Advertisements

Wednesday, May 25, 2016

SERIKALI YABAINISHA NGAZI TANO ZA UJANGILI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema ujangili nchini hufanyika katika ngazi tano ukiwahusisha baadhi ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi na watumishi wasio waaminifu.
Ngazi nyingine ni wawindaji haramu wanaojihusisha moja kwa moja na kuua wanyama, wasafirishaji na madalali; wawezeshaji kwenye ngazi ya nchi zinakonunuliwa nyara na wasambaza silaha ambao ni kiungo kati ya majangili nguli na watakatishaji fedha. Ngazi ya mwisho ni majangili nguli wa kimataifa.
Profesa Maghembe ambaye alitaja ngazi hizo jana bungeni alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17, alisema kutokana na hali hiyo, wizara imeimarisha kitengo chake cha intelijensia na kufanya doria kwa kuzingatia mfumo wa makundi hayo.
“Katika kudhibiti ujangili wa wanyamapori, doria zilifanyika ndani na nje ya mapori ya akiba na mapori tengefu ambapo doria 109,474 zilifanyika katika mwaka 2015/2016. Doria hizi ziliwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 176 na kesi 654 zilifunguliwa,” alisema.
Alisema kesi 161 zilimalizika kwa wahalifu 53 kuhukumiwa kifungo cha jumla ya miezi 6,360 na Sh363.9 milioni kulipwa kama faini.
“Kati ya wahalifu waliohukumiwa, wanane ni majangili nguli wenye mitandao ya kimataifa,” alisema Profesa Maghembe.
Alisema katika doria zilizofanyika, nyara mbalimbali za Serikali zilikamatwa ambazo ni pamoja na mijusi 315, kobe 202, tumbili 81 na nyani mmoja.
Profesa Maghembe alisema vipande 253 vya meno ghafi ya tembo vyenye uzito wa kilo 634 na vipande 34 vya meno ya tembo yaliyochakatwa vyenye kilo mbili, vilikamatwa.
“Vilevile, kilo 10,096 za nyamapori ya wanyama aina mbalimbali na ngozi 39 za wanyamapori zilikamatwa. Pia, bunduki 85 na risasi 1,235 za aina tofauti zilikamatwa,” alisema.
Majangili watajwe
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige alisema haiwezekani Serikali na Bunge wakawa wanapambana na ujangili huku baadhi ya wabunge wakidaiwa kuhusika.
Magige alitaka Bunge lifanye uchunguzi na kujua wabunge majangili ni kina nani ili waweze kutajwa kwa kuwa tembo wanakaribia kuisha nchini.
“Hakuna mbunge ambaye yuko juu ya sheria, hivyo watajwe kwa kuwa haiwezekani tunapambana na ujangili halafu kumbe wengine wapo humuhumu,” alisema Magige.
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa wizara hiyo, Esther Matiko alisema suala la ujangili nchini limekuwa ni tishio kwa wanyama na hata binadamu wanaofanya shughuli ndani ya hifadhi.
“Ujangili nchini umeiletea nchi sifa mbaya kimataifa. Serikali hii yenye falsafa ya kutumbua majipu lazima sasa ijielekeze katika kuwatumbua wale wote wanaohusika katika kukwamisha kesi za ujangili ili zisimalizike kwa wakati,” alisema Matiko.

3 comments:

Anonymous said...

Nimefuatilia hotuba ya waziri wa mali asili na utalii jana,na nimewasikiliza wabunge wakiongea kwa uchungu sana,binafsi imenigusa sana kwa kuwa huko nyuma niliwahi kuchangia katika blogu hii kuwa waziri huyu ni mtu wa kukurupuka hasa pale walioshitakiwa na kupelekwa mahakamani kuwa wanataka kutosha ngedere kule Arusha na nilisema kuwa huyu waziri utendaji wake unashaka watu wale wameonewa bure vibali ni halali kwa nini?? wanafunguliwa mashitaka ya uonevu,kwa kosa gani?? ndiyo maana hata leo hii DPP anandanganywa kuwa kuna maagizo toka ngazi za juu,kesi inashindwa kuendelea kwa kuwa wameshaona hawa watu watawashinda zaidi ya kuwapiiga tarehe kesi haianzi zaidi ya kuahirishwa kila siku,kwa kweli ni aibu najua wale waholanzi watadai hasara ya kuwaweka ndani kwa uonevu.nashikuru sana wabunge wa upinzani kwa kusemea na kukemea hili suala la aibu kwa nchi

Anonymous said...

Nimefuatilia hotuba ya waziri wa mali asili na utalii jana,na nimewasikiliza wabunge wakiongea kwa uchungu sana,binafsi imenigusa sana kwa kuwa huko nyuma niliwahi kuchangia katika blogu hii kuwa Waziri huyu ni mtu wa kukurupuka hasa pale walioshitakiwa na kupelekwa mahakamani kuwa wanataka kutosha ngedere kule Arusha na nilisema kuwa huyu waziri utendaji wake unashaka aliitwa mzigo.watu wale wameonewa bure vibali ni halali kwa nini?? wanafunguliwa mashitaka ya uonevu,kwa kosa gani?? ndiyo maana hata leo hii DPP anandanganywa kuwa kuna maagizo toka ngazi za juu,kesi inashindwa kuendelea kwa kuwa wameshaona hawa watu watawashinda zaidi ya kuwapiga tarehe kesi haianzi zaidi ya kuahirishwa kila siku,kwa kweli ni aibu najua wale waholanzi watadai hasara ya kuwaweka ndani kwa uonevu.nashukuru sana wabunge wa upinzani kwa kusemea na kukemea hili suala la aibu kwa nchi.Vile vile hapa kuna dalili dhahiri kabisa ya rushwa juu ya hawa jamaa kuwekwa ndani si bure.kwa kuwa mfanyabiashara mmoja wa kirusi aliye na leseni ya nyara aliyekosa deal au tender ya kusupply huko Armenia hawa tumbili akishirikiana na wafanyabiashara wa kiasia wenye nguvu hapa Tanzania ndiye aliyeshirikiana nao na kuwakomoa kushirikiana na huyu Waziri ili ionekane wanatorosha hawa ngedere.ambao hawa wanyama si adimu na waharibifu kwenye mashamba ndiyo maana Tanzania ina quota ya cites ya kuuza nje 6000 kila mwaka.nafikiri Raisi Magufuli kadanganywa au hajui kabisa kuwa hii ni biashara halali na watu wana leseni na inafanywa na wazawa

Anonymous said...

If the so called allegations are groundless why should anyone protest against the judicial process? If you have any contrary evidence register yourself as a witness. Huwezi kudai watu wameonewa bila kuwa na ushahidi. Ndio maana kuna Mahakama. Vinginevyo ni kilio cha part of a network that has benefitted from the corruption that the government is trying to stump. The issue here, if any, ought to be kilio kwamba utaratibu wa Mahakama uwe expedited ili iwapo hawana makosa wasiendelee kuwa chini ya wingu la tuhuma. Vile vile iwapo wana hatia wakatumikie rupango na kurejesha kile nchi ilichopoteza. Simple. Zingine ni siasa tu.