Serikali imeanza mchakato wa kutekeleza mpango wa kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii katika ofisi za umma ili kuongeza ufanisi.
Mpango huo umelenga kuzuia mitandao ya kijamii ikiwamo Facebook, Twitter, Whatsapp na Instagram.
Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala wa Serikali Mtandao (Ega), Suzan Mshakangoto alisema mpango huo umelenga kuwadhibiti watumishi wa umma wanaotumia mitandao hiyo kuanzia saa 1.30 asubuhi hadi saa 9.30 alasiri.
Alisema sehemu kubwa ya wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa taasisi za umma wameshapewa mafunzo mbalimbali kufanikisha mpango huo.
Hatua hiyo imekuja baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kuuagiza wakala huyo miezi mitano iliyopita kutafuta njia madhubuti ya kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii ofisini ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Mtumishi akishaingia ofisini hataweza kutumia mitandao ya kijamii na huduma za barua pepe nje ya mfumo wa Serikali kama Yahoo na Gmail. Tunawataka watumie mfumo wa barua pepe za Serikali ili wafanye mawasiliano salama,” alisema Mshakangoto.
Utekelezaji wa mpango huo huenda ukachukua muda kidogo kuanza kwani Mshakangoto alisema taasisi zote za umma zaidi ya 500 zinatakiwa kuunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa lakini huenda ukaanza na taasisi 72 zilizounganishwa zikiwamo wizara zote, wakala wa Serikali na idara kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Ega ilianzishwa miaka minne iliyopita kwa ajili ya kujenga mfumo wa mtandao wa Serikali, kuimarisha uratibu, usimamizi na uzingatiaji wa viwango vya Serikali Mtandao katika utoaji wa huduma kwa umma. Pia, kuimarisha mifumo shirikishi ya Tehama na kuboresha uwezo wa taasisi za umma katika kutekeleza Serikali mtandao.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ega, Dk Jabiri Bakari alisema sasa wamejikita kuhakikisha mifumo yote ya taasisi za umma inaingiliana kama ilivyobainishwa kwenye miongozo ya Serikali Mtandao ili kurahisisha mawasiliano na kuongeza uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment