ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 28, 2016

Supastaa wa Malawi Tay Grin awapania Diamond na Vanessa

Rapper na supastaa wa Malawi, Tay Grin, amedai kuwa ana mpango wa kuwashirikisha Diamond Platnumz na Vanessa Mdee. Tay ambaye hivi karibuni aliachia video ya wimbo ‘Chipapapa’aliomshirikisha msanii wa Nigeria, 2 Face Idibia, amesema kuwa hao ni wasanii wa Tanzania anaowakubali zaidi.

“Ningependa sana kufanya kazi na wasanii wa Tanzania,” anasema Tay.

“Napenda jinsi wasanii wa Tanzania wanavyoimba. Ni kimuziki sana hata kama sizungumzii Kiswahili, muziki wao unasikika vizuri na ni mtamu. Nimesikiliza wasanii kama Vanessa Mdee, Diamond Platnumz, Alikiba na muziki wao wa Bongo Flava. Nadhani Nyau Music inaweza kuchanganyikana vizuri na wasanii hawa wakali. Kwa sasa ninafanyia kazi wimbo na Vanessa Mdee na nina matumani ya kumpata Diamond Platnumz kwenye wimbo huo,” ameongeza.

Tay amesema anawakubali wawili hao kutokana na jinsi wanavyojituma na mapenzi yao makubwa kwenye muziki.

“Nimekuwa nikifuatilia kazi zao kwa muda sasa na naweza kusema kuwa wamenishika.”

Tay ni msanii anayeheshimika zaidi nchini Malawi na amewahi kutumbuiza mara mbili kwenye shindano la Big Brother Africa na amewahi kutajwa zaidi ya mara tano kuwania tuzo za Channel 0.

Amewahi kushirikisha wasanii kama Sway (UK), Brick & Lace (Jamaica), Naeto C, Ice Prince, na 2face wa Nigeria), Wahu na Nameless wa Kenya, Double HP, Da Les na Lira wa Afrika Kusini na wengine.

No comments: