Advertisements

Thursday, May 12, 2016

CHADEMA: UTUMBUAJI MAJIPU WA JPM UMEKOSA DIRA

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Vincent Mashinji ameponda mtindo wa utawala wa Rais John Magufuli wa utumbuaji wa majipu akisema umekosa dira na kinachoendelea ni utashi wa kisiasa na kukurupuka.
Kazi kubwa aliyoifanya Rais Magufuli tangu aingie madarakani, katika kipindi cha miezi sita sasa ni kubana matumizi ya fedha za umma kwa kufuta safari za nje za watumishi, kuzuia mikutano kufanyika mahotelini, kuhimiza mamlaka husika kukusanya kodi, kupambana na watumishi hewa, kuwasimamisha au kutengua uteuzi wa watendaji aliodai kuwa ni wazembe na walioshindwa kwenda na kasi yake pamoja na kuwashughulikia wala rushwa na wahujumu uchumi.
Katika namna inayoonekana ni kufuata upepo wa kisiasa, Rais Magufuli huwatumbua baadhi ya watendaji kwenye mikutano ya hadhara.
Akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari wa gazeti hili hivi karibuni likiwamo anaionaje miezi sita ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Dk Mashinji alisema umekosa dira licha ya mambo mengi kufanyika.
“Kuna vitu vingi vinafanyika lakini hatujui kipi ni kipi na wapi tunaelekea. Kuna mambo mengi yanafanyika, lakini hakuna hata mtu mmoja katika nchi hii anayejua Taifa hili lina mpango gani na linaelekea wapi,” alisema Dk. Mashinji alipofanya ziara katika ofisi za gazeti hili mapema wiki hii, Tabata Relini, Dar es Salaam.
Huku akifananisha utawala wa Rais Magufuli na wa mtangulizi wake Jakaya Kikwete, Dk Mashinji alisema walau ahadi ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania” ilikuwa inaeleweka hata kama haikutekelezeka.
“Rais Kikwete alitwambia Maisha bora kwa kila Mtanzania na tulijua maisha hayo yanapatikana kwa kupambana wenyewe na tulipambana. Lakini sasa hatujui tunaelekea wapi. Hapa kazi tu! Umemfukuza huyu kazi halafu nini kitaendelea? Keshaondoka kakuacha, unaajiri mwingine? Tunahitaji mtu wa kujibu hayo maswali. Nchi yote sasa inavurugwa. Halmashauri zinavurugwa,” alisema.
Katibu mkuu huyo alisema kwa sasa kila kitu kinavurugwa jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa nchi na kwamba inaonekana wazi nchi inaelekea sehemu ambayo mbele kuna giza.
Akitoa mfano wa mfumo ulivyobadilika alisema hivi sasa wakurugenzi wa halmashauri wametangaziwa kusitisha mawakala wote wanaokusanya ushuru badala yake wakusanye wenyewe. “Hivi tujiulize halmashauri ina wafanyakazi wangapi ambao wana uwezo wa kukusanya mapato yake? Huku ni kudanganyana,” alisisitiza Dk Mashinji.
Hata hivyo, Dk Mashinji alisema hawapingi anachokifanya bali tofauti yao na Rais Magufuli ni namna ya kukabiliana na jambo. “Sisi tunaamini katika mfumo na siyo mtu. Huwezi leo kuniambia meya anaiba Sh5 bilioni halafu chama kisijue. Kwa nini chama kisimwondolee udhamini kabla?” alihoji. “Anachofanya sasa ni kudhibiti na siyo kurekebisha mfumo. Rais Magufuli hana dhamana na Mungu, asipokuwepo sioni wa kuendeleza falsafa zake. Kwa nini kusiwe na mfumo madhubuti ambao upo kisheria na kila mmoja aujue na kuufuata?” alieleza.
Aiota Katiba ya Warioba
Dk Mashinji alisema chama chake bado kinaamini mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti Jaji Joseph Warioba yanapaswa kuendelezwa.
“Ile ilikuwa Katiba ya wananchi na endapo ikitekelezwa italeta manufaa makubwa katika Taifa letu, masuala yote ya mfumo na nguvu za Rais katika masuala mbalimbali yatapatiwa ufumbuzi,” alisisitiza.
Sekretarieti ya chama
Kuhusu sekretarieti ya Chadema atakayoiunda Dk Mashinji alisema haitakuwa na wabunge. “Hatuwezi kuwa na watu wanaofanya kazi mbili mbili. Kwa nini umpe mtu kazi mbili wakati kuna wengine wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo?” alisema katibu huyo aliyeandamana na Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ni Katibu Mkuu ambaye ndiye mwenyekiti, Naiu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Wakurugenzi wa Idara zote Makao Makuu, Wajumbe watano wataalamu watakaoteuliwa na Mwenyekiti kwa kushirikiana na Katibu Mkuu, Katibu wa Sekretariet atakayeteuliwa na Katibu Mkuu pamoja na Makatibu wa Mabaraza yote ya chama Taifa.
Kwa mantiki hiyo, wabunge kadhaa ambao huingia katika Sekretarieti hiyo kwa nyadhifa zao watakuwa njiapanda. Wabunge hao ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na mbunge wa Viti Maalumu Grace Tendege.

CHANZO: MWANANCHI

3 comments:

Anonymous said...

Kwani chadema wana dira gani? Wakeshajibu hilo halafu tena ndio waje kuhoji dira ya Magufuli. Walikuwa na sera na dira ya kupambana na ufisadi Tanzania lakini imekufa hafla na ni baada ya kumkumbatia kigogo wa ufisadi kuwa chaguo lao la uraisi. Dira yao nyengine ilikuwa ni kuhakikisha Tanzania haitawaliki kwa vurugu imekufa baada ya mamlaka husika kuimarisha vyombo vyake vya ulinzi na usalama. Dira ya chadema kwa sasa ni kumpiga vita Magufuli na serikali yake isiwaletee watanzania maendeleo yao. Na ukitaka kujua dira ya Magufuli wapi anataka kuipeleka Tanzania basi hahiitaji hata kwenda shule kuelewa ni kwamba Maghufuli anapambana kujenga Tanzania yenye nidhamu kiuchumi,kiutawala na kimaadili na kwa bahati nzuri watanzania wanamuelewa wapi anataka kuipeleka nchi yao na kwa kiasi kikubwa wanamuamini na kuridhika na utendaji wake wa kazi hizo kelele na kejeli za chadema kwa Magufuli watanzania waliowengi wanazichukulia kama ni usaliti kwa nchi yao.

Anonymous said...

Well said

Anonymous said...

Nakuunga mkono mtoa maoni wa kwanza, hawa wapinzani hawa Chadema Kwisha habari Yao, sasa wamebaki kubwabwaja Nonsense tu, nyie kaeni kimya msubiri Rais wetu anavyoijenga Tanzania mpya Well done Baba yetu & keep it up!! Ukawa sijui Chadema chaliiiii! Kwisha habari yake .hivi kwani ukiwa mpinzani lazima upinge kitu!??