Leo rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli ametimiza siku 200 tangu ameapishwa kuwa rais wa awamu ya tano kuiongoza Tanzania.
Tangu alipoapishwa Novemba 5 kwenye uwanja wa Uhuru na kuanza kazi siku hiyo hiyo aliyoapishwa, rais Magufuli amekutana na changamoto kadhaa zilizofanya uchumi wa nchi usikuwe kwa kasi inayotakiwa.
‘Hapa Kazi Tu’ ndiyo ulikuwa msemo wa rais Magufuli kwenye kampeni zake za kuwania urais lakini baadhi ya watu walidhani hayo yalikuwa ni maneno lakini kwenye utekelezaji wake wa vitendo usingeweza kufanya kazi kutokana na mizizi iliyopandikizwa tangu hapo awali.
Disemba 4 mwaka jana, Magufuli alifanya mkutano na wafanyabiashara na kuwapa siku saba wale wote waliopitisha makontena yao bandarini bila ya kuyalipia kodi ikiwa ni zaidi ya makontena 1300 yalipitishwa bila ya kulipiwa kodi.
Rais Magufuli ameweza kujitahidi kupunguza baadhi ya matumizi yasiyokuwa ya lazima kwa watu wachache na fedha zake kuzipeleka kwenye vitu vya msingi vyenye manufaa kwa wengi.
Hakika serikali ya Magufuli ina safari ndefu ya kupambana mpaka kumaliza awamu ya kwanza ya uongozi wake. “Kuanzisha mahakama ya mafisadi” ndiyo ilikuwa moja ya ahadi ya rais Magufuli aliyoitoa wakati wa kuomba kura kwa wananchi za Urais.
Rais Magufuli akiwa kwenye mapumziko nyumbani kwao, Chato alisema, “kama kule Dar es Salaam kuna mfanyakazi mmoja wa TRA analipwa mishahara hewa ya wafanya kazi 17.” Mpaka sasa agizo la rais kwa Wakuu wa Mikoa limetekelezeka kwa asilimia kubwa na kubaini zaidi ya watumishi hewa 2500 huku bado zoezi la uhakiki likiendelea zaidi.
Watumishi kadhaa mpaka sasa wamekutana na rungu la rais Magufuli na amefanikiwa kuwatumbua kutokana na oparesheni yake ya ‘Tumbua Majipu’ akiwemo aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga [Anne Kilango], Waziri wa Mambo ya Ndani [ Charles Kitwanga], Mkurugenzi wa TIC [Juliet Kairuki], na wengine kibao.
Tatizo la sukari kwa sasa ndiyo changamoto kubwa inayokabiliana nayo serikali ya awamu ya tano huku baadhi ya maeneo sukari ikionekana kuuzwa kati ya shilingi 2500 mpaka 4000 kwa kilo moja.
Lakini wiki iliyopita Waziri Mkuu alizungumzia suala hilo bungeni na aliahidi serikali bado inalifanyia kazi tatizo hilo huku tukiendelea kusubiri tani elfu hamsini ambazo serikali imeziagiza nje ili zije kuziba tatizo la sukari lililopo nchini.
Hakuna binadamu aliye mkamilifu, kuna baadhi ya mambo rais Magufuli ameweza kuteleza kama binadamu lakini kwa kiasi kikubwa ameweza kuiongoza safari ya jahazi la Tanzania ipasavyo na kuwaacha midomo wazi wale walioamini kuwa hawezi.
No comments:
Post a Comment