ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 21, 2016

BENKI YA DUNIA YAMPA JPM MAMBO SITA

 Benki ya Dunia imezindua ripoti mpya ya hali ya kiuchumi ikionyesha mwenendo imara wa ukuaji wake nchini, lakini ukiawaacha Watanzania zaidi ya milioni 12 wakiishi katika umasikini wa kutopea.
Benki ya Dunia, ambayo inasifu juhudi za Rais John Magufuli kukusanya kodi, kupambana na ufisadi na kuondoa uzembe, inasema katika ripoti hiyo kuwa ili ukuaji huo wa uchumi uendane na ustawi wa jamii, Serikali inatakiwa kufanya mambo sita ambayo yatasaidia kuimarisha ubia baina yake na sekta binafsi (PPP) kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu na huduma kwa jamii.
Ripoti hiyo inayoitwa “The Road Less Travelled: Unleashing Public Private Partnership in Tanzania”, ilizinduliwa jana jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alisema Serikali inakubaliana na ripoti hiyo na mapendekezo yaliyomo na kwamba inaandaa mazingira mazuri ya kuhakikisha sekta binafsi inashirikishwa kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kuinua hali ya maisha ya watu.
Ripoti hiyo iliyojikita katika namna Tanzania inavyoweza kuchagiza maendeleo kwa kutumia ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi, imesema wananchi hao maskini wanaishi chini ya Dola 0.6 ya Marekani (sawa na Sh1,300) kwa siku, kinyume na kiwango kinachotakiwa cha Dola 1.9 za Marekani, ambazo ni sawa na Sh4,000.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird alisema Watanzania milioni 10 ndiyo ambao si maskini wapo juu ya mstari wa umaskini kwa asilimia 10 tu, hivyo wapo hatarini kurudi tena katika umaskini wa kutopea iwapo utatokea mtikisiko wa kiuchumi.
Alisema idadi hiyo ya maskini inaonekana kutobadilika sana kutoka ile ya mwaka 2007 kutokana na kasi ya ongezeko la idadi ya watu nchini.
Ripoti hiyo ya nane imesema uchumi wa Tanzania unatabiriwa kukua kwa kiwango cha asilimia saba kwa mwaka katika kipindi cha miaka miwili ijayo, wakati kasi ya kuongezeka kwa bei ya bidhaa na huduma inatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia tano.
“Hata hivyo, ukuaji huo uchumi wa asilimia saba utakuwa na mchango mdogo katika mapambano na umaskini iwapo kitatumika kipimo cha Dola 1.9 za Marekani kwa siku,” inasema ripoti hiyo.
“Kiwango hicho cha umaskini kinatabiriwa kushuka kutoka asilimia 41 ya mwaka 2015 hadi asilimia 39 mwaka huu,” inabainisha ripoti hiyo na kuonya kuwa makadirio hayo ni iwapo bei za bidhaa ulimwenguni zitabaki kama zilivyo na uchumi wa China hautaendelea kuyumba.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa Tanzania bado inasuasa katika maendeleo ya miundombinu na huduma za kijamii kutokana na kukosekana kwa fedha za kutosha, hivyo PPP itasaidia kupunguza mwanya wa kibajeti kugharamia masuala hayo.
Benki hiyo imesema kuwa Tanzania ina mifumo na uzoefu wa PPP lakini kuna mengi yanatakiwa kufanyika ikiwamo kutekeleza mambo sita ambayo yataimarisha ushirika huo kama ambavyo Brazil, India, Chile na Mexico zilivyofanikiwa kukusanya asilimia 25 hadi 30 za fedha zake kutoka sekta binafsi.
Mambo hayo ni pamoja kuchagua kwa makini aina ya miradi ya kushirikiana kwa mujibu wa mahitaji ya utekelezaji kifedha na ambayo yana mvuto kwa sekta binafsi.
Uchambuzi huo wa kina umeelezwa kuwa utasaidia kung’amua iwapo mradi huo unatekelezeka, unawavutia wawekezaji wa sekta binafsi na unaendana na thamani ya fedha zitakazotumika.
“Miradi ya PPP si dawa ya magonjwa yote na sehemu kubwa ya miradi hiyo haifai kutekelezwa kwa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kwa kuwa baadhi ya matatizo hayawezi kutatuliwa kwa mfumo huo,” inasema ripoti hiyo.
Pia, benki hiyo imeshauri kuwa kuna ulazima wa kuanzisha mfumo imara wa kitaasisi na kiudhibiti utakaosaidia kuimarisha utekelezaji wa miradi ya PPP.
Ripoti hiyo ya kurasa 62 inaeleza kuwa Serikali lazima ijiimarishe katika njia zitakazosaidia kuimarisha taasisi za kusimamia ubia na sekta binafsi ikiwamo kuanzisha kituo maalumu cha PPP ambacho kinatakiwa kiendeshwe na mtendaji mkuu mwenye uzoefu.
Mbali na kuimarisha mfumo huo, WB imesema kuwa miradi ya PPP inatakiwa kuwa na maandalizi mazuri katika utekelezaji wake kwa kutoa vyema rasilimali fedha na watu ikiwamo kupokea ushauri wa kitaalamu.
Kama ambavyo ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikisisitiza, Benki ya Dunia nayo imesema kuwa miradi ya PPP haitafanikiwa iwapo hakutakuwa na ushindani na uwazi katika kutafuta wabia kutoka sekta binafsi.
Inasema ushindani wa zabuni na uwazi vinasaidia kupata kampuni bora kutoka kwenye sekta binafsi na kuisaidia Serikali kuwa na miradi mikubwa inayoendana na thamani ya fedha zinazowekezwa.
“Tanzania inapaswa kuanzisha sera itakayoongoza utoaji wa fedha zake katika miradi ya PPP ikiwamo kutoa dhamana na kuamua aina ya miradi itakayopata fedha hizo,” inashauri ripoti hiyo katika jambo la tano.
Pamoja na njia hizo, ripoti imeitaka Serikali kutoa elimu ipasavyo kwa umma na watumishi wake wa ngazi zote ili wafahamu mfumo wa utekelezaji wa miradi ya PPP.
Benki ya Dunia imesifu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Rais Magufuli katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuongeza kasi ya ukusaji wa mapato nchini, lakini imeonya kuwa mkakati wa kodi ufanyike katika mfumo ambao hauathiri mazingira ya biashara.
Imeeleza kuwa mazungumzo yanayoendelea baina ya pande hizo mbili yatasaidia kupunguza athari hizo na kwamba ni lazima Serikali ipunguze mlolongo wa kodi na ushuru ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za biashara.

Makamu wa Rais
Akizungumza baada ya kuzinduliwa kwa ripoti hiyo, Samia alisema Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa kitaasisi, kisheria na kiudhibiti kwa ajili ya kuimarisha ubia na sekta binafsi.
Aliwatoa hofu wadau wa maendeleo nchini kuwa Serikali itahakikisha rasilimali zote zinapatikana kwa ajili ya kuendeleza miradi mikubwa ya PPP zikiwamo kutoka katika mfuko wa kuimarisha ubia kati ya Serikali na sekta binafsi na Benki ya Dunia.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kanda Maalumu za Uwekezaji (EPZA), Joseph Simbakalia alisema hakuna ulazima wa PPP kwa kuwa sekta binafsi inaweza kutekeleza miradi mingi kwa asilimia 100 wakati Serikali ikibaki kama mwezeshaji.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Dk Samuel Nyantahe alisema Serikali imekuwa ikifanya kazi nzuri kwa kipindi cha miaka 15 kuboresha barabara, lakini imesahau reli ambayo ni muhimu katika usafirishaji wa mizigo.
Alikosoa msisitizo wa Serikali katika kukuza biashara na kuweka nguvu kidogo katika sekta za uzalishaji jambo ambalo linakatisha tamaa sekta ya viwanda.
Hata hivyo, alisema anaamini kuwa Serikali ya Awamu ya Tano iliyojikita kwenye viwanda, itaondoa upungufu huo.
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali inajitahidi kuongeza mapato kupitia kodi na matokeo ya awali mwaka huu yanaonyesha hali ni nzuri.
Habari zaidi na Bernard Lugongo

CHANZO: MWANANCHI

No comments: