Alisema kuna kikundi cha wafanyabiashara wachache sana kila kitu wanataka wafanye wao bila hata kuwahurumia Watanzania na wanataka kuiendesha nchi wanavyotaka ikiwa ni pamoja na kuingiza bidhaa wakati wowote wanavyotaka na kuwaumiza Watanzania, hilo halitakubalika kamwe.
“Hapa kwangu ni mkong’oto tu. Kwa wale wafanyabiashara wenye kuitakia mabaya nchi hilo halitavumiliwa… awe CCM, CHADEMA au CUF atashughulikiwa kikamilifu,” alisema Rais Magufuli jana mjini hapa kabla ya kuzindua rasmi jengo la PPF la ghorofa 11 na jengo la Mfuko wa Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) lenye urefu wa ghorofa 13, mbili za chini yote yakiwa na gharama ya zaidi ya Sh bilioni 60.
“Hapa ni Tanzania kwanza na kuwajali wanyonge na mimi ni Rais wa Watanzania na wala sibagui mtu.” Rais Magufuli alitumia nafasi hiyo kuwaambia wakazi wa Arusha na vitongoji vyake kuwa uchaguzi umeshakwisha na kinachotakiwa kwa sasa ni maendeleo kwa wote bila ya kujali chama, dini wala kabila.
Akizungumzia mifuko ya jamii, ameitaka kubadilika katika suala la kuwekeza na kujikita zaidi katika kuwekeza katika viwanda ili ajira ipatikane kwa vijana wengi wasio na ajira sasa nchini. Alisema serikali yake inahitaji nchi ya viwanda ili vijana wengi waliopo vijiweni wapate ajira hivyo mifuko hiyo na mingine inapaswa kujikita zaidi katika kuwekeza katika viwanda ili uchumi wa nchi ukue.
Alisema bodi za PPF na NSSF na Menejimenti zake zinapaswa kubadilika na kubuni mbinu mpya za kuisogeza nchi mbele kwa kuwekeza katika viwanda na kuacha kuwekeza katika majengo makubwa makubwa na ya kifahari yasiyokuwa na tija kwa walalahoi.
Alisema fedha zilizotumika katika majengo yote mawili ya thamani ya zaidi ya Sh bilioni 60 zingewekezwa katika viwanda, vijana wengi wangepata ajira na kuwataka kuacha kuwekeza tena katika majengo hayo.
“Ninaomba mkiniita tena hapo baadaye nije kufungua kiwanda na sio majengo haya makubwa yasiyokuwa na tija,” alisema Rais na kuongeza kuwa mifuko hiyo imefanya vizuri sana katika kuwekeza katika majengo kwa kupendezesha miji, lakini hiyo haimsaidii Mtanzania wa hali ya chini kwa sasa hivyo jitihada za ziada zinapaswa kupelekwa katika viwanda ili Watanzania wa kawaida wafaidike na mifuko yao.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment