Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ameamuru kukamatwa na kuswekwa rumande Ofisa Utumishi wa Jiji la Mwanza, Henry Sadatale kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuhusu wafanyakazi hewa.
Hatua hiyo inakuja siku nne tangu uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza kubaini kuwa jiji hilo lina wafanyakazi hewa watano kinyume na taarifa iliyowasilishwa ofisini kwa mkuu huyo wa mkoa iliyoeleza kuwa hakuna watumishi hao.
Akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Nyamagana, wakuu wa idara na watumishi wa Jiji la Mwanza jana, Mongella alisema uchunguzi unaoendelea umebaini jiji hilo lina wafanyakazi hewa ambao licha ya kutokuwapo kazini tangu 2008, lakini mishahara yao inaingizwa benki na kuchukuliwa.
“Mfano kuna mwalimu John Mihambo wa Mkolani Sekondari aliyeacha kazi mwaka 2008, lakini hadi juzi akaunti yake ya benki imekutwa ina Sh8 milioni zilizolipwa na Serikali kama mishahara,” alisema Mongella.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini pia kuna baadhi ya watumishi wa idara ya elimu ambayo ni kinara wa watumishi hewa pamoja na idara za fedha na utawala wanaghushi fomu za mikopo na hati za mishahara kwa majina ya walimu ambao hawako kazini na kuchukulia mikopo kwenye taasisi mbalimbali za fedha.
Mkuu huyo wa mkoa alitumia fursa hiyo kumuagiza Kaimu Ofisa Utumishi wa Jiji, Sigrifid Kaunara kushirikiana na wakaguzi wanaohakiki upya taarifa za watumishi hewa huku akionya kwamba akienda kinyume, naye atakamatwa na kushtakiwa.
“Ukitaka kumfuata mwenzako magereza jaribu kuficha taarifa kuhusu wafanyakazi hewa,” alionya Mongella.
Aliwataka viongozi na watumishi wa Jiji la Mwanza aliloliita kioo cha mkoa huo kufanya kazi kwa uadilifu, nidhamu na uwajibika huku akiwaonya kuwa hakuna mtumishi yeyote atakayepona katika awamu hii kama hatatimiza wajibu wake.
Alisema Mkoa wa Mwanza unafanya kazi ya uhakiki wa wafanyakazi kwa kupitia hati za malipo ya mishahara kuanzia Januari hadi Machi. Kazi hiyo itafuatiwa na uhakiki wa kupitia mfumo wa kisasa wa Biometric Identification Registry (BVR).
Aliwageukia madiwani na kusema ni viongozi wa kisiasa ambao ni wasimamizi na waidhinishaji wa shughuli za halmashauri, hivyo wasifanye kazi kwa mazoea.
Aliwataka waanze kuhoji kila taarifa na mipango kazi inayowasilishwa na watendaji wa halmashauri kwenye mabaraza yao ya madiwani.
“Muda umefika kwa waheshimiwa madiwani kuacha kuangalia posho wakati wa vikao, badala yake mjielekeze kupitia na kukagua kikamilifu kila taarifa inayofikishwa kwenye vikao vyenu kwa sababu ndiyo kazi mliyotumwa na wapigakura,” alisema Mongella.
Alitolea mfano mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kuleana cha jijini Mwanza kinachosimamiwa na halmashauri ya jiji uliogharimu zaidi ya Sh19 milioni kuwa uchunguzi umebaini ungegharimu Sh2 milioni, lakini hakuna diwani aliyehoji matumizi hayo makubwa yametoka wapi.

No comments:
Post a Comment