Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, amemwondoa kwenye nafasi yake, Mnunuzi wa Vifaa na Boharia Mkuu wa jeshi hilo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Adriano Magayane ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
Kuondolewa kwa DCP Magayane katika nafasi hiyo kunatokana na taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari hivi karibuni, kuwa anamiliki nyumba zaidi ya 40 na kumbi kadhaa za starehe ndani na nje ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Gazeti la Mtanzania, IGP Mangu amefikia uamuzi huo kwa kile kinachodaiwa kuwa tuhuma hizo ni nzito na zinalenga si kumfedhehesha yeye kama ofisa mkuu wa Jeshi la Polisi, lakini kwa jeshi zima.
“IGP Mangu amemwondoa mara moja DCP Magayane kutokana na tuhuma zinazomkabili, kwa kweli ni nzito, nadhani hatua zilizochukuliwa ni sahihi… unajua sisi askari tuna miiko ya utendaji kazi, sasa inapotokea tuhuma kama hizi kwa ofisa kama huyu, lazima uchunguzi wa kina ufanyike,” kilisema chanzo .
Kilisema kuwa uchunguzi dhidi ya ofisa huyo unafanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Diwani Athumani.
Katika mabadiliko hayo, habari za ndani zinasema kuwa DCP Magayane amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi, Kitengo cha Uzuiaji wa Makosa.
Alipoulizwa ana, IGP Mangu alikiri kumwondoa ofisa huyo, lakini hakueleza amepangwa kitengo gani.
“Ni kweli nimemwondoa kwenye nafasi yake jana (juzi) ili kupisha uchunguzi wa suala hili kwani ni zito, lazima tujiridhishe kabla ya kuchukua hatua zaidi,” alisema.
Alipoulizwa ni nafasi gani ambayo atapewa DCP Magayane baada ya kuhamishiwa Makao Makuu ya Polisi, IGP Mangu alisema jeshi hilo lina kazi nyingi hivyo atapangiwa majukumu mengine bila kuingia kwa undani.
Aidha, IGP Mangu alisema ameagiza uchunguzi wa tuhuma hizo zilizotolewa kwenye vyombo vya habari, uanze mara moja ili wajiridhishe kabla kuchukua hatua zaidi.
Pamoja na uamuzi huo wa IGP Mangu, tayari vyombo vya dola vimeanza kumuhoji DCP Magayane, ikiwamo kumtaka awasilishe nyaraka zinazohusu umiliki wa mali zake zote.
Kutokana na hali hiyo, IGP Mangu amelazimika kufanya mabadiliko madogo ndani ya jeshi na kumteua Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Suzan Kaganda kushika nafasi ya DCP Magayane.
ACP Kaganda amewahi pia kuwa msaidizi wa Boharia Mkuu miaka kadhaa iliyopita kabla ya kuwa msemaji wa Jeshi la Polisi mwaka 2007 hadi 2008, baada ya kustaafu kwa aliyekuwa msemaji, ACP Abdallah Msika.
Mbali na kushika wadhifa huo, ACP Kaganda aliwahi pia kuwa Ofisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Dodoma na baadae kuteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma ambako alihudumu kwa miaka miwili kabla ya kuhamishiwa Mkoa wa Tabora.
3 comments:
How rotten is Bongoland. Pole sana JPM, you have a lot to do.
HII NDIO INATAKIWA> UKITAJWA KWA RUSHWA, UNATOKA AU UNATOLEWA, WATU WANAKUCHUNGUZA, NA KUTEGEMEANA NA MATOKEO YA UCHUNGUZI, UNAWEZA KURUDI, VINGINEVYO NDIO IMETOKA HIYO.
i think wachunguzwe but isiwe ndiyo uchunguzi inacost more than the crime committed. Inabidi pia walipe hizo pesa walizoiba kufungwa bado kuna igarim serikali hela.
Post a Comment