Tuesday, May 10, 2016

CHADEMA: BUNGE LA SASA KIBOGOYO

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji akiwaeleza jambo wahariri na waandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, alipotembelea makao makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), iliyopo Tabata Reli, Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory

By Elias Msuya na Tausi Mbowe,Mwananchi;emsuya@mwananchi.co.tz,tmbowe @mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Dk Vincent Mashinji amesema kitendo cha Serikali ya Awamu ya Tano kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge ni sawa na kuling’oa meno bunge hilo.

Tofauti na mikutano miwili iliyopita ya Novemba 2015 na Januari/ Februari 2016, Serikali hii inayoongozwa na Rais John Magufuli, iliamua kufuta matangazo ya moja kwa moja ya Bunge la Bajeti lililoanza vikao vyake Aprili 19 kwa maelezo kwamba ni gharama kubwa kwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Badala yake TBC huonyesha kipindi cha maswali na majibu pekee na hurekodi matangazo mengine na kurushwa katika kipindi cha ‘Leo katika Bunge’ saa nne usiku.

Suala hilo lilipingwa vikali na wabunge wa upinzani lakini uongozi wa Bunge ulitia chumvi kwenye kidonda baada ya kukataza vyombo vya habari kupiga picha za video, badala yake wanatakiwa kuchukua picha kutoka kwa televisheni ya Bunge.

Akizungumzia hali hiyo jana alipofanya ziara katika ofisi za gazeti hili zilizopo Tabata jijini Dar es Salaam, Dk Mashinji alisema kuwa huu ni mkakati maalum uliosukwa na CCM ili kuvibana vyama vya upinzani.

“Siri ni kwamba Bunge la sasa halina meno….Kwa taarifa tulizonazo, CCM walifanya utafiti wakagundua kwamba wapinzani wamepata nguvu kubwa kupitia bungeni; yaani Bunge limekuwa njia kubwa ya utetezi wao. Kwa hiyo, njia pekee ni kulinyamazisha. Wakasema acheni tu kipindi cha maswali na majibu kwa sababu hakina kitu. Acha punda afe lakini mzigo wa bwana ufike,” alisema Dk Mashinji.

Dk Mashinji ambaye aliteuliwa mapema mwaka huu kuchukua nafasi hiyo iliyoachwa na Dk Willibrod Slaa aliyeamua kujiondoa katikati ya uchaguzi mkuu mwaka jana alisema licha ya kuweka mipango ya kupambana katika suala hilo, bado wanajua nyuma yake kuna mpango maalumu wa CCM.

Hata hivyo, alisema katika kupambana na hali hiyo chama chake kimeamua kurusha moja kwa moja majadiliano yanayofanyika katika mabaraza ya madiwani.

“Moja ya vitu ambavyo tunavifanya ni kuwaambia mameya wetu, mikutano yao ya mabaraza ya madiwani iwe ya hadhara. Arusha wameshaanza, wanarusha kwenye Radio 5, wamefunga na spika nje japokuwa uwezo wa kulipia televisheni bado ni mdogo,” alisema.

“Tumeshauriwa pia tufungue kesi lakini sasa suala ni kwamba, ukishafungua tu kesi tunajiweka kwenye wakati mgumu. Ukitaka tu kulisema utaambiwa liko mahakamani.”

Hesabu kwa CAG

Kuhusu kutowasilisha hesabu za Chadema katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Dk Mashindji alisema bado hawajapitisha muda unaotakiwa licha ya taarifa kuonyesha kuwa hawajapeleka.

“Hilo ni suala dogo, wahasibu wetu walikuwa wanakamilisha. Bado tuko ndani ya wakati. Ndiyo maana hata wenzetu CCM wamekaa kimya tu,” alisema. “Kuna tetesi nyingi kwenye ruzuku ya Chadema. Kuna mtu aliniambia mdogo wangu siku hizi una hela sana, mimi nikamwambia hela gani? Mtu niliyekuwa nasimamia miradi ya Dola za Marekani 600 milioni ndiyo ulinganishe na Sh500 milioni?” alihoji.

Kuondoka kwa Dk Slaa

Kuhusu kuondoka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Slaa, Dk Mashinji alikiri kuwa kwa namna fulani alisababisha kuyumba kwa chama kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu licha ya mafanikio yaliyopatikana.

“Katibu Mkuu alipoondoka ilikuwa mgogoro, ilichangia kukitingisha chama. Kwa sababu kama wewe ni Katibu Mkuu wa chama, unashikilia rasilimali zote za chama, wewe ndiye mtia saini halafu unaondoka, kwa hiyo, inayumbisha,” alisema Dk Mashinji.

Alipoulizwa kama viatu vya Dk Slaa vinamtosha alitania, “Viko wapi?” Alisema mwelekeo wao kwa sasa ni kujenga chama kuanzia ngazi ya chini na kazi hiyo itafanywa na viongozi wa majimbo.

Katibu huyo alisema wameshajipanga na kwamba watarudi barabarani kuanzia Juni mwaka huu tena kwa kasi kutekeleza operesheni zake japo zinaweza kuwa na mtazamo tofauti na wa zamani.

“Lakini nawaahidi kwamba mwezi ujao tunarudi kwenye shughuli zetu za kawaida japo zinaweza zikawa na mtazamo tofauti kidogo. Kwa sababu tuna jukumu la moja kwa moja la kushughulikia mambo ambayo tumekuwa tukiyalalamikia,” alisema.

Kuhusu madai kwamba kwa sasa hawana ajenda baada ya Rais Magufuli kuteka hoja yao ya kupambana na ufisadi, Dk Mashinji alisema ajenda ya kupambana na ufisadi ni ya kudumu ila kwa sasa watakuwa wanajishughulisha zaidi na mkakati wa kupeleka maendeleo kwa wananchi badala ya kulalamika tu.

“Sasa unaweza kuambiwa ajenda kubwa ya Chadema ilikuwa ufisadi, sasa this ‘gentleman’ (Rais Magufuli) amejibu, hawana gia tena’. Sidhani kama chama cha siasa kinaendeshwa kwa matukio. Chama cha siasa kinaundwa na itikadi na falsafa. Hakipo kusubiri, chama tawala kikosee ndiyo kipate gia. Chama cha siasa kina kazi ya kueneza itikadi yake. Hapo ndipo mimi nataka kusimamia. Sipendi kuona Taifa linalolalamika wakati kuna uwezo wa kudhibiti kinachotokea kwenye mazingira,” alisema.

Alisema kutoka na mikakati hiyo, Chadema inajipanga kufanya vizuri kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa yakiwa ni maandalizi ya kushika dola.

No comments: