Advertisements

Friday, May 27, 2016

MAGUFULI ASEMA MAZITO KWENYE MKUTANO WA WAKANDARASI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Wakandarasi, Wahandisi na wadau mbalimbali wa sekta ya Ujenzi kabla ya kufungua rasmi Mkutano  wa Siku mbili wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini CRB uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam

Rais John Magufuli jana alituma ujumbe mzito katika mapambano dhidi ya rushwa nchini, akisema mapambano hayo ndiyo mwelekeo wake na hatabadilika hata kama itakuwa ni kutoa sadaka mwili wake.
Alitoa ujumbe huyo alipofungua mkutano wa wakandarasi jijini Dar es Salaam, akiendelea na ‘kampeni yake’ ya kuhimiza uzalendo na kupambana na ufisadi.
“Na bahati nzuri nashukuru, Watanzania wananiombea na Mungu ananisimia kwa sababu nafahamu kazi hii zikupewa na mtu, nilipewa na Mungu,” alisema Rais huku akipigiwa makofi.
“Na watu wanaoteseka ni watu wa Mungu, hasa watu maskini. Ni lazima nitimize wajibu wangu, hata kama ni kwa kutoa sadaka yangu, sadaka ya mwili wangu.”
Magufuli hakuwa anapewa nafasi ya kupitishwa na CCM kuwania urais, lakini upepo ulibadilika ghafla baada ya jina la Edward Lowassa kukatwa na kubakia makada watano. Magufuli aliongoza kwenye kura za Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu na kushinda urais katika kinyang’anyiro kilichokuwa na ushindani mkali.
Tangu aingie madarakani amekuwa akieleza jinsi nchi ilivyofikishwa pabaya kutokana na wizi, ufisadi, uzembe na matumizi mabaya ya fedha za umma na amepambana na wafanyabiashara wakubwa katika masuala ya ulipaji kodi.
Akiwa mapumzikoni jimboni kwake Chato, Rais alinukuliwa akisema angejua urais ulivyo asingejitokeza, lakini akaahidi kuendelea na mapambano.
Jana Magufulim ambaye aliambatana na mkurugenzi wa Takukuru, Valentino Mlowola, aliendelea kusisitiza msimamo wake wakati akizungumzia suala la makandarasi wazalendo kuweka viwango vya juu vya fedha wakati wanapoomba zabuni serikalini.
“Na ndio maana nawaomba sana wakandarasi, sana. Tubadilike kwa ajili ya nchi yetu,” alisema.
“Unapoona watu wanashangaashangaa sana (ni) kwa sababu hawakuzoea haya. Na walifikiri nitakuwa part of them (sehemu yao), never (haitatokea), not me (si mimi).
“Ni mara 10 nisiwe rais, nikachunge hata ndege, nikakae kijijini kuliko niwe Rais halafu nivumilie uozo huu unaofanyika. I’m saying never (nasema haitatokea).”
Rais alisema ataendelea na vita aliyoianzisha na atawashughulikia kikamilifu wanaofanya uovu huo.
“Kama ni kutumbua kila siku nitatumbua tu. Watu lazima wabadilike. That is my direction and I will never change it (huu ndiyo mwelekeo wangu na sitaubadili).”
Akieleza sababu ya kuambatana na Mlowola, Rais Magufuli alisema anataka ashirikiane naye katika kupambana na rushwa katika sekta hiyo ya wakandarasi.
“Mlowola nina uhakika hawajakualika, lakini nimekuchukua ili kusudi tushiriki mimi na wewe kwenye kikao na sifahamu kwa nini mwenyekiti hakukualika,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli, ambaye hakutaka kusoma hotuba aliyoandaliwa, alisema baadhi ya makandarasi wamekuwa wakikadiria gharama kubwa za miradi ili watoe rushwa kwa watendaji wa Serikali.
“Inawezekana tatizo liko ndani ya Serikali, kwamba mnakadiria nyingi kwa sababu nyingine zipo za watendaji wangu. Na hilo ni kweli au uongo?” alihoji.
“Kwamba unajua kabisa huu mradi unaweza kuumaliza kwa Sh200 milioni, lakini lazima upeleke asilimia fulani kwa mtu. Inawezekana hata wakati unaendelea na kazi lazima uandae mfuko fulani mahali fulani na ndiyo maana hata zabuni ziko juu.”
“Kama hiyo ndiyo sababu, tuna chombo chetu cha Takukuru. Kwa nini hamkitumii? Kwa nini mnakubaliana na wale wanaowaomba rushwa? Kwa nini kila mahali mnapoomba zabuni unaweka asilimia ya kulipa rushwa?”
Alisema kwa kuwa wanaoomba rushwa ni wachache kuliko makandarasi, waungane kuwashtaki.
“Tukichukua watendaji hata 100 au 50 wakifungwa kwa kupokea rushwa, hizi gharama za miradi zitashuka,” alisema.
“Mnieleze ukweli, nataka tujipange vizuri zaidi. Inawezekana hatujaenda mwendokasi unaotakiwa.
“Siku hizi kila unapoenda ni hewa tu. Unakwenda unakuta wafanyakazi 1,000 ni hewa. Jana nilikuwa nashuhudia wanafunzi wa chuo kikuu ni hewa. Nina uhakika hata makandarasi hewa wapo.”
