ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 28, 2016

DUDU JINGINE BANDARI YA DAR

Ticts ni kampuni ya kimataifa ya huduma za makontena inayosimamia na kuhifadhi makontena katika bandari ya Dar es Salaam.Pia ni mwanachama wa kampuni ya kimataifa ya CK Hutchison Holdings inayofanya kazi katika bandari 52 kwenye nchi 26 duniani. 

Baada ya kuibuka sakata la mita za kupimia mafuta na ukwepaji wa kodi kwa makontena bandarini, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebainisha kashfa nyingine kwenye kitengo cha mizigo kinachoendeshwa na Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Makontena (Ticts).
Ripoti hiyo iliyotolewa mapema wiki hii imebaini Ticts imevunja taratibu za mkataba na hivyo kusababisha kuikosesha mapato Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA).
CAG Mussa Juma Assad ameonyesha katika ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma kuwa Ticts ilianza kuvunja makubaliano ya mkataba na TPA baada ya kubadilisha umiliki wa asilimia 51 wa hisa za Ictis zilizoko kampuni ya Ticts kwenda Hutchison International Port Limited (HPH).
TPA iliingia makubaliano kwa upande mmoja na Ticts na kampuni ya Huduma za Makontena ya Kimataifa (Ictis) Mei, 2000 ili kuendesha na kusimamia kitengo cha makontena na ghala lililopo Kurasini jijini Dar es Salaam kwa miaka 10.
Katika mkataba huo ulioanza utekelezaji Septemba 2000, Ticts ilitakiwa kuilipa TPA dola 3.68 milioni za Marekani (Sh7.9 bilioni) zilizotakiwa kulipwa siku ya kwanza ya mkataba kwa miezi 12 iliyofuata.
Hata hivyo, CAG katika ripoti yake iliyotolewa hivi karibuni alisema kuwa hisa hizo za Ictis zilihamishwa Oktoba 2001, ikiwa ni siku 20 tu baada ya kusainiwa mkataba wa upangishaji wa kitengo cha makontena.
Profesa Assad pia amebaini kuwa mkataba huo ulifanyiwa mabadiliko ya pili Desemba 30, 2005, ikiwa ni miaka mitano kabla ya mkataba kumalizika na kuongeza miaka ya upangaji kutoka 10 ya awali hadi miaka 25 kinyume na makubaliano.
Mbali na kubadilisha muda wa upangaji, TPA ilifanya makubaliano na Ticts na kuongeza eneo la kazi na kuchukua sehemu yote ya gati Namba 8 na maeneo yote ya jirani na kupatiwa bandari kavu ya kuhifadhia makontena ya Ubungo ambayo haikuwepo kwenye mkataba wa upangishaji.
“Kutokana na kifungu Namba 9.1 cha mkataba wa upangishaji, mabadiliko ya muda wa mkataba wa upangishaji hayaruhusiwi,” anasema Profesa Assad katika ripoti yake ya ukaguzi ya mwaka 2014/15.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa hata upangishaji wa maeneo ya makontena ya Ubungo na Kurasini hayakuzingatia nia njema ya ubinafsishaji uliolenga kuongeza ufanisi kwa mashirika ya umma kwa kuwa tayari maeneo hayo mawili yalikuwa yakifanya kazi kwa ufanisi.
Pamoja na kwamba Ticts bado ni mbia wa TPA, mwaka 2007 kampuni hiyo ilishawahi kushuka kiwango cha ufanisi cha asilimia 26 kilichopo kwenye mkataba kinachoruhusu utenguzi wa mkataba huo.
Profesa Assad anabainisha kuwa Ticts ilikiri kushuka huko kwa ufanisi na kusababisha Bodi ya Wakurugenzi ya TPA kupendekeza mapitio ya mkataba huo kwa wizara ya miundombinu, ikiwamo kuondolewa kipengele cha upekee, kuongeza kiwango cha ufanyaji kazi na kiwango cha malipo ya mrabaha.
Mapendekezo mengine ya bodi hiyo, yaliyoendana na nia ya kutoa notisi kwa Ticts kutokana na kushuka kwa ufanisi, yalikuwa ni kuitaka kuwasilisha mpango wa uwekezaji utakaojumuisha ununuzi wa vifaa vipya vya kazi na kuongezea kipengele cha upitiaji mkataba kwa kila baada ya miaka mitano.
Hata hivyo, Profesa Assad anasema Serikali ilitoa maelekezo kwa TPA isitoe notisi hiyo kwanza mwaka 2008, badala yake wafanye majadiliano kati ya pande mbili yaliyozalisha mapitio ya mkataba wa mwaka 2009 na kufanikisha kusainiwa kwa randama ya mpango kazi wa kuongeza ufanisi Oktoba mwaka huo.
