Mbunge wa Mtambwe (CUF), Khalifa Mohamed Issa ametaka kujua kama Serikali haioni kuruhusu ndege kuongozwa na rubani mmoja ni sawa na kuyaweka rehani maisha ya abiria.
Akijibu swali hilo jana bungeni, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema taratibu zinazoongoza fani ya kuendesha ndege nchini huongozwa na miongozo inayokubalika kimataifa ambayo imeridhiwa na Bunge.
Alisema kuna matakwa ya kisheria na kiufundi ambayo yakifuatwa yanaweza kuwa na uwezekano mdogo wa kukumbwa na athari ya kiafya na kushindwa kumudu kuendesha ndege.
“Marubani hupimwa afya zao na madaktari bingwa kila muda maalumu kulingana na umri kama ilivyoainishwa katika kanuni ya 140 mpaka 177 ya Sheria ya Anga kuhusu kanuni za (leseni binafsi) 2012,” alisema Ngonyani.
Hata hivyo, alisema Serikali inaruhusu ndege kuendeshwa na rubani mmoja kwa kuzingatia taratibu hizo na kanuni ya 32(5) ambayo inasema ndege iliyoandikishwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuruka kwa shughuli za kibiashara yenye uzito unaozidi kilo 5,700 itakuwa na marubani wasiopungua wawili.
Alibainisha kuwa shughuli za usalama wa anga nchini zinaongozwa na sheria namba 80 na kanuni zilizotengenezwa chini yake ambazo zinasaidia kufanya mambo hayo kuwa na utaratibu mzuri katika kurusha ndege.
“Aidha urushaji wa ndege yenye abiria tisa au zaidi unaongozwa na kanuni ziitwazo za usalama wa anga, 2012 ambapo ndege inayotimiza vigezo vilivyowekwa kwenye vifungu(2), (3) na (4) vya kanuni ya 32 kuwa na uzito wa chini ya kilogramu 5,700 inaruhusu kuendeshwa na rubani mmoja,” alisema Naibu huyo
Hata hivyo, alisema katika viwango vinayotolewa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) kwenye kiambatanisho namba 19, chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga wa Chicago, hakuna kiwango chochote kinachobainisha wazi kuwa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 10 au zaidi ni sharti iendeshwe na marubani wawili.

No comments:
Post a Comment