Pichani ni makaburi yakiandaliwa kwa ajili ya kuzikwa kwa miili saba ya familia moja mapema leo Wilayani Sengerema .
Mazishi ya watu saba wa familia moja waliouawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumatano, yanatarajiwa kufanyika leo kwa gharama za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, msemaji wa familia, Simon Mbata na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Stamil Ndalo walisema mazishi hayo yanatarajiwa kufanyika saa nane mchana.
“Miili ya marehemu itazikwa kwenye shamba la familia katika Kijiji cha Sima, kulikotokea mauaji,” alisema Mbata.
Ndalo alisema halmashauri imeamua kugharamia majeneza na kusafirisha miili ya marehemu kutoka Hospitali ya Wilaya hadi eneo la mazishi, ikiwa ni ishara ya kushirikiana na ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na mauaji hayo.
Waliouawa katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Eugenia Kwitega na watoto wake watatu, Leonard Thomas aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Sima, Leonard Aloyce na Mkiwa Phillip, wote walikuwa wakisoma Shule ya Msingi Ijinga. Wengine ni Maria Phillip ambaye ni mdogo wa mama wa familia hiyo aliyefika kijijini hapo kumtembelea dada yake, pamoja na wageni wengine wawili waliotambulika kwa jina mojamoja la Samson na Donald.
Akizungumzia upelelezi wa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Zainab Terack alisema ni mapema kutoa taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika msako kwa sababu polisi wanaendelea na upelelezi.
“Ninachoweza kuahidi ni kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama haitapumzika, hadi wauaji wote watiwe mbaroni,” alisema Terack.
Mbata yeye aliomba wote wenye taarifa zinazoweza kusaidia wahusika kutiwa mbaroni kuziwasilisha kwa vyombo vya dola.
No comments:
Post a Comment