ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 12, 2016

Tanga yabaini VVU, utapiamlo shuleni


Ni kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali la Kanisa Katoliki la Pasadit, linaloendesha mradi wa Pamoja Tuwalee na Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Taasisi hizo zilipata takwimu hizo baada ya kuwapima kwa hiari VVU na kuwachunguza hali ya lishe wanafunzi wa shule hizo pamoja na kuwapa elimu ya lishe bora.

Takwimu zilizotolewa na wadau hao zilionyesha kwamba wanafunzi 15 wanaishi na VVU na wanatumia dawa wakati 30 ni wale wenye maambukizi mapya.

Akizungumza katika mahojiano na Nipashe, Mratibu wa Ukimwi Halmshauri ya Jiji la Tanga, Mosses Kisibo, alisema wanafunzi 5,527, wavulana 2,544 na wasichana 2,983 waliochunguzwa kwa hiari, 15 walikuwa wakiishi na VVU na wanatumia dawa.

Kisibo aliongeza kuwa kati ya hao wanafunzi 30 walikutwa na maambukizi mapya na idadi ya wavulana waathirika ni 21 na wasichana ni tisa.

Kwa upande wa utapiamlo, wanafunzi hao wanatoka kwenye shule 18 za msingi na moja ya sekondari zote za jijini Tanga na kwamba wamebainika kuwa wana lishe duni inayoathiri ukuaji wa mwili na akili.

Kwa upande wa utapiamlo utafiti uliofanyika shuleni ulibaini kuwa wanafunzi 1,927 walikuwa na dalili ya utapiamlo kati yao wavulana ni 1,125 na wasichana 802. Kwa ujumla 135 walikuwa na utapiamlo wasichana wakiwa 53 na wavulana 82, kwa mujibu wa Pasadit Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Alisema waliochunguzwa ni wanafunzi wenye umri kati ya miaka 5 hadi 18 kutoka shule zilizopo kwenye kata za Nguvumali, Pongwe, Maweni, Usagara, Mnyanjani, Duga,Mzingani na Chumbageni.

“Upimaji huu ni endelevu kwani tumepanga kufikia shule zote zilizopo ndani ya halmashauri ya Jiji la Tanga, kikubwa ni kuwatambua ili aliyeathirika asaidiwe kuishi vizuri na kutunza afya yake sambamba na uhakika wa upatikanaji wa tiba na lishe bora,” alisema Mratibu.

Aliongeza kuwa hali ya maambukizi ya VVU jijini Tanga ni asilimia 3.8 na kimkoa ni asilimia 2.4 kwa kujibu wa takwimu za mwaka 2015/2016.

Pasadit inafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na wahisani wa World Education International na Shirika la Kimataifa la Misaada la Marekani (USAID) na Halmashauri ya jiji inayohusika na kutoa wataalamu.

NIPASHE

No comments: