Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Eng. Patric Mfugale kuhusu kukamilika kwa upanuzi wa barabara ya Morocco-Mwenge KM 4.3.
Mafundi wa kampuni ya Estim Construction wakiendelea na Ujenzi wa barabara ya Mwenge –Morocco KM 4.3 ambayo ni sehemu ya Barabara ya Morocco –Mwenge-Tegeta.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa wiki mbili kwa
mkandarasi ESTIM Construction anayejenga barabara ya Bagamoyo, Sehemu ya Morroco-Mwenge
kilomita 4.3 kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.
Akizungumza
mara baada ya kukagua barabara hiyo, Prof. Mbarawa amesema baada ya wiki mbili
barabara hiyo itafunguliwa kwa ajili ya matumizi ili kupunguza msongamano wa
magari yanayoingia na kutoka katikati ya
jijini.
“Hakikisheni
barabara hii inakamilika ndani ya wiki mbili, ili msongamano wa magari
yanatoingia na kutoka katika ya jiji upungue, na hivyo kuiunganisha vizuri
barabara hii na ile ya Mwenge-Tegeta”. Amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha amewataka
waananchi na madereva wanaotumia barabara hiyo kulinda mazingira kwa kuepuka
vitendo vya
kumwaga mafuta kwenye barabara hiyo na kutupa takataka zinazosababisha mifereji
iliyo pembezoni mwa barabara kuzipa na kuharibu barabara hiyo.
“Nawataka
watumiaji wa barabara, kuzingatia matumizi sahihi ya barabara, tunawekeza fedha
nyingi katika ujenzi wa barabara mijini ili kuondoa msongamano hivyo zingatieni
matumizi sahihi ya barabara ili zidumu kwa muda mrefu”. Amesema Prof. Mbarawa.
Naye Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Eng. Patrick Mfugale
amemhakikishia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwa ili kupunguza
msongamano ujenzi wa barabara hiyo umelazimika kuweka sehemu maalum za watembea
kwa miguu kutokana na wingi wa watumiaji wa barabara hiyo katika sehemu hiyo na
kupanua maingilio ya barabara ili kurahisisha magari kutoka na kuingia katika
barabara hiyo.
Eng. Mfugale
amesema zaidi ya magari 15,000 yanakadiriwa kuwa yatapita katika barabara itakapokamilika
na hivyo kupunguza msongamano mkubwa uliokuwepo katika eneo hilo.
Takribani shilingi
bilioni 4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo na hivyo kuiunganisha
barabara ya Mwenge-Morroco na ile ya Mwenge-Tegeta.
Katika hatua
nyingine Prof. Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), kufanya
tafiti na kuangalia fursa zitakazoiwezesha kupata mapato kutokana na kazi
inazozifanya.
Amesema iwapo
Mamlaka hiyo itafanya kazi kwa uadilifu na uaminifu itaongeza idadi ya watu
inaowahudumia kwa mwaka nchini na hivyo kusaidia wadau mbalimbali wa sekta za
Kilimo, Ujenzi, Afya, Uvuvi kufanya kazi kwa faida.
Prof. Mbarawa
amekagua vitengo cha takwimu za hali ya hewa, hali ya hewa ya kilimo na Utabiri
na kusisitiza kuwa ni wakati wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa teknolojia ya
kisasa ili kuhudumia wadau wengi kwa wakati mmoja.
“Hakikisheni
taarifa zenu zinawafikia watu wengi hususan wale wanaozihitaji taarifa hizi kwa
kutekeleza shughuli zao kiuchumi”. Amesema Prof. Mbarawa.
Naye
Mkurungenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa
Mamlaka hiyo inafanya utabiri kwa
usahihi wa asilimia 80 na ni miongoni mwa Mamlaka inayofanya vizuri katika
huduma za utabiri barani Afrika.
“Taarifa zetu
ni sahihi na kila baada ya dakika 15 tunatoa taarifa zinazoonyesha hali ya hewa
nchini”. Amesema Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi
amesema mamlaka hiyo imejipanga kuongeza uelewa wa watumiaji wa hali ya hewa
hapa nchini ili kuwezesha wadau wa hali ya hewa kunufaika kikamilifu na utabiri
unaotolewa na Mamlaka hiyo.
Imetolewa na
Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano,
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini..
No comments:
Post a Comment