ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 18, 2016

HASSAN KESSY NI KAMA MFALME YANGA

Beki wa zamani wa Simba, Hassan Kessy (kulia) alipokuwa katika timu yake hiyo ya zamani.

AMINI usiamini. Aliyekuwa beki wa Simba, Hassan Kessy aliyetua Yanga kwa sasa ni kama Mfalme Jangwani, kiasi hata mwenyewe haamini kile alichokutana nacho.

Achana na kuanza kutengenezwa kwa jezi zenye jina la beki huyo wa kulia, Kessy amesema hata mapokezi aliyoypata kutoka kwa wachezaji wenzake yamemfanya ajisikie faraja kubwa.

Kessy alisema kuwa kwa sasa ametuliza akili akijipanga kuhakikisha anapata namba pale kwa msimu ujao, lakini alisema japo hajatua kikosini, wachezaji wenzake wamekuwa wakimpa sapoti kubwa na kujiona kama yupo sehemu salama.

Kessy alisema hata kabla ya kutua Simba, Yanga ilimhitaji ila aliona ni vizuri aende Simba kwani tayari walikuwa wamefanya makubaliano na mbaya zaidi mama yake kipenzi, Rukia Kessy ni shabiki mkubwa wa Wekundu wa Msimbazi.

“Nimejifunza mengi ndani ya Simba, hasa juu ya kuishi na klabu kubwa, ila kwa ukweli maisha ya Msimbazi yaliniumiza tofauti na nilivyotarajia niliposaini mkataba, ila yote namuachia Mungu na sasa naangalia maisha mapya ya Yanga kwa msimu ujao.

“Naamini sijakosea kutua Yanga maana ndiyo timu pekee iliyoonyesha nia. Sina hofu na ninaowakuta kwa sababu tunafahamiana na wamekuwa wakinipigia simu kuonyesha furaha yao kutua katika kikosi chao,” alisema Kessy.

Beki huyo alisema kwa kipindi hiki atakitumia kupumzika na kufanya mazoezi kujiweka vema ili atakaporejea msimu ujao akiwa na Yanga awe zaidi na alivyo sasa.
MWANASPOTI

No comments: