufuli bwege na akapelekwa mahakamani. Na wewe tutakupeleka mahakamani.

Mkazi huyo wa Arusha, Isaack Habakuk Emily alipandishwa kizimbani takribani wiki mbili zilizopita akikabiliwa na shtaka la kumuita Rais kuwa ni bwege.

Msigwa alisema Bunge “nalo ni jipu” kwa kuwa haliwezi kuishauri Serikali kutokana na kufanya maamuzi bila ya kushirikisha makamishna wake, akitoa mfano wa chombo hicho kurejesha Sh6 bilioni serikalini ambazo zilibanwa kwenye matumizi yaliyoelezewa kuwa hayakuwa muhimu.

Baada ya Msigwa kumaliza kuchangia, alifuatia mbunge wa viti maalumu (Chadema), Tunza Malapo ambaye aliungana kauli na Msigwa na kumponda Nape na uamuzi wa Serikali.

Wakati Malapo akiendelea kuchangia, alisimama Khatibu kutoa taarifa.

“Kwa taarifa yako wewe Malapo aliyelishauri Bunge kutorushwa live ni Nape vuvuzela,” alisema.

“Kwani kuanzisha studio za Bunge maana yake ni Bunge kutorushwa moja kwa moja?”

Wakizungumzia tukio hilo la asubuhi, mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey Mgimwa alisema Dk Tulia alighafilika wakati akitoa kauli hiyo baada ya kurushiwa maneno mara kwa mara na wabunge wa upinzani, tena bila kufuata kanuni na taratibu za kibunge.

“Kwanza mtu mwenyewe (Bungara) huwa anapenda kuitwa bwege sasa kama ukiamua kumuita bwege utakuwa umekosea?” alihoji.

Alisema mara nyingi huibuka mvutano bungeni kwa sababu baadhi ya wabunge hawataki kuzingatia kanuni za chombo hicho cha kutun ga sheria.

Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Antony Komu alisema: “Kauli iliyotolewa na Naibu Spika inaonyesha wazi kuwa ni kiongozi anayekiuka misingi, taratibu na kanuni za Bunge. Tazama anatukana watu tu bila kujali jambo lolote, hii si sawa kabisa.”

Alisema Bunge linapaswa kuongozwa kwa haki na si kama ilivyo sasa ambayo inawafanya wabunge wa CCM waonekane kuwa na haki zaidi ya upinzani.

“Mfano (mbunge wa Tarime Vijijini-Chadema, John) Heche aliomba mwongozo akanyimwa ila Dk Kigwangalla akapewa,” alisema.

Kwa takribani wiki moja Bunge lilikuwa limepoa kutokana na wabunge wa vyama vya upinzani kususia kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini jana walishiriki kwenye mjadala wa wizara ya Ofisi ya Rais na kurejesha uhai kwenye chombo hicho.

Katika hoja zao jana, wabunge hao walijikita zaidi kuponda Serikali ya Awamu ya Tano kuwa inakiuka kanuni za utawala bora na kupinga uamuzi wake wa kusitisha matangazo ya Bunge, jambo lililomlazimu Nape kusimama mara kwa mara kutetea uamuzi wa Serikali, huku Dk Ackson akitoa ufafanuzi wa kanuni za Bunge.

Mara zote ambazo Nape na Dk Ackson walikuwa wakitoa ufafanuzi wao, walizomewa na wabunge hao wa upinzani huku mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji akimfananisha Nape na “vuvuzela” kwa maelezo kuwa ndiye aliyeishauri Serikali kusitisha matangazo hayo. 

Akichangia mjadala huo, Mchungaji Msigwa alisema utawala bora na unaozingatia sheria hauanzi na bajeti, bali huanza na utawala bora.

“Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, dhana nzima ya utawala bora haionekani. Utawala bora ni kuongoza nchi kwa ufanisi, tija na kwa uwazi, uadilifu, uwajibikaji na ushirikishwaji wa watu kwa kufuata utawala wa sheria,” alisema.

Alisema ni ajabu Ofisi ya Rais-Utawara Bora kuomba bajeti ya Sh800 bilioni wakati nchi haina utawala bora. Alirejea kauli ya kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe kuwa Serikali inaongozwa bila ya maamuzi yake kuwekwa kwenye Gazeti la Serikali.

“Walikuwa wanafanya kazi kama sisi tu mawaziri vivuli wa upinzani.Wanatoa maagizo wakati hawapo kisheria. Huu si utawala bora,” alisema Mchungaji Msigwa.

Alisema licha ya jambo hilo kubainika wazi Bunge lilikaa kimya huku akidai kuwa hata baadhi ya mawaziri walikuwa wanajua jambo hilo, na kwamba wanapokuwa nao katika mgahawa wa Bunge, wamekuwa wakiponda na kuukosoa utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli.

“Mawaziri mnakuwa kama vinyonga. Kwenye chai mnasema ukweli, mkija bungeni mnakaa kimya.Huwa tunawarekodi na mkibisha tutataja mmoja mmoja humu ndani,“ alisema Msigwa huku akimtaja Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla kuwa ni mmoja wa mawaziri hao baada ya waziri huyo kusimama kuomba mwongozo, kupinga kauli ya mbunge huyo.

Dk Kigwangalla alitumia kanuni 68 (7) na 63 (1) kuomba mwongozo, akimtaka Mchungaji Msigwa athibitishe kauli yake kwa kuwataja kwa majina mawaziri wanaopingana na uongozi wa Serikali.

Dk Ackson naye alitoa ufafanuzi akinukuu kifungu cha 63 (1) (2), kinachomtaka mbunge kuthibitisha jambo analolisema hapohapo ama apewe muda na kwamba atatoa maelezo ya kuwataka Dk Kigwangalla na Mchungaji Msigwa kuwasilisha ushahidi wao.

Msigwa: Mbona Kigwangalla unajihisi mwenye hatia? 
Dk Ackson: Msigwa unaongea na kiti usibishane na mbunge.

Msigwa: Mheshimiwa Spika wakati wa kuchangia tunakuwa na taarifa sio mwongozo ila nashangaa huyu (Dk Kigwangalla) kaomba mwongozo kapewa. Ila tunaendelea tu ila kiti bado kinayumba.

Dk Ackson: Mbunge anaweza kukosea na wengi tu hukosea. Ametaja kanuni zinazohusu utaratibu naomba tusiendelee kujibizana.

Akiendelea na mjadala huo Mchungaji Msigwa alisema Bunge la Tisa na la Kumi yaliendeshwa kwa uwazi mkubwa tofauti na Bunge la Kumi na Moja, kwamba hata utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne ulikuwa haubani demokrasia na kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.

“Bunge ni mkutano wa wazi wa wananchi wote, lakini Serikali hii inaanza kuminya na kuweka siri. Huu si mkutano wa unyago, tunaongelea matumizi ya fedha za Watanzania,” alisema.

“Serikali inayokandamiza uwazi ni Serikali iliyojaa uoga na inayoficha madudu. Mnasimama na kusema mnakusanya fedha za kuvunja rekodi sasa mnaficha nini kuwaonyesha Watanzania hiki mnachokifanya?”

Huku akiipongeza Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mchungaji Msigwa alisema pamoja na udhaifu wake, ilikuwa haizuii watu kuzungumza na kusema ukweli.

“Nyinyi mmekuja na ‘hapa kazi tu’, lakini hamtaki kukosolewa. Wakati tunamkosoa Kikwete wabunge wa CCM mlikaa kimya na kutuzomea, leo mnaufyata na inaonekana hata Dk Magufuli akidondosha kijiko, mtasimama na kupiga makofi kwa sababu ya uoga wenu,” alisema Mchungaji Msigwa na kuwataka wabunge kuhoji mambo kwa maslahi ya wananchi. 

No comments: