Mtoto wa aliyekuwa mwanasiasa machachari na Mbunge wa Tarime, Chacha
Wangwe, amebadili msimamo mahakamani katika kesi ya kuchapisha taarifa
za uongo kupitia mtandao wa kijamii, kuwa Zanzibar inakandamizwa na
Tanzania Bara na kwamba ni koloni lake.
Mtoto huyo, Bob Chacha
Wangwe (24), ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
alibadili msimamo jana aliposomewa shtaka hilo kwa mara ya pili, katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wangwe alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Mei 11, na alisomewa shtaka linalomkabili na alikiri kutenda kosa hilo.
Mshtakiwa
anapokiri kosa, kwa kawaida Mahakama inaweza kumtia hatiani na kumpa
adhabu kwa mujibu wa sheria, kulingana na kosa siku hiyo hiyo au siku
nyingine yoyote.
Baada ya kusomewa shtaka na kukiri, Hakimu
Mkazi Mkuu, Waria lwande Lema, aliamuru mshtakiwa huyo apelekwe rumande
hadi jana, Mei 17, kwa kuwa hakimu aliyepangwa kusikiliza kesi hiyo
hakuwapo.
Hata hivyo, jana mshtakiwa huyo alipopandishwa
kizimbani na kusomewa shtaka hilo, ili kusomewa maelezo ya awali kabla
ya Mahakama kumtia hatiani na kumhukumu, tofauti na siku ya kwanza,
alikana kutenda kosa hilo.
Kutoka na mshtakiwa huyo kukana kosa,
Wakili wa Serikali, Salim Msemo, aliieleza Mahakama kuwa upelelezi bado
haujakamilika, hivyo aliiomba ipange tarehe nyingine ya kutajwa kwa
kesi hiyo.
Wakili wa mshtakiwa huyo Peter Kibatala aliiomba
Mahakama impe dhamana kwa kuwa shtaka linalomkabili linadhaminika,
maombi ambayo yalikubaliwa na aliachiwa kwa dhamana na kesi iliahirishwa
hadi Juni 15.
Wangwe ambaye baba yake kwa sasa ni marehemu,
anadaiwa Machi 15, jijini Dar es Salaam, alisambaza taarifa za uongo
kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.
No comments:
Post a Comment