CAG ameendelea kufichua kuwa Ticts haijatekeleza agizo la mkataba la kuitaka kupanua umiliki wake kwa wananchi kwa kuuza asilimia 40 ya hisa zake kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Profesa Assad alisema kifungu namba 6.1.6 cha mabadiliko namba mbili ya mkataba yaliitaka Ticts kuongeza umiliki wa kampuni hiyo kwa kuuza hiza zake ifikapo 31 Desemba 2011.
“Hata hivyo, hadi nakamilisha ripoti hii Februari 2016 sikuweza kupata uthibitisho iwapo hisa za Ticts zimeuzwa kwenye soko la hisa kwa Watanzania kama inavyotakiwa kwenye mkataba wa upangishaji,” alisema.
Jana DSE ilisema haijapokea ombi lolote kutoka Ticts la kuuza hisa hizo kupitia Mamlaka ya Masoko ya Dhamana na Mitaji (CMSA) licha ya kufahamu kuwa kuna kifungu cha mkataba baina yake na TPA kinacholazimisha hivyo.
CAG pia alibaini kuwa TPA imekuwa ikikabiliwa na ugumu wa kusimamia ipasavyo mapato yanayokusanywa na Ticts kutokana na kukosa haki ya kuingia kwenye mfumo wa kompyuta wa Tancis ambao humilikiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Profesa Assad anasema kuwa TPA haina chombo chochote kinachosimamia na kufahamu idadi ya makontena yaliyopokelewa na kuhifadhiwa na Ticts na kwamba imekuwa ikitegemea taarifa zinazotoka kampuni hiyo.
“TPA haifanyi usawazishaji wa taarifa halisi za makontena yanayotunzwa na kusimamiwa na Ticts mara baada ya kupata taarifa hizo,” anasema mkaguzi huyo na kueleza kuwa majibu ya TPA yalikuwa kwamba hawapati haki ya kuingia kwenye mfumo wa Tancis.
Profesa Assad amependeleza Serikali iruhusu TPA kupata haki kuingia kwenye Tancis ili kufuatilia taarifa za makontena yanayosimamiwa na Ticts na menejimenti ya mamlaka hiyo ifuatilie kikamilifu masuala ya kampuni hiyo ili kuhakikisha haivunji mkataba.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa sehemu kubwa ya malengo waliyojiwekea kuongeza ufanisi hayatekelezwi ipasavyo kutokana na kuwa na bajeti ya maendeleo isiyo halisi ambayo kati ya Sh4.24 trilioni zinazotakiwa kutekeleza mpango mkakati wa TPA, asilimia 85 zinategemewa kutoka nje kupitia wadau wa maendeleo na wabia.
Akielezea utegemezi taarifa kutoka Ticts katika kukokotoa tozo zinazostahili na uwezekano wa TPA kupoteza kiasi kikubwa cha mapato, Janeth Ruzangi, msemaji wa mamlaka hiyo alisema: “Kipo kitengo maalumu kinachofuatilia.”
Alisema kuwa hana taarifa sahihi ya namna kinavyojiendesha kwa kufahamu changamoto ya kutokuwa na fursa ya kuingia kwenye mfumo wa Tancis wa TRA.
Kuhusu mabadiliko ya mkataba, alisema: “Yalikuwa maamuzi ya Baraza la Mawaziri.”
Alisema maamuzi hayo yaliongeza muda wa mkataba kutoka miaka 10 mpaka 25, jambo ambalo alisema lilikuwa nje ya uwezo wa mamlaka hiyo.
“Sisi ni watekelezaji tu. Serikali inapanga na kuamua kila kitu juu ya mkataba huu,” aliongeza Ruzangi.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, William Budoya aliomba muda ili kujiridhisha juu ya kuhamishwa kwa asilimia 51 ya hisa za Ictis kwenda Hutchison badala ya kuuzwa kwa Watanzania kama ilivyokubaliwa.
Akitambua ukiukwaji uliobainishwa na CAG, Budoya alisema mkataba ni suala la kisheria na kushauri kuwe na subira ili aupitie na kuona jinsi ya kushughulikia hoja zilizotolewa na CAG.
Alipotafutwa kwa simu ya mkononi ili aeleze ni kwa namna gani kampuni yake ilifanikiwa kuendelea na utekelezaji wa makubaliano licha ya kukiuka kanuni, meneja wa kitengo cha makontena wa Ticts, Donald Talawa alitaka kutumiwa maswali yote kwa barua pepe akisema hiyo ndiyo njia sahihi kwake kutoa taarifa ya ofisi anayoihudumia.
Alisema bado hajaipata ripoti ya CAG na kwamba anaisoma kupitia magazeti na vyombo vingine vya habari.
Nyongeza na Julius Mathias, Mwananchi; jmathias@mwananchi.co.tz

No comments: