Uhalifu wa kutumia silaha uliokithiri nchini huenda ukapungua au kumalizika kabisa kuanzia Julai Polisi itakapofanya msako wa silaha haramu zinazokadiriwa kufikia kati ya 500 na 5,000 zilizomo mikononi mwa wahalifu.
Msako huo utafanyika baada ya kukamilika utaratibu wa kuhakiki silaha unaofanywa hivi sasa, watu wote wanaomiliki silaha wanatakiwa kuzipeleka makao makuu wa polisi wilaya kuonyesha nyaraka za umiliki au kuzisalimisha. Baada ya miezi mitatu iliyoanza Machi, watakaokutwa nazo watahesabiwa ni wahalifu na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Idadi ya silaha haramu zilizopo mikononi mwa wahalifu haijulikani, lakini Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman anasema kwa kuangalia rekodi ya silaha zilizokamatwa katika msako mwaka jana zinakaribia 500.
Kwa mujibu wa Athumani, mwaka uliopita (Januari hadi Desemba 2015), polisi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama maeneo mbalimbali nchini walikamata silaha 492 ambazo uchunguzi unaonyesha zinaingizwa kinyemela na makundi ya wahalifu.
“Silaha hizo kwa kiwango kikubwa, zinapitia mikoa yenye mipaka na nchi jirani ambako kuna mapigano ya wenyewe
kwa wenyewe, makundi ya uhalifu kama Al Shabaab na kwenye nchi ambazo kuna wapiganaji maeneo ya misituni,” anasema Athumani.
Kazi inayofanyika kwa sasa ni kuhakiki nyaraka za umiliki wa silaha na kupokea zinazorejeshwa na watu waliozipata kinyume cha sheria, ama walioziokota au kupokonya wahalifu. Baada ya muda uliopangwa kumalizika kila anayemiliki bila kibali atahesabiwa ni mhalifu, hivyo lazima apokonywe kwa nguvu.
Baadhi ya mikoa ambayo silaha zilikamatwa na idadi yake kwenye mabano ni Tabora (45), Rukwa (38), Katavi (34), Kigoma (32), Iringa (27), Mbeya (27), Morogoro (25), Pwani (20), Tanga (20) na Rukwa (19).
“Katika mikoa hii, watuhumiwa 395 walikamatwa; wanaume 379 na wanawake 16. Silaha zilizokamatwa ni pisto 47, Sub Mashine Gun (SMG) 41, SAR 13, Shotgun 69 na magobole 258,” anasema.
Wakati makadirio ya polisi ni kidogo, Shirika lisilo la Serikali linaloshughulikia udhibiti wa silaha ndogondogo na nyepesi (Tanansa) linasema idadi ya silaha haramu inafikia 5,000.
Mkurugenzi wa Tanansa, Dk Peter Mcomalla anasema tatizo la kusambaa kwa silaha za moto mikononi mwa wahalifu ni kubwa na linaisumbua dunia siyo Tanzania pekee.
Kwa Tanzania, Dk Mcomalla anasema licha ya silaha kuingia nchini na kuwafikia wahalifu zikitokea nchi jirani zenye migogoro, kuna maeneo wanatengeneza kama Kigoma, Kagera, Mara, Geita.
Katika mahojiano maalumu, mkurugenzi huyo anasema miji mikubwa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya kuna silaha nyingi na uhalifu mwingi.
Dk Mcomalla anasema utafiti uliofanywa na mashirika ya kimataifa ya kudhibiti silaha, umeonyesha kwa sasa kuna silaha takriban 638 milioni, kati ya hizo milioni 259.6 zipo mikononi mwa vyombo vya Serikali, wananchi wanamiliki silaha milioni 370 kwa ajili ya ulinzi binafsi huku makundi ya wahalifu na wapiganaji yakimiliki zaidi ya milioni moja.
Dk Mcomalla anasema utafiti wa Tanansa katika mikoa ya Mara, Kagera na Kigoma mwaka 2010 hadi 2014 umebaini baadhi ya wananchi wa mikoa hiyo wanamiliki silaha ambazo zimeingizwa nchini kinyemela.
“Silaha zimekuwa zikiingizwa nchini kwa mbinu mbalimbali, ikiwamo ya kutumia majeneza ili kudanganya kuwa wanasafirisha miili ya marehemu kumbe ni silaha. Katika Kijiji cha Shirati, wilayani Lorya, tulibaini pia kuna biashara haramu ya silaha na risasi na tulibahatika kukutana na kijana mwenye bunduki aina ya SAR na risasi 26,” anasema.