“Sisi wazee ndiyo tumeliharibu hili taifa. Hakuna mtu ambaye hajui kwamba rushwa ilikuwa imechakaa kila mahali. Haiwezi kuingilia akilini kwamba Tanzania ilikuwa na wafanyakazi hewa 10,295.
“Unalipa mishahara hewa kwa wafanyakazi hao na sasa wameongezeka, wakati kuna vijana wamemaliza chuo kikuu hawana ajira. Inaumiza sana.”
Rais Magufuli pia aligusia suala la kusimamishwa vigogo wa Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU), akisema ndiyo uozo uliokuwapo nchini.
“Huwezi kuamini nchi hii unatenga bilioni 87 kwenda kulipia mikopo ya wanafunzi, halafu unaowalipia kwa sababu unaamini ni watoto wa maskini ili waje walikomboe taifa, kumbe wengine ni division four (daraja la nne) na wengine hata hawaingii darasani,” alisema.
“Wanafunzi zaidi ya 480 ni hewa lakini unawalipia mkopo na unashangaa zaidi anayesimamia hicho kitengo ni Profesa.”
Alisema kuwa ilifika wakati meli 65 zilifika bandari ya Dar es Salaam lakini hazikuandikishwa popote na zikaondoka bila kulipa kodi, zikiwa zimepakia makontena ya kutosha.
Kuhusu ombi la Bodi ya Makandarasi (CRB) kupewa upendeleo katika zabuni za ujenzi, Rais Magufuli aliwataka kuwa wazalendo na kuacha kukadiria gharama kubwa kuliko uwezo wa Serikali.
“Nitatolea mfano idara ya mahakama. Imetangaza kujenga mahakama za mwanzo na za wilaya. Kwenye bajeti wana bilioni 24. Kwenye makadirio ya wahandisi kila jengo lisizidi Sh200 milioni. Wakandarasi walipokadiria, jengo moja ni Sh1.4 bilioni.
“Sasa nakuuliza mwenyekiti, hata kama una upendeleo, utapasuka moyo. Kiasi kidogo cha aliyejitahjidi sana ilikuwa milioni 620. Hata kama ungekuwa na upendeleo namna gani kwa wazalendo, utashindwa,” alisema Rais.
Kuhusu madeni ya makandarasi, Rais Magufuli alisema Serikali imeshalipa Sh640 bilioni kwa makandarasi waliokuwa wakidai na Sh460 bilioni zitatolewa kwenye Mfuko wa Barabara ili walipwe wengine wanaodai.
Alisema idadi ya makandarasi 8,631 waliosajiliwa ni ndogo kwa kuwa mmoja anahudumia Watanzania 6,000 tofauti na Japan ambako mkandarasi mmoja anahudumia watu 50.
Aliwataka kushirikiana na kujipanga kushiriki kwenye miradi mikubwa ya ujenzi wa viwanda inayokuja.
“Tumezungumza kuhusu kujenga viwanda. Serikali ya Ujerumani inataka kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea kule Kilwa, makandarasi mmejipangaje? Kitaleta ajira za watu zaidi ya 6,000,” alisema.
Yapo makampuni mengi sasa yanataka kujenga viwanda vya sukari, makandarasi Watanzania mmejipangaje?” alihoji Rais Magufuli.
Akizungumza katika mkutano huo, Mlowola alisema sekta ya ujenzi ni eneo hatarishi kwa rushwa, hivyo Takukuru inalichunguza kwa karibu.
“Sisi Takukuru, sekta yenu ya ujenzi tunaiita ni corruption high risk sector kwa sababu ya wingi wa fedha za Serikali zinazotumika katika sekta hii. Kwa hiyo uwezekenano wa rushwa ni mkubwa,” alisema.
“Rais kunileta hapa ni ujumbe tosha kwenu, na sisi bila kusita tutatekeleza kwa vitendo. Kwa hiyo mshirikiane na sisi. Viongozi wa Serikali wenye tabia ya kutaka miradi yenu kabla ya kuipitisha, mtujulishe tutachukua hatua.”
Naye mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitoa mfano wa ufisadi alipokuwa Mkuu wa wilaya ya Kikondoni akisema fedha zililiwa kwenye ujenzi wa barabara.
“Wakati niko Kinondoni niliunda kamati ya kuchunguza barabara tu. Walibaini zaidi ya Sh2.2 bilioni zilitumika kujenga barabara ambazo hata mvua isingenyesha zingeharibika.
“Barabara hizo zimekuwa sugu zimesababisha kutokuwa na maendeleo. Namshukuru wa Mwenyekiti wa Road Fund kwa kuzuia fedha na kuwataka kujenga barabara kwa fedha zao na kurudisha zile Sh2.2 bilioni kwa upande wa Serikali,” alisema Makonda.
Awali mwenyekiti wa CRB, Mhandisi Consolata Ngimbwa alimwomba Rais Magufuli upendeleo wa makandarasi wa Tanzania katika zabuni za ujenzi.
“Ombi letu kubwa, tunaomba upendeleo kwa makandarasa wa Kitanzania. Sisi makandarasi wa Tanzania hapa ndiyo nyumbani, tutakachopata tutawekeza hapa. Hata kama makandarasi wa kiume kaka zangu wakioa wake wawili, watawekeza hapa, hawatakwenda kwingine,” alisema Ngimbwa.

Chanzo:Mwananchi

No comments: