
Dar es Salaam. CCM imesema kitendo cha Rais John Magufuli kumvua uwaziri Charles Kitwanga kutokana na kuingia bungeni akiwa amelewa, kimedhihirisha kuwa bado kuna baadhi ya watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma, lakini hakitachukua hatua kwa kuwa ameshaadhibiwa.
Wakati CCM ikisema hayo wachambuzi waliohojiwa na Mwananchi wamesema ili nafasi hiyo ipate mtu anayefaa, Rais atalazimika kuweka pembeni uteuzi unaozingatia kufahamiana au kufuata mfumo uliokuwa ukitumiwa na watangulizi wake kwani ndani ya mfumo huo hakuna anayeweza kwenda na kasi anayoitaka.
Akizungumza na gazeti hili jana, msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka alisema kitendo cha Kitwanga kuingia bungeni akiwa amelewa kimewapaa fundisho na sasa wanajua kuwa kuna baadhi wa watumishi waliopewa dhamana na chama hicho, lakini wanakiuka miiko ya maadili ya utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume na taratibu zao.
Sendeka alisema licha ya kwamba Rais Magufuli amechukua hatua juu ya hilo na kutoa adhabu, CCM itaendelea kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya wanasiasa waliopewa dhamana na chama hicho.
“Hatutasita kuchukua hatua endapo tutabaini kuna kada anayekiuka maadili ya viongozi wa umma,” alisema Sendeka.
Alisema CCM inampongeza Rais Magufuli kwa uamuzi aliochukua dhidi ya Kitwanga kwa kuwa hatua hiyo imedhihirisha kauli aliyowahi kusema kwamba hataangalia mtu usoni wala kujali kabila au dini, ikiwa mtu huyo atakiuka miiko ya uongozi.
Kuhusu CCM kumuadhibu Kitwanga, Sendeka alisema adhabu aliyopewa na Rais inatosha.
“Hukumu haitolewi mara mbili,” alisema Sendeka.
Kitwanga ambaye anatajwa kwenye sakata la utekelezaji mbovu wa mkataba wa kufunga vifaa vya kuchukua alama za vidole baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises, alivuliwa ukuu wa wizara hiyo nyeti baada ya kutinga ndani ya ukumbi wa Bunge Ijumaa asubuhi na kujibu maswali akiwa amelewa.
Hadi jana jioni, Rais Magufuli alikuwa bado hajajaza nafasi hiyo nyeti huku wananchi wakibashiri jina la mrithi wa Kitwanga kwa kuangalia jinsi marais waliopita walivyokuwa wakijaza nafasi kama wa kumpandisha naibu waziri wa wizara hiyo au nyingine, kumteua mtu anayemfahamu, kubadilisha mawaziri na kumrejesha aliyewahi kuwa waziri ama kuteua kutoka kwenye kanda anayotoka aliyetimuliwa.
Rais aliwahi kusema wakati akimuombea kura kwa wananchi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita kuwa Kitwanga ni rafiki yake na anamuelewa sana kwa kuwa alisoma naye chuo kikuu na akawataka watu kupuuzia maneno dhidi yake.
Lakini wachambuzi wanaona kuteua watu waliowazoea au kutumia utaratibu huo wa marais waliopita hautasaidia kwa kuwa walio ndani ya mfumo huo hawataweza kwenda na kasi ya Magufuli, ambaye hadi sasa amewavua madaraka watu wawili aliowateua, ambao ni Kitwanga na Anne Kilango, aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
“Wengi wamezoea mfumo wa zamani, hivyo kasi ya Magufuli hawaiwezi. Nadhani wanaoiweza kasi yake wanapatikana nje ya mfumo wa zamani, yaani ambao si miongoni mwa wabunge,” alisema Profesa Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua).
Profesa Gabagambi alisema Rais anapaswa kuteua mawaziri kutoka nje ya watu aliowazoea kwa kuwa wengi hawawezi kwenda na kasi yake. “Anachokitaka Rais ni nidhamu katika utendaji wa kazi na kuondoa mazoea sambamba na kurejesha uwajibikaji. Tukiendelea hivi tutafika mbali maana haoni shida kumuweka mtu pembeni, hasa anayeonekana kutaka kumkwamisha.”
Kauli kama hiyo ilitolewa na makamu mkuu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Dk Charles Kitima.
“Rais anataka watu wanaofuata sheria na taratibu katika uwajibikaji wao wa kazi ili kuwaondolea kero wananchi wanufaike na uongozi wa wizara husika,” alisema Dk Kitima.
Alisema kiongozi huyo mkuu wa nchi anataka waziri asiye na mazoea ya zamani na ambaye ataweza kuendana na kasi yake na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Waziri anapaswa kuhakikisha majukumu yake yanakwenda sawa na hilo ndilo jambo la msingi. Rais anataka nidhamu serikalini na hilo limeanza kufanikiwa maana uwajibikaji ni mkubwa. Yaani waziri atimize majukumu yake kwa kufuata sheria na taratibu,” alisema.
Naye naibu makamu mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence Mpangala alisisitiza sifa ya uchapakazi na uadilifu kwa mtu atakayeteuliwa.
“Maslahi binafsi hayapaswi kupewa kipaumbele. Uadilifu, uwajibikaji na usafi kiutendaji ndiyo sifa za msingi kwa sasa,” alisema mwanazuoni huyo.
Alieleza kuwa uteuzi wa Kitwanga kutenguliwa utakuwa umeshtua makada wengi ambao wanasubiri kuteuliwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi hivyo akatahadharisha: “Kila mwenye shauku hiyo anatakiwa kuichukia rushwa na ufisadi.”
Alikumbusha kuwa licha ya tuhuma za ulevi zilizomng’oa Kitwanga, tayari kulikuwa na kashfa iliyokuwa inasimamiwa na wapinzani wakimtaka ajiuzulu wadhfa wake.
Mwanasheria mkongwe na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abdallah Safari alisema suala la uteuzi ni mamlaka ya Rais na yeyote anayetajwa hawezi kulalamika pindi atakapobadilishwa.
“Tunahitaji kiongozi mchapa kazi,” alisema Profesa huyo.
Mara nyingi katika uteuzi wa mawaziri, viongozi wakuu wa nchi wamekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya manaibu kuwa mawaziri, kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka katika mkoa ambao anatokea waziri aliyeondolewa.
Mara zote saba ambazo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri alifuata utaratibu huo.
Alipomuondoa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye ni mbunge kutoka mkoa Kagera alimteua mbunge mwingine kutoka mkoa huo, Charles Mwijage kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Kwa sasa Mwijage ni Waziri wa Viwanda na Biashara.
Utaratibu huo unaweza kunufaisha wabunge sita wa majimbo yaliyopo mkoa wa Mwanza ambao ni Chalres Tizeba (Buchosa), Mansoor Hirani (Kwimba), Kiswaga Boniventura (Magu), Stanslaus Mabula (Nyamagana), William Ngeleja (Sengerema) na Richard Ndassa (Sumve).
Mbali na Kitwanga ambaye aliteuliwa kuwa waziri kutoka mkoa huo, Rais pia alimteua mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Hata hivyo, nafasi ya Ngeleja kuteuliwa inaweza kuwa ndogo kutokana na mbunge huyo kujiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini mwaka 2012 baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini ufisadi kwenye wizara hiyo na kuvuliwa uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kutokana na kashfa ya uchotwaji Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow baada ya kuonekana aliingiziwa Sh40.4.
Katika awamu ya pili ya utawala wake, Kikwete aliteua wabunge wanane, na watano kati yao walipewa wizara, akiwamo Mbarawa.
Iwapo Rais atatumia utaratibu wa kupandisha naibu waziri kuwa waziri, neema huenda ikamuangukia mbunge wa Kikwajuni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandishi Hamad Masauni au naibu mawaziri kutoka wizara nyingine.
Katiba pia inampa Rais fursa ya kuteua wabunge 10 na tayari ameshatumia nafasi sita. Aliowateua kwa kutumia haki hiyo
Dk Tulia Ackson, ambaye ni Naibu Spika, Balozi Augustine Mahiga (Mambo ya Nje), Dk Abdallah Posi (Naibu Waziri-Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu) na Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango).
Rais Kikwete pia aliwahi kuwapandisha manaibu kuwa mawaziri kamili. Hao ni Dk Emmanuel Nchimbi, Ezekiel Maige, Hamisi Kagasheki, Anthony Diallo, Ngeleja, Dk Harrison Mwakyembe, Dk Cyril Chami na Dk Mathayo David.
No comments:
Post a Comment