Advertisements

Monday, May 2, 2016

Dk Shein: Mimi si msanii kuhusu mishahara

Wakati Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, akijitetea kwa kutoongeza mshahara, Bara wafanyakazi wamelia kunyanyaswa na wawekezaji, huku walimu watoro wakinyooshewa kidole.
Akizungumza katika maadhimisho hayo ya Mei Mosi, Dk Shein (pichani) aliwaacha hoi wafanyakazi pale aliposema kuwa katika utekelezaji wa ahadi ya kuimarisha masilahi yao, hawezi kufanya usanii na hawezi kuahidi yasiyotekelezeka.
“Ni kweli mimi nilikuwa msanii nikiigiza nilipokuwa nasoma shule, miaka ya 60 na 70, nikicheza michezo ya kuigiza pamoja na kuimba, lakini kwa sasa mimi ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi siwezi kufanya mzaha na haki ya watu ninaowaongoza, hii ni haki ya wananchi”, alifahamisha.
Akikumbushia ahadi aliyotoa wakati wa kampeni alipokuwa akiomba kuchaguliwa tena kabla ya Oktoba 25, 2015, Dk Shein alisema:
“Serikali itaendelea kuimarisha masilahi ya wafanyakazi kwa kutekeleza ahadi yangu niliyoitoa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu, nilipokuwa nikinadi Ilani ya CCM ya kutoa mshahara wa kima cha chini cha Shilingi 300, 000 kwa mwezi”.
Hata hivyo katika utekelezaji wa ahadi hiyo iliyosubiriwa kwa hamu na wafanyakazi hao, Dk Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliwataka Wazanzibar kuwa na subira wakati Serikali ikiandaa kuangalia upya suala la mafao na posho za watumishi.
“Nakuombeni sana muwe na subira kwani subira huvuta heri tutayaangalia upya mafao na posho nyingine za watumishi ili ziende na wakati kwa kadri hali yetu ya uchumi inavyoruhusu,”alisema.
Pamoja na ahadi hiyo iliyosababisha sehemu ya wafanyakazi kuguna na kuinamisha vichwa wakati wa hotuba hiyo, Dk Shein alibainisha changamoto iliyopo katika kukabiliana na madeni ya wafanyakazi, pensheni za wastaafu, pamoja na walimu wanaoidai Serikali.
“Vile vile tutafanya kila tuwezalo ili tulipe viinua mgongo kwa wakati na tulipe malimbikizo ya malipo ya wafanyakazi hasa walimu, ninafahamu kwamba bado walimu wanadai haki yao ambayo bado hawajalipwa; tutawalipa walimu deni lao ambalo ni haki yao ambayo bado hawajalipwa, tutaandaa utaratibu bora zaidi wa namna ya kulimaliza deni hilo”.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar (Zatuc), Khamis Mwinyi Mohamed, akisoma risala ya watumishi wa sekta ya umma na binafsi katika kilele hicho alisema, ni vyema Rais akatekeleza ahadi zake kwa wafanyakazi kila anapozitoa, ili kuwapa moyo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Alisisitiza haja ya waajiri kuzingatia mazingira ya utoaji wa bima ya afya kwa wafanyakazi, ili kuwapa moyo na kuwahakikishia usalama wakati na baada ya utumishi wao.
Kilimanjaro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki amesema wafanyakazi hewa ni pamoja na walimu ambao hawaingii darasani kufundisha na badala yake wanafanya biashara nyingine.
Akihutubia umati wa wafanyakazi katika viwanja vya Ushirika Mjini Moshi mkoani hapa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, alisema kuwapo kwa walimu hewa shuleni kumechangia ongezeko la kushuka kwa daraja la elimu kimkoa.
“Kiwango cha ufaulu mkoani hapa ni tofauti na miaka iliyopita, kwani mkoa huu ulikuwa ukishika nafasi za mwanzo katika viwango bora, na mwaka huu umeshika nafasi ya 17 kati ya mikoa yote, hii ni kutokana na walimu kutoingia madarasani kufundisha,’’alisema Sadiki.
Sadiki alilaani unyanyasaji wa waajiriwa ambao wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi kama likizo, malimbikizo na nyongeza ya mshahara.
“Kila mfanyakazi lazima apate stahiki zake iwe ni wa serikalini au ni wa kutoka shirika binafsi, lazima apewe haki zake zinazohitajika na mwajiri akienda kinyume basi sheria itachukuliwa dhidi yake,’’ alisema Sadiki.
Mbeya waangua kilio
Wakati hayo yakijiri Kilimanjaro, mkoani Mbeya wafanyakazi zaidi ya 20 wa kampuni ya kutengeneza marumaru za miamba, maarufu kwa jina la Marmo and Granito Mines (T) Limited, waliamua kujiangusha chini na kulia kwa sauti wakidai Serikali iwaokoe na manyanyaso.
Tukio hilo lilitokea wakati wafanyakazi wakiandamana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla aliyekuwa akiyapokea maandamano hayo ya Mei Mosi Uwanja wa Sokoine.
Wafanyakazi hao walisema mwajiri wao anawanyanyasa kwa matusi, kuwapiga, kuwalipa mshahara mdogo na kwamba Serikali haijawasaidia tangu walipowasilisha kero hizo miaka kadhaa iliyopita.
Tukio hilo lilisababisha vicheko kwa watu mbalimbali huku, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi mkoa wa Mbeya (Tucta), Pilipili Zege Kokoko akisema kilio hicho ni cha kuashiria kero kubwa na ya siku nyingi.
Kokoko alimwomba Mkuu wa mkoa kulifuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba wawekezaji wengi wamekuwa kero kwa Watanzania kutokana na kuwalipa mishahara midogo na kuwanyanyasa.
Naye Kaimu Katibu wa Tucta mkoani hapa Juma Bwikitia akisoma risala alisema kampuni za ujenzi, migodi, viwanda na mashambani ndizo zinazoongoza kwa kuwanyanyasa wafanyakazi pamoja na kushindwa kutoa mikataba kwa wafanyakazi.
Bwikitia alisema kampuni za aina hiyo pia ndizo zinazoongoza kwa kuajiri wafanyakazi wa kigeni na wasiofuata taratibu ambao wanapata mishahara mikubwa ikilinganishwa na ile ya wanaopata Watanzania.
Akizungumzuia suala la wafanyakazi kwa ujumla, Mkuu wa mkoa alisema tatizo la wafanyakazi waliolia uwanjani hapo, atalishughulikia wiki hii atakapokwenda kiwandani ili kuzungumza na wafanyakazi wote wakiwa na waajiri wao.
Makalla alisema atahakikisha anazishughulikia kero za wafanyakazi kupitia kwa wakuu wa wilaya na viongozi wengine.

No comments: