Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa tozo kwa vyombo vya usafiri vitakavyopita katika daraja la Nyerere kuanzia Jumamosi tarehe 14 ,mwezi huu.
Akizungumzia na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema kuwa kuanzia siku hiyo , vyombo vyote vya usafiri vitatakiwa kulipia ushuru wa kupita katika daraja la Nyerere.
“Tumeanza kutoza tozo hii mara baada ya kufunguliwa kwa daraja hili na kuanza kutumika kwa kupita bila kulipa kwa vyombo vya usafiri tangu Aprili 19 mwaka huu na sasa tunaanza rasmi kutoza tozo kwa ajili ya kukusanya gharama za usimamizi, utunzaji na uendeshaji wa daraja hili.” alisema Mhandisi Nyamhanga.
Mhandisi Nyamhanga amefafanua kwamba watembea kwa miguu watapita bure katika daraja hilo huku wenye baiskeli wakilipia Sh. 300, pikipiki Sh. 600, waendesha maguta ,bajaji na magari ya kawaida(Saloon Cars) watatakiwa kulipia Sh.1500.
Mabasi yanayobeba abiria 15 yatalipia Sh. 3,000, yale ya abiria zaidi ya 15 Sh. 5,000 na yale yanayobeba abiria zaidi ya 29 yatalipia Sh. 7,000.
Aidha magari yenye tani zaidi ya mbili mpaka saba yatalipia Sh. 7,000, tani 7 hadi 15 watalipa Sh.10,000, tani 15 mpaka 20 watalipa Sh.15,000 na yale yenye tani 20 mpaka 30 yatalipia Sh. 20,000.
Mhandisi Nyamhanga ameongeza kuwa magari yenye namba za Jeshi la Wananchi(JWTZ), Jeshi la Polisi(PT), Jeshi la Magereza(MT), gari za wagonjwa, magari ya zimamoto na magari yenye vibali maalum yataruhusiwa kupita bure.
No comments:
Post a Comment