Jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji ambayo yanaongoza kwa uchafu Tanzania.
Kutokana na hali ya uchafu inavyozidi kuwa kubwa kila siku kwenye jiji hili imepelekea kutokea kwa magonjwa ya milipuko mara kwa mara ikiwemo kipindupindu ambapo watu wengi hupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Rais Magufuli alionesha kuchukizwa na mazingira ya nchi kuonekana machafu, hivyo basi alitoa agizo la kuvunja sherehe za Uhuru na kuagiza kila mwananchi anatakiwa afanye usafi kwenye maeneo yake na fedha za kuandaa sherehe hizo alizipeleka kwenye utengenezaji wa barabara ya Morocco hadi Mwenge jijini la Dar es Salaam.
Aidha siku chache baada ya kuapishwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliitisha mkutano wa wenyeviti wote wa serikali za mitaa wa jiji la Dar es Salaam na kutoa agizo kwa viongozi hao kusimamia ipasavyo usafi ndani ya mitaa yao, pia aliahidi kutoa zawadi nono kwa mwenyekiti ambaye mtaa wake utaonekana kuwa msafi zaidi.
Hongera Mhe. Makonda kwa kufikiria na kuanzisha kampeni ya ‘Kataa Uchafu’ ambayo kwa asilimia kubwa itasaidia kupunguza uchafu, lakini tukumbuke kuwa hilo litawezekana endapo wananchi tukimuunga mkono mkuu wa mkoa kwa moyo mmoja ili kuhakikisha tunatokomeza uchafu kwenye jiji la Dar es Salaam ili kupunguza magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na uchafu.
Kutokana na kuonyesha kuunga mkono juhudi za mkuu wa mkoa, Clouds wameonekana kuwa mstari wa mbele kupinga uchafu kwa kuanzisha kampeni ya ‘Kuwa mstaarabu na usijifanye mstaarabu’.
Kuna maeneo mengi ndani jiji la Dar es Salaam kiukweli yanasifika kuwa na mazingira mabaya ya uchafu, hakika ukitajiwa Tandale, Bonde la Mpunga, Buguruni, Keko n.k ni sehemu ambazo kiukweli mazingira yake ni hatarishi kutokana na wananchi wake walio wengi wamekuwa kukitupa uchafu sehemu zisizo stahili.
Mjini kuna mapipa mengi ya uchafu yamewekwa lakini kutokana na kukosa ustaarabu watu tulio wengi tunatupa uchafu barabarani na kwenye mitaro ya kupitishia maji machafu na kuyaacha mapipa hayo ya kuwekea uchafu yakiwa hayana uchafu.
Tukumbuke kuwa sababu nyingine ya kupata mafuriko ni utupaji hovyo wa takataka kwenye mitaro ambazo zinasababisha kuziba kwa mitaro hiyo na kufanya maji kushindwa kufuata njia yake na kuanza kuingia kwenye makazi ya wananchi.
Nakumbuka alipokuja rais Obama baadhi ya maeneo aliyopitia kwenye jiji la Dar es Salaam yalionekana kuwa ni masafio lakini pia hata barabara zilionekana kudekiwa ikiwa ni kitu ambacho hakijawahi kutokea.
Tukiamua tunaweza tuungane kwa pamoja kwa kumuunga mkono rais Magufuli na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhakikisha Tanzania yote inakuwa safi.
No comments:
Post a Comment