Zanzibar. Wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad akipata mapokezi makubwa baada ya kuwasili Pemba kuanza ziara ya kikazi ya siku nne, vurugu zimesababisha viongozi wa chama hicho na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuungana kuzipatia ufumbuzi.
Maalim Seif aliwasili visiwani humo jana saa 4 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume na kulakiwa na mamia ya wafuasi wa chama hicho.
Umati wa wananchi wakiongozwa na viongozi mbalimbali wa CUF akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui walijipanga kuanzia uwanjani hapo kuelekea Mji wa Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Hali ilikuwa hivyo katika barabara zote za kisiwani humo mpaka katika Mji wa Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba ambako Maalim Seif alifikia, tofauti na alipokuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ alikuwa akifikia katika nyumba Serikali iliyopo Mkanjuni, Wilaya ya Chake Chake.
Katika ziara hiyo ya kichama, kiongozi huyo anatarajiwa kuonana na viongozi wa wilaya nne za Pemba.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kutembelea rasmi kisiwani humo tangu Machi 20, ulipofanyika uchaguzi wa marudio wa Zanzibar.
Juzi, Serikali na Jeshi la Polisi waliwaangukia viongozi wa CUF kwenda kuzima hali ya taharuki iliyoibuka katika vijiji vya Kiuyu na Maziwang’ombe katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kutokea vurugu zilizosababisha polisi kupiga mabomu mengi ya machozi.
Viongozi wa polisi mkoani humo wakiongozwa na Kamanda wao, Hassan Nassir Ali, ofisa upelelezi wa mkoa pamoja Serikali ya mkoa na Wilaya ya Micheweni walilazimika kuwaomba viongozi wa ngazi za juu wa CUF walioongozwa na Waziri mstaafu wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk kwenda kuwatuliza wananchi waliocharuka baada ya kupigwa mabomu hayo.
Kamanda Hassan alisema taharuki hiyo ilizuka baada ya wananchi wa kijiji hicho kuishambulia kwa mawe, nyumba ya Sheha wao, Asha Yussuf Juma wakimtuhumu kutaka kuuza ardhi yao kwa mzungu.
Hata hivyo walimaliza tofauti zao na wananchi baada ya viongozi na wazee kuingilia kati suala hilo na amani kurejea.
No comments:
Post a Comment