Na Baraka Mbolembole
Kuelekea mchezo wa Jumamosi hii kati ya mabingwa wa ligi kuu Tanzania Bara, Yanga SC dhidi ya Al Ahly ya Misri, nahodha wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Shadrack Nsajigwa amesema kwamba timu yake hiyo za zamani inapaswa kuishinda Al Ahly kwa namna yeyote katika mchezo huo wa kwanza wa mzunguko wa pili katika kugombea kufuzu kwa hatua ya makundi.
Yanga wanakutana na Al Ahly kwa mara ya 3 ndani ya miaka 7 na mara zote mbili (2009 na 2014) walipokutana Yanga ilitupwa nje ya michuano.
Nimefanya mahojiano na mlinzi huyu namba mbili wa zamani ambaye amepata kuzichezea pia klabu za Tukuyu Stars, Tanzania Prisons za mkoani Mbeya na Moro United iliyomaliza katika nafasi ya pili VPL msimu wa mwaka 2005.
Ungana nami hapa kwa mengi zaidi, kumbuka kwa sasa Nsajigwa ni kocha wa timu ya vijana ya Yanga (Yanga B) na mchambuzi mahiri wa kandanda nchini.
www.shaffihdauda.co.tz: Kocha ulikuwa kama mchezaji katika michezo miwili ya Yanga dhidi Al Ahly mwaka 2009, pia miaka miwili iliyopita Yanga walikutana tena na timu hiyo ya Misri katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, na Yanga walipata ushindi wa 1-0 hapa nyumbani lakini bahati mbaya wakapoteza kwa mikwaju ya penalti katika gemu ya ugenini na kutolewa katika michuano, Jumamosi hii timu hizo zinakutana tena baada ya kupita miaka miwili huku Al Ahly ikiwa haijapata kufuzu kwa hatua ya makundi kwa misimu miwili mfululizo.
Ukiitazama Yanga namna inavyocheza hivi sasa inaonyesha ni timu yenye ‘usongo’ wa kufanikiwa zaidi kimataifa, wewe kama mchezaji mzoefu wa zamani ukiwa kama nahodha wa Yanga na timu ya Taifa (Taifa Stars) pia umecheza dhidi ya timu za kiarabu mara kadhaa ni vitu gani muhimu tunapaswa kuvitazama kuelekea mchezo ujao siku ya Jumamosi?
NSAJIGWA: Kwanza tunapaswa kutambua kwama mechi itakuwa ngumu kwa kila upande. Waarabu manapocheza mechi za ugenini hucheza kwa lengo la kujilinda zaidi na kufanya mashambulizi timilifu ya kushtukiza. Pia huwa hawajali sana matokeo ya ugenini kwa sababu wanaamini ‘KWAO’ ni lazima wataenda kucheza kwa kufunguka.
Ni kweli katika miaka ya karibuni kutokana na machafuko ya kisiasa nchini Misri yalipelekea kushuka hata kwa kiwango chao cha mpira na hilo limechangia Al Ahly kutofanya vizuri sana katika ligi ya mabingwa, lakini sasa ukiitazama unaona namna timu yao inavyojipanga upya.
Katika timu yao kuna wachezaji 7 hadi 8 wanaofanya vizuri katika kikosi cha timu yao ya taifa hivi sasa. Naamani watacheza vizuri, wana kocha ambaye ana ujuzi mkubwa (M-holland, Martin Jol,) hivyo watakuwa na mbinu nyingi kiuchezaji.
Kwa hiyo tutarajie kuona mechi ngumu na ya kimbinu zaidi. Katika mechi kama hizi (mechi za mtoano) kila timu inategemea zaidi uwanja wake wa nyumbani, kikubwa upande wetu sisi (Yanga) tunahitaji kuwa makini sana tusiige mpira ambao wataucheza Al Ahly kwa sababu waarabu wakiwa hapa watacheza mchezo wa taratibu kwa lengo la kutupoozesha sisi ili wapate matokeo wanayotaka wao.
