ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 14, 2016

MAGUFULI ATANGAZA MALI ZAKE

john-magufuli

Rais John Magufuli.

RAIS John Magufuli amewasilisha orodha ya utajiri wake kwa Sekretarieti ya Madili ya Viongozi wa Umma, kama Sheria inavyomtaka.

Magufuli aliyeingia Ikulu Novemba 5, mwaka jana, alikuwa Mbunge ama waziri kwa miaka 20 mfululizo, akitumika kama Naibu Waziri wa Ujenzi na baadaye Waziri kamili kwenye Wizara mbalimbali.
Kamishna wa Tume ya Maadili, Jaji mstaafu Salome Kaganda alilieleza Nipashe katika mahojiano maalum hivi karibuni kuwa Rais Magufuli alishawasilisha kwenye tume hiyo orodha ya mali alizonazo.

Jaji Kaganda alisema Rais Magufuli aliwasilisha fomu inayoonyesha mali alizozipata kwa muda wote alipotumikia nyadhifa mbalimbali serikalini, kabla ya kuingia Ikulu.

Nipashe lilizungumza na Jaji Kaganda kujua kama Rais Magufuli alishatoa tamko kama Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 na kanuni zake zinazoeleza, lakini pia kufahamu idadi ya mali anazomiliki Rais huyo na thamani yake.
Kaganda alisema ni kweli Rais Magufuli aliorodhesha mali zake zote katika tume lakini alikataa katakata kumtajia mwandishi mali zlizomo kwenye tamko hilo.

Kaganda alisema Sheria inazuia kumwonyesha mtu mwingine mali za mtumishi wa umma hadi kuwe na sababu ya maana ya anayehitaji, na pia kuwe na ulazima wa kufanya hivyo.

“Mwananchi anaweza kupata taarifa za mali za viongozi kwa kufuata utaratibu uliopo, lakini baada ya kupata taarifa hizo, haruhusiwi kuzitangaza au kuzichapisha kwenye vyombo vya habari,” alisema Jaji Kaganda.
Rais Magufuli amekuwa tofauti na marais waliopita baada ya kuonyesha msisitizo kwa viongozi wa umma kujaza fomu hizo na kuzirudisha kwa wakati.

Katika kuonyesha msisitizo katika jambo hilo, Rais Magufuli kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Februari 26, mwaka huu aliwatangaza mawaziri ambao hawakujaza fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni, na kuwapa saa nane hadi saa 12:00 jioni wawe wamejaza na kurudisha fomu hizo.

Viongozi hao walitajwa kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira na Muungano, January Makamba, ambao wote hawakuwa wamerudisha fomu za rasilimali na madeni na fomu za ahadi ya uadilifu, kwa wakati huo.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Augustine Mahiga hakuwa amerudisha fomu ya Ahadi ya Uadilifu. Mwingine alikuwa ni Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ambaye hakuwa amerudisha fomu ya tamko la rasilimali na madeni, na Naibu Waziri ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina ambaye hakuwa amerudisha fomu zote mbili.

SHERIA INASEMAJE?
Kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 kifunga 9(1), “Kila kiongozi wa umma atatakiwa katika kipindi cha miezi mitatu au katika kipindi cha siku thelathini baada ya kupewa wadhifa, mwisho wa mwaka au mwisho wa kutumikia wadhifa wake:
kumpelekea kamishna tamko la maandishi katika hati rasmi linaloorodhesha mali au rasilimali zake.” Aidha, kifungu namba 9(6) kinaeleza kuwa “Wakati wa kutoa tamko la rasilimali zake kwa mujibu wa fungu hili, kiongozi wa umma atatakiwa:
(a)kutaja thamani ya mali aliyotamka na chanzo au namna alivyopata mali hiyo. Kifungu namba 11 (2) cha sheria hiyo, kinaeleza kuwa rasilimali zinazotakiwa kutajwa ni pamoja na:

Nyumba, mali ya starehe na mashamba yanayotumiwa au yanayotarajiwa kutumiwa na viongozi wa umma au familia zao. Rasilimali nyingine ni kwa mujibu wa kifungu 2(b) ni kazi za sanaa, mambo ya kale na vitu alivyonunua kidogokidogo, (c) magari na aina nyingine binafsi za usafiri kwa matumizi binafsi, (d) fedha taslimu na amana zilizowekwa benki au taasisi nyingine za fedha, (e) hawala za hazina na uwekezaji mwingine katika dhamana zenye thamani maalumu, zinazotolewa au kudhaminiwa na serikali au wakala wa serikali.
Mwezi uliopita Jaji Kaganda aliiambia Nipashe kuwa naye Rais mstaafu Jakaya Kikwete alitangaza utajiri wake kwa sekretarieti hiyo ya maadili punde baada ya kung’atuka, lakini sekretarieti hiyo ilikataa kutaja mali hizo.

MAGUFULI AKASIRIKA KUDANGANYWA MASHINE JNA MBOVU
RAIS John Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza na kubaini ‘madudu’ katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Jiulius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Alibaini madudu hayo jana alipofanya ziara hiyo ya ghafla katika uwanja huo, akiwa ametua akitokea jijini Kampala, Uganda alikokwenda kushuhudia kuapishwa kwa Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni.

Rais Magufuli alibaini kuwa mashine za ukaguzi za sehemu ya kuwasili abiria na mizigo hazifanyi kazi kwa muda mrefu na ofisa mmoja wa uwanja huo alijaribu kumdanganya kuwa ni nzima. Maofisa wa uwanja huo waliokuwa wakitoa taarifa kwa kutofautiana katika maelezo yao ndio waliomkera Rais Magufuli na kuanza kuwahoji maswali ambayo walishindwa kujibu.
Ofisa mmoja alimweleza Rais Magufuli kuwa mashine hizo zinafanya kazi na mwingine alisema kuwa hazifanyi kazi kwa muda mrefu.

Kutofautiana kwa maelezo hayo kulimfanya Rais Magufuli kuwa mkali na kuanza kumfokea ofisa aliyemdanganywa kwamba mashine hizo zinafanya kazi.
“Unajua mimi sipendi kudanganywa, ni vizuri uzungumze ukweli tu, kwanini nimeanzia hapa huwezi kujiuliza?” Alihoji Rais Magufuli.
“Sasa nakwambia sipendi kudanganywa, ukinidanganya nitachukia sasa hivi, wewe umenidanganya kwamba hiyo hiyo ndiyo mbovu na hii ni nzima nikawaambia muiwashe hiyo nzima, amekuja huyu mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema hii ni mbovu kwa miezi miwili.
“Kwa hali hii mizigo inayopitia hapa huwa hamuikagui kwa namna yeyote ile, kwa hiyo mimi nikiamua kuja na dawa za kulevya, nikaja na dhahabu zangu na almasi zangu na pembe za ndovu napita tu?” aliendelea kuwabana maofisa hao ambao walikosa cha kujitetea.
Rais Magufuli aliagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja dhidi ya dosari hizo alizoziona.

(CHANZO: NIPASHE)

No comments: