Dar Es Salaaam. Mchungaji wa Kanisa la Hopran Mission lililopo Tabata Kinyerezi, Jimmy Kapenye (42) amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh2m baada ya kupatikana na hatia ya kutapeli Sh13.7m, mali ya askofu wa kanisa hilo.
Kapenye amekuhumiwa kifungo hicho leo katika mahakama ya wilaya ya Ilala ambapo mbali na kifungo hicho, mchungaji huyo ametakiwa kulipa fidia ya Sh13.7m alizotapeli.
Mchungaji huyo anadaiwa kupewa mahindi na alizeti yenye thamani ya Sh13.7m na askofu wa kanisa hilo, Charles Nicholas kwa ajili ya kuuza na fedha itakayopatikana itumike kulipa mkopo wa trekta ambalo waumini walikopeshwa na Suma JKT. Hakufanya hivyo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu wa Wilaya ya Ilala, Maua Hamduni amesema mahakama yake imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka waliotoa dhidi ya mshtakiwa huyo.
“Kutokana na ushahidi ulitolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka, mahakama inakuhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh2m na kulipa fidia ya Sh 13.7milioni ili liwe fundisho kwa watu wote wenye tabia kama hizi ambao ni viongozi wa dini,” alisema Hakimu Hamduni.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwanini asipewe adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 10 jela na mshtakiwa huyo alijitetea kuwa apunguziwe adhabu kwa kuwa ana maradhi ya tezi dume na ana familia inayomtegemea.
No comments:
Post a Comment