ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 7, 2016

SOMA HAPA HISTORIA YA HAYATI ABEID AMANI KARUME


Na Ali Shaban Juma.
MIAKA 44 iliyopita hapo tarehe 7 Aprili, 1972 Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume aliuwawa kwa kupigwa risasi katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro-Shirazi hapo Kisiwandui mjini Zanzibar. Katika mfululizo wa makala haya mwandishi ALI SHAABAN JUMA anaelezea historia ya maisha ya Mwanamapinduzi huyo.

Bwana Abeid Amani Karume muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar alizaliwa katika kitongoji cha Pongwe, Mudiria ya Mwera kisiwani Unguja tarehe 4 Agosti 1905. Karume ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto watano ya Bwana Amani Karume na Bibi Amina binti Kadir (Amina Kadudu). Bwana Amani Karume na Bibi Amina Binti Kadudu walifunga ndoa huko Mwera.

Bwana Abeid Amani Karume alizaliwa na ndugu wanne wa baba mmoja na mama mmoja ambao ni wanaume wawili na wanawake wawili. Lakini wote walifariki kutokana na maradhi mbalimbali na kubaki yeye peke yake. Kwa upande wa mama mmoja, Abeid Amani Karume alizaliwa na ndugu watatu, wanawake wawili na mwanaume mmoja ambao ni Asha, Shumbana na Othman. Baba yake mzazi Abeid Amani Karume alifariki dunia mwaka 1909 wakati Abeid Amani Karume akiwa na umri wa miaka minne. Bwana Abeid Amani Karume alipata elimu ya Kurani na alianza masomo ya msingi katika skuli ya Mwera mwaka alofariki baba yake wa 1909, ambapo darasa lao lilikuwa la kwanza kuifungua skuli hiyo.



 Hapa ndipo alipouwawa Rais wa kwanza wa Zanzibar  Hayati Sheikh Abeid Amani Karume miaka 44 iliyopita ndani ya ofisi za Makao Makuu ya CCM Kisiwandui, Unguja, wakati akicheza bao na marafiki zake. Matundu yanayoonekana ukutani ni ya risasi ambayo muuaji alimimina kabla na yeye kuuwawa kwa kupigwa risasi na walinzi wa Hayati Karume. Sehemu hii imewekwa uzio maalumu ili kupahifadhi kama kumbukumbu, kwani kila kitu kipo vile vile kilivyokuwa siku hiyo

Katika mwaka 1913 wakati akiwa na umri wa miaka 8 mama yake mzazi alimpeleka mjini Unguja kuendelea na masomo. Huko aliishi na mjomba wake aliyekuwa Sajenti katika jeshi la polisi la King African Rifle (KAR). Kwa bahati mbaya muda wake wote wa masomo ulikuwa miaka mitatu. Akiwa mjini Zanzibar Abeid Karume alipata marafiki kadhaa na kuvutiwa mno na harakati za bandari ya Zanzibar.


Kwa wakati huo, bandari ya Zanzibar ndiyo iliyokuwa kubwa Afrika mashariki. Pia Zanzibar, ilikuwa ndiyo kituo kikuu cha biashara katika eneo zima la Afrika mashariki na Maziwa Makuu.

Meli za mataifa ya nje hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa na Italia zilitia nanga bandarini Zanzibar kupakia na kupakua bidhaaa mbalimbali. Pia meli nyingi zilifika Zanzibar kuchukua maji safi ya kunywa yatokayo katika chemchem ya Mwanyanya. Meli hizo zilitoa ajira ya muda ya kusafisha mashine na kupangusa moshi. Mara nyingi mabaharia wa meli hizo waliajiri watoto kuwachukulia vikapu vya kununulia vyakula sokoni na kuwalipa ujira mdogo.

Kwa vile alipendelea kazi ya ubaharia, Abeid Amani Karume alifuatana na bwana mmoja aitwae Juma hadi bandarini. Alijumuika na watoto kadhaa waliofuata ajira ya muda huko bandarini. Ajira ya muda aliyoipata Karume huko bandarini ilimfanya akutane na mabaharia wa nchi mbalimbali na hivyo kuvutiwa na uzuri wa maisha ya ubaharia ya kusafiri na kuona nchi na watu mbalimbali. Hali hiyo ilimfanya Karume azidi hamu na ari ya kutafuta kazi ya ubaharia na kumuomba mama yake ruhusa ya kufanya kazi melini. Mwanzoni mama yake mzazi alikataa shauri hilo. Lakini baadaye alikubali ombi hilo baada ya kufahamishwa kuwa meli atakayofanyakazi mwanawe haitosafiri mbali na itatia nanga bandarini Zanzibar mara kwa mara.

BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI

1 comment:

Anonymous said...

King African Rifles lilikuwa ni jina la Jeshi la Ulinzi la Makoloni ya UIngereza katika Afrka; halikuwa Jeshi la Poloisi!Jina rasmi: King African Rifles.