Wakati Serikali ikiendelea kuchunguza mikataba kati ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) kuhusu Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ametia pilipili kidonda kwa kuibua udanganyifu unaolizunguka shirika hilo.
Kwenye ripoti yake ya mwaka wa fedha 2014/2015 aliyoitoa bungeni Jumatatu, CAG Profesa Mussa Assad amebainisha kwamba Dart ilifanya makubaliano na msimamizi wa uendeshaji, Uda-RT kutoa huduma ya mpito ya usafiri kwa kutumia mabasi 76 yenye vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba.
Tofauti na makubaliano hayo, Uda ilinunua mabasi 140 ambayo yalikuwa na nembo ya Uda-RT badala ya Dart kinyume na vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba.
Meneja wa Miundombinu wa Dart, Mhandisi Mohamed Kuganda alisema wenye taarifa sahihi ni Uda-RT.
Hata hivyo, alikiri kufahamu ununuzi wa mabasi hayo na kusema waliwauliza Uda-RT na wakajibiwa kuwa, “barabara za kutumika mabasi hayo zipo nyingi.”
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group na Uda-RT, Robert Kisena alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa limeelekezwa serikalini: “Hoja za CAG zinaihusu Serikali hivyo siwezi kujibu.”
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Msajili wa Hazina Lawrence Mafuru alisema Serikali hairidhishwi na uendeshwaji wa Uda, lakini haina la kufanya.
Alifafanua kuwa Serikali haijawahi kujitoa katika umiliki wa shirika hilo na kwamba bado inazo asilimia 49 ya hisa zote na Simon Group ina asilimia 51 zilizobaki.
Alieleza kuwa uendeshaji wa shirika hilo: “Hauna utawala bora.” Hata hivyo, alisema ni vigumu kwa sasa kumiliki shirika hilo kwa asilimia 100 kwa sababu wenye hisa nyingi ndiyo wenye uamuzi.
“Tulichukuaje hilo shirika? Labda kama wenzetu watakubali kutuuzia hisa, vinginevyo hatuwezi kuwanyang’anya,” alisema.
Uchunguzi wa CAG
Akikumbusha juu ya ufuatiliaji baada ya ubinafsishaji, CAG ameiambia Serikali kuwa hisa za Uda ambazo hazikugawiwa, ziliuzwa kwa kampuni ya Simon Group kwa Sh1,142,643,935.
Alisema kampuni hiyo ililipa asilimia 24.9 tu ya makubaliano ya bei ya mwanzo, Sh285 milioni kwenye akaunti ya Uda yenye namba 01J1021393700 iliyopo Benki ya CRDB. Ripoti inasema hakuna ushahidi wa malipo ya asilimia 75.1 ambazo ni sawa na Sh858 milioni zilizobakia.
CAG amebainisha pia kuwa aliyekuwa mwenyekiti wa Uda, Idd Simba alipokea Sh320 milioni alizowekewa katika akaunti yake binafsi kwa ajili ya huduma ya ushauri wa kitaalamu kutoka Simon Group Limited.
Utata uliopo ni kwamba Simon Group inadai kuwa kiasi hicho: “Ni sehemu ya malipo ya mauzo ya hisa za Uda.”
Akizungumzia suala hilo hivi karibuni, CAG mstaafu Ludovick Utouh alisema anashangaa kuona Uda ikiuzwa na fedha zake kuwekwa kwenye akaunti ya mtu binafsi kitendo ambacho ni kosa la jinai lakini kesi hiyo ilifunguliwa na kisha kufutwa.
Ingawa mwaka 2013 aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi aliwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kuwashtaki Idd Simba na wenzake, CAG ameendelea kuishauri Serikali kupitia Msajili wa Hazina kufuatilia kwa karibu juu ya ubia wake ndani ya Uda ili kuhakikisha: “Maslahi ya umma hayapotei.”
Hata hivyo, Mafuru alisema kwa kuwa kesi iliyokuwa mahakamani imekwisha na uamuzi umeshatolewa, itakuwa vigumu kulirejesha serikalini shirika hilo. “Kesi zilizokuwa mahakamani zimekwisha ndiyo maana ninaweza kuzungumzia… Uda inaendelea kufanya kazi.”
Simba, aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika awamu ya tatu, alishtakiwa pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo, Salim Mwaking’inda na Meneja Mkuu, Victor Milanzi na Mkurugenzi wa Simon Group Limited, Simon Kisena, kwa kosa la uhujumu uchumi.
Kupuuzwa mapendekezo
CAG alisema alitoa mapendekezo ya kukiukwa kwa kanuni za uuzaji wa hisa hizo tangu mwaka 2011/2012 lakini yalipuuzwa. Alisena Uda iliuzwa bila kibali cha Serikali na hisa zilithaminishwa kwa Sh744.79 kwa kila moja Oktoba 2009, lakini Novemba 2010, zikashushwa mpaka Sh656.15.
Hata hivyo, katika uuzaji, Bodi ya Wakurugenzi ya Uda ilitoa punguzo la asilimia 60 kwa kila hisa kwa mwekezaji huyo. Bodi ilizingatia tathmini ya Oktoba 2009 bila kuwapo na sababu za kufanya hivyo.
CAG alisema: “Kwa mujibu wa majibu ya Mlipaji Mkuu wa Serikali, Serikali haitambui uuzwaji wa hisa hizo.”
Uda ni moja ya mashirika 158 yaliyokaguliwa na CAG kwa mwaka wa fedha uliopita kati ya 185 yanayostahili.
UDA
Licha ya tahadhari iliyotolewa mwaka jana na wabunge wa upinzani juu ya uharamu wa kuuzwa kwa hisa za Uda, ripoti ya CAG imeweka wazi kilichokuwa kinaelezwa.
Kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wa Kibamba, John Mnyika walisema shirika hilo liliuzwa kwa: “Bei ya kutupwa.”
No comments:
Post a Comment