Sisi tunapaswa kucheza kwa kasi na tukitaka kufuzu kwa hatua inayofuata ni lazima tuwafunge Al Ahly hapa, ushindi wa aina yo yote ule, goli 1-0, 2-0 au lolote linalowezekana ili twende ugenini tukiwa na ushindi kama ilivyokuwa miaka miwili iliyopita tulipotolewa kwa mikwaju ya penati.
Lolote linaweza kutokea kama tukienda Misri na ushinda, itakuwa rahisi kujipanga kama tutapata ushindi katika mchezo wa hapa nyumbani kuliko tukiwa na matokeo ya sare au kupoteza mechi. Yanga si timu mbaya, inacheza vizuri, timu imeonekana kuimarika zaidi katika idara mbalimbali, cha msingi, labda cha kusisitiza tu ni kwamba, wachezaji wetu wanapaswa ‘kufunguka’ hii iwe ndiyo kama mechi ya kuamua nani afuzu na nani atoke.
www.shaffihdauda.co.tz: Ukiitazama Yanga kiukweli inacheza vizuri, lakini ni kama wamejijengea kitu fulani, kwamba, ‘tunaweza tukashinda mechi hata kama tukianza kufungwa goli’, nimeona katika baadhi ya michezo ya ligi wakianza kufungwa ndani ya dakika 20 za mwanzo lakini wakafanikiwa kupata matokeo, pia tuliona APR walipokuja Dar es Salaam kucheza na Yanga walitangulia kupata goli lakini nao wakapoteza mechi.
Sijafurahishwa na uchezaji wao wa taratibu wanapoanza mechi na kuanza kuchangamka baada ya dakika 15 na kuendelea. Sasa wanakwenda kucheza na Al Ahly timu ambayo inakawaida ya kufunga magoli ya harakaharaka wanapotawala mechi, madhara gani wanaweza kukutana nayo Yanga kama watajikuta wakianza kufungwa goli katika mchezo wa Jumamosi?
NSAJIGWA: Mimi ninaamini kwamba kuelekea mchezo huo mwalimu na hata mchezaji yeye mwenyewe binafsi atakuwa anajua anakwenda kucheza mechi kubwa. Mechi za ligi na zile za kimataifa hata barani Ulaya huwa na mbinu tofauti kwa sababu wanakutana wachezaji ambao wana akili, wanajua nini ambacho wanafanya kwa wakati gani na kitaleta faida gani kwa timu.
Sasa kama mchezaji hilo si jukumu la kocha tena ni suala la mchezaji mwenyewe kutambua kuwa hii ni mechi kubwa zaidi, mechi ambayo inaweza kutengeneza maisha ya mchezaji mwenyewe kwa hiyo wanapoingia uwanjani wanapaswa kujua kabisa wanakwenda kupambana kuanzia dakika ya kwanza hadi ile ya mwisho kwa ajili ya timu na maisha yao wenyewe.
Kuanzia dakika ya kwanza wanapaswa kujua fika kuwa hii ni mechi ya nyumbani na tunahitaji ‘matokeo salama’ kuelekea mchezo wa marejeano ugenini. Kucheza na Al Ahly ni jambo gumu lakini kwa vile tuko katika michuano tunapaswa kuhakikisha tunawashinda na kuwatoa. Watu wengi wanatamani kucheza dhidi ya Al Ahly.
Kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki klabu nyingi zinatamani kucheza na timu kubwa kama Al Ahly. Ni lazima tuwafunge Al Ahly kwa sababu ni timu kubwa na yenye mafanikio zaidi barani Afrika, wapo kwenye ubora kwa muda mrefu huku ikishikilia chati ya timu yenye mataji mengi zaidi duniani.
Kuwafunga itakuwa ‘deal’ kubwa sana kwetu, na wanafungika kwa kuwa mpira wa sasa umebadilika sana hakuna tofauti kubwa ya kiuchezaji kama zamani.
Hii mechi kubwa hivyo wachezaji wa Yanga wanapaswa kucheza kwa umakini na tahadhari kubwa ya kutokubali kufungwa goli la mapema na hii si mechi ya kutangulia kufungwa eti ukijiamini utasawazisha na kushinda mechi.
APR baada ya kushangazwa na kiwango cha Yanga katika uwanja wao wa nyumbani walikuja Dar na mbinu tofauti. Kwao walicheza sana mpira katikati ya uwanja lakini walipokuja hapa walifunguka kwa kasi wakitumia zaidi pembeni ya uwanja.
Wakapata goli, lakini Yanga walijipanga na kuwadhibiti, tukaona wakapata goli la kusawazisha kisha wakashinda mechi. Al Ahly wanakuja hapa na wachezaji wa daraja la juu zaidi, wanakuja huku wakijua wanataka matokeo ya aina gani.
Kwa hiyo hata sisi hivi sasa ukitazama utaona timu inawachezaji waliopevuka kimchezo na kiumri ambao tayari wamepata uzoefu wa kutosha wa kucheza mechi kubwa kama hizi.
Lolote linaweza kutokea kama tukienda Misri na ushinda, itakuwa rahisi kujipanga kama tutapata ushindi katika mchezo wa hapa nyumbani kuliko tukiwa na matokeo ya sare au kupoteza mechi.
www.shaffihdauda.co.tz: Unazungumziaje tabia ya baadhi ya mashabiki kuzishangilia timu za nje zikija kucheza na timu zetu katika michuano ya ndani. Mimi nadhani tunapaswa kushinda sisi wenyewe na inapofikia wakati wa mechi za kimataifa tunakuwa upande wa timu ya nyumbani au kama haiwezekani ni bora watu waende uwanjani kutazama mechi tu lakisi si kushangilia timu ngeni.
NSAJIGWA: Katika miaka ya karibuni jambo hilo si rahisi kutoweka katika miaka ya karibuni na kama tunataka kuliondoa kwanza ni lazima tuanzie katika timu ya Taifa. Wakati nachezea Yanga tumewahi kuzomewa uwanjani na mashabiki wa hapa nyumbani.
Kiukweli ni utamaduni uliopo Tanzania tu. Kuna wakati Simba ilikuwa na wachezaji nane hadi tisa katika kikosi cha kwanza cha timu ya Taifa Stars na ilipotokea wakapoteza mechi mashabiki wa hapa hapa nyumbani walisema ‘Simba ndiyo imefungwa,’ miaka ya karibu Yanga imekuwa ikitoa wachezaji wengi katika timu ya Taifa na timu ikifungwa watu wanasema ‘Yanga imefungwa.’
Haya ni mambo ambayo hayapo kwingine. Mfano mzuri ni Al Ahly na Zamaleki timu hizi hasimu nchini Misri hazishangiliani kamwe lakini katika miaka ya karibu si rahisi timu mojawapo kuisapoti timu ngeni inapocheza na timu mojawapo.
Hii inakuzwa kwa sababu ya visasi, hatuwezi kubadilika katika hili kama tutaendelea kuishi kwa visasi lakini ni mambo yaliyopitwa na wakati. Tujaribu kuwafuata wao safari hii (mfano Yanga na Azam FC) na tusubiri wakati ujao watafanya nini.
Simba na Yanga ndiyo timu kubwa zaidi nchini, zina ushawishi mkubwa, zina mashabiki wengi wanaozipenda kwa dhati timu zao, hivyo kupitia timu hizi mbili naimani ndiyo zinaweza kubadilisha muelekeo wetu wa mpira na muonekano kwa sababu hiyo ya ushawishi na wingi wa mashabiki wao.
Credit:Shaffihdauda.
No comments:
Post a Comment