Dk Mcomolla anasema mikoa ya Kigoma na Kagera, inaathiriwa na mapigano ya Burundi na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Katika maeneo haya tulibaini watu wakimiliki silaha za kivita kama SMG, ambazo kwa kawaida si silaha za kiraia,” anasema Dk Mcomalla na kuongeza:
“Tumebaini watu wengi wana silaha. Kwa mfano, maeneo ya machimbo kama Tanzanite Mererani kuna zaidi ya watu 3,000 wanamiliki silaha, sasa kama hawana elimu ya kutosha juu ya umiliki wa silaha ni tatizo.”
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini pia miaka ya hivi karibuni, wahalifu wamekuwa wakijipatia silaha kwa kuvamia vituo vya polisi na kupora bunduki.
Baadhi ya vituo vilivyowahi kuvamiwa na kuporwa silaha ni Bukombe na Ushirombo vya Mkoa wa Geita; Kilombero, Morogoro; Tanga; Mkuranga, Pwani na Sitakishari, Dar es Salaam.
Vilevile, uchunguzi unaonyesha wahalifu wamekuwa wakitumia mabomu ya kurushwa kwa mkono katika matukio ya ujambazi, uporaji na hata yanayosadikiwa kuwa ya kigaidi ambayo hurushwa kwa kuwalenga makundi ya watu.
Mabomu yamewahi kurushwa wakati wa uzinduzi wa kanisa Arusha, kufunga mikutano ya kampeni Arusha na hivi karibuni walipofanya uporaji Benki ya Access tawi la Mbagala, Dar es Salaam.
Kuwapo matumizi ya mabomu hayo ya kutengenezwa viwandani ni ishara kuwa wahalifu wamejizatiti vilivyo na popote zilipotumika zimesababisha madhara makubwa kwa jamii kama vifo na ulemavu kwa raia wasio na hatia.
Kudhibiti
Dk Mcomalla anasema unahitajika ushirikiano wa wadau wengi ili kudhibiti uingizaji holela wa silaha, kwani wamebaini katika utafiti wao kuwa baadhi ya mapori ambayo yalitumika kama kambi za wapigania uhuru hasa ya maeneo ya mipakani.
“Tunapaswa kuwa na udhibiti wa wahamiaji na hapa tunaona ni vyema kuboresha utaratibu wa polisi jamii ili wananchi wawe na fursa ya kutoa taarifa kwa polisi mara kwa mara,” anasema
DCI Athumani anasema ukubwa wa nchi ni moja ya changamoto kwani kuna silaha nyingi zinaingia kwa kificho na kwamba mikoa yote nchini ipo katika mchakato wa uhakiki ili kujua wamiliki halali na kusisitiza polisi wametoa miezi mitatu.
“Wananchi wenye silaha ambazo si halali wazisalimishe polisi, ofisi za Serikali au katika nyumba za ibada, hakuna ambaye atachukuliwa hatua,” anasema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Filex Ntibenda anasema mkoa huo ni miongoni mwa iliyopo mipakani na utaratibu wa uhakiki unakwenda vizuri. Kwa wilaya moja ya Ngorongoro, bunduki 103 zimehakikiwa zikiwamo zilizokuwa zikitumika kwa uhalifu.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas anasema katika uhakiki huo wamefanikiwa kukamata hata silaha za kivita ambazo zilikuwa mikononi mwa wahalifu.
“Tunawaomba kuzileta polisi silaha zote ili zihakikiwe, ambao hawamiliki kihalali wazisalimishe,” alisema na kuonya kuwa muda wa miezi mitatu utakapomalizika watakaokamatwa katika msako watachukuliwa hatua za kisheria.
“Tunaomba wananchi watuunge mkono kuhakiki silaha zao zote, zoezi ambalo litasaidia kujua kiwango cha silaha kilichopo mikononi mwa raia na kuwa na mfumo mzuri wa kumbukumbu zao,” alisema.
Athumani anasema Tanzania ni moja ya nchi zilizopo katika mchakato wa kuweka alama za utambulisho wa silaha zake (NACN) ili kujua zinakotoka kwa nchi wanachama wa jumuiya mbalimbali.
Pia, ni mwanachama wa taasisi za udhibiti wa silaha na imesaini makubaliano kadhaa, yakiwamo ya kuzuia biashara haramu ya silaha.
Mkurugenzi huyo anasema kuna sheria ambazo tayari zimepitishwa na Serikali katika suala la udhibiti wa silaha, mojawapo ni udhibiti na matumizi ya silaha ya mwaka 2015. Yote yanafanyika chini ya Sera ya Kudhibiti Silaha (NPFC) ya mwaka 2011 .

No comments:
Post a Comment