ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 13, 2016

SAKATA LA SUKARI: MKURUGENZI MTENDAJI WA CHAMA CHA KUTETEA WALAJI TANZANIA (TCSA) ATOA TAHADHARI

Wakati Serikali ikiendelea kuwaadhibu wafanyabiashara wakubwa kwa madai ya kuficha sukari katika maghala, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kutetea Walaji Tanzania (TCSA), Benard Kihiyo amesema hatua za kuwasaka ni nzuri lakini itaharibu usambazaji na upatikanaji wa bidhaa hiyo.

Kauli ya Kihiyo imekuja wakati msako dhidi ya wanaoficha sukari ukiwa umepambamoto. Jana, mfanyabiashara wa Arusha, Romanus Macha alisalimisha tani 33 za bidhaa hiyo serikalini.

Akizungumza baada ya kutembelewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Arusha, Macha alisema ameamua kusalimisha sukari hiyo ikiwa ni kufuata agizo la Serikali. Alisema alitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa na wa wilaya kuwa ana sukari.
“Mfuko wa kilo 50 nilinunua kwa Sh90,000, nilitegemea kuuza Sh92,000. Kwa kuwa nimeshaisalimisha nasubiri bei elekezi ya Serikali,” alisema Macha.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Daniel Machunda alisema maofisa wake hawakukuta dosari kwenye sukari hiyo lakini wanasubiri ripoti ya polisi kabla ya kuruhusu iuzwe.

“Pia tunataka kujua kama sukari hii ina ubora kwa matumizi ya binadamu,” alisema Machunda.

Katika msako huo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na polisi jana iliwakamata wafanyabiashara tisa waliokuwa wakiuza sukari kinyume na bei elekezi ya Sh1,800 kwa kilo.

Tani 27 zakamatwa
Jijini Dar es Salaam, mifuko 1,092 sawa na tani 27 za sukari ilikamatwa jana maeneo ya Manzese baada ya msako ulioendeshwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni.

Msako huo ulioongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Salum Hapi ulibaini shehena hiyo katika maghala zaidi ya matatu yasiyo rasmi.

Hapi alisema, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema, waliendesha operesheni hiyo na kuwabaini walioficha sukari.

“Tumeikuta kwenye viroba vya kilo 25 katika maghala mbalimbali likiwamo la Mtaa wa Mferejeni,’’ alisema.

Wataalamu wakosoa 
Wakati polisi na viongozi wengine wakihaha kuwasaka wafanyabiashara hao, wataalamu wameeleza kuwa janga la sukari linatokana na kukosekana kwa sera ya kumlinda mlaji.

Kihiyo alisema kama sera hiyo ingekuwapo, wafanyabiashara wasingekuwa na nguvu ya kuuza sukari kwa bei wanayotaka au kufanya bidhaa hiyo iwe adimu sokoni.

Hata hivyo, maoni hayo yalitofautiana na ya mtaalamu wa masuala ya viwanda na biashara, Adam Zuku ambaye alisema suala la sukari lina siasa ndani yake.

Zuku ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi wa maendeleo ya viwanda wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), alishangaa kuona sukari iliyokamatwa inaachiwa kwa madai kwamba, wafanyabiashara husika hao walikuwa hawajakamilisha taratibu za kuitoa.

“Mbona wakati tunalalamika hakuna sukari hawakusema kwamba wameagiza sukari wanamalizia taratibu ili isambazwe madukani?” alihoji Zuku.

Alisema jambo hilo linatokana na wafanyabiashara hao kujali masilahi yao binafsi. “Wanalalamika kisiasa tu,” alisema Zuku.

Alisema Serikali isipoendelea kuvalia njuga suala hilo, hata viwanda vya sukari vya ndani vitakufa.

Pia, alisema Serikali inatakiwa kuwa na takwimu halisi ya sukari inayohitajika nchini ili kusiwe na mkanganyiko linapotokea tatizo kama hilo.

No comments: