Wakati sakata la kampuni ya Lugumi Enterprises likiendelea kutikisa nchi, mashine za utambuzi wa alama za vidole, zimeanza kufungwa katika mikoa kadhaa ikiwamo ya Dodoma na Geita.
Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha kwamba juzi mashine hizo zilifungwa katika vituo vya polisi vya wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma na kazi hiyo ilitarajiwa kufanywa mjini Dodoma jana. Pia, vyanzo vya habari kutoka mkoani Geita vimeithibitishia Mwananchi kwamba mashine hizo zimefungwa katika vituo vitano vya polisi.
Kampuni ya Lugumi iliingia mkataba na Jeshi la Polisi mwaka 2011 kufunga mashine hizo kwenye vituo 108, lakini hadi wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anamaliza ukaguzi, ni vituo 14 tu vilikuwa vimefungwa mashine hizo.
Taarifa hiyo ya CAG ililistua Bunge na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) iliunda kamati ndogo ili kuzunguka mikoani kuthibitisha taarifa hiyo ya mkaguzi mkuu.
Lakini wakati kamati hiyo ikiwa imepewa kazi hiyo, Mwananchi imeambiwa kuwa mashine hizo zinafungwa.
“Tulikuwa na Lugumi hapa,” alisema mmoja wa watoa habari waliozungumza na Mwananchi.
“Vijana wa Lugumi walikuwa wanafunga mashine, wameondoka kwenda Kongwa. Kesho (jana) watakuwa Dodoma.”
Imeelezwa kuwa vijana wanaofunga mashine hizo walikwenda Mpwapwa wakitokea Kibaha mkoani Pwani. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, katika Mkoa wa Geita, mashine hizo zimefungwa wilaya za Nyang’hwale, Chato, Geita, Bukombe na Mbogwe.
Alipotafutwa kutoa ufafanuzi wa kazi ya ufungaji mashine hizo, Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Latson Mponjoli alisema suala hilo ni la kitaifa hivyo kutaka watafutwe viongozi wa kitaifa.
“Mimi nitazungumzia nini kuhusiana na Lugumi? Suala hilo ni la kitaifa unaniuliza mimi? Hilo suala mtafute waziri mwenye dhamana au IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi) ndiyo wenye mamlaka ya kulizungumzia jambo hilo,” alisema Kamanda Mponjoli.
Lakini juhudi za kumpata IGP Ernest Mangu kwa simu hazikufanikiwa badala yake simu yake ilipokewa na msaidizi wake. Mwandishi alipoanza kuzungumza naye, simu yake ilikatika.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema hataki kujibu maswali yanayohusu kampuni hiyo na kwamba mwandishi awasiliane na kampuni hiyo. “Taarifa za Lugumi kawaulizeni Lugumi wenyewe, sipendi kujibu maswali ya kijinga na upumbavu, kwa sababu nimekwenda vituoni mwenyewe nimejionea,” alisema na kukata simu. Alipopigiwa simu tena ili aeleze amejionea nini hakupokea.
Hata hivyo, hakuna mtu yeyote kutoka Lugumi ambaye amekuwa tayari kuzungumza ingawa vyanzo vya habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi vimesema kwamba utekelezaji wa kazi ya kufunga kompyuta hizo aina ya Dell umeanza.
“Unajua hili ni agizo na amri ya kamishna mmoja wa makao makuu. Kuna gari lililofuata vifaa hivyo makao makuu na kompyuta hizi zilifika hapa Jumatano na zikafungwa Alhamisi, lakini kama nilivyosema haziwaki na hata askari hawana mafunzo ya kuzitumia,” alisema mpashaji mwingine aliyeomba jina lake lihifadhiwe.
Mtoa taarifa huyo alisema uharaka wa kufunga mashine hizo unafanywa ili kujiandaa kwa ukaguzi wa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wanaotarajiwa kupita wilayani na mikoani kuthibitisha uwepo wa mashine hizo. Kwamba watakapofika wakaguzi wadhani kwamba vifaa hivyo vilikuwapo tangu awali wakati si kweli.
‘’Ndugu yangu, huwezi kuamini kompyuta za Lugumi zimewasili hapa mkoani kwetu (Geita), lakini sasa zimeletwa kwa lengo moja tu kuwahadaa wakaguzi kwamba zilikuwepo tangu awali wakati si kweli. Hizo kompyuta zililetwa Jumatano wiki iliyopita na zilifungwa Alhamisi na mbaya zaidi haziwaki, yaani ni mbovu,” alisema mtu huyo.
Mjumbe mmoja wa PAC aliwahi kulalamika kuwa kuna mchezo unachezwa wa kukwamisha kamati ndogo baada ya Bunge kuchelewa kutoa fedha za kuwezesha kazi ya ukaguzi kuanza kwa lengo la kutoa mwanya wa kufungwa kwa mashine hizo nje ya muda.
Juhudi za kumpata Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hillaly ili atoe ufafanuzi wa kazi hiyo kufanywa sasa tena na polisi wenyewe, hazikuzaa matunda. Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ndogo ya PAC iliyopewa jukumu la kuchunguza sakata la Lugumi kwa siku 30, alisema mambo yote yatakuwa kwenye ripoti yao. “Kama wanafunga mashine au hawafungi hilo sijui, we subiri tu tumalize kazi tutatoa ripoti,” alisema.
Habari zinasema tayari kamati hiyo iliyogawanywa katika makundi matatu imekamilisha ukaguzi katika Mkoa wa Dodoma.
Kamati ya PAC ndiyo iliyoibua sakata hilo katika vikao vya kamati vya Aprili, ikinukuu ripoti ya CAG ya mwaka 2014/2015 kwamba kampuni hiyo iliyoingia mkataba na Polisi kufunga mashine hizo haikuwa imekamilisha kazi hiyo.
Pamoja na kutokamilisha ufungaji mashine hizo, Lugumi ilishalipwa Sh34 bilioni sawa na zaidi ya asilimia 90 ya jumla ya malipo ya Sh37 bilioni za mkataba, jambo ambalo wabunge wanaona ni viashiria vya ufisadi katika Jeshi la Polisi.
Katika sakata hilo, pia anatajwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga akitakiwa ajiuzulu kwa madai kuwa ana hisa kwenye kampuni ya Infosys, ambayo ilitoa ushauri wa kitaalamu kwenye mradi huo, ikiwa imeombwa na kampuni ya Kimarekani ya Biometrica ambayo iliipa Dola 75,240 (sawa na zaidi ya S150 milioni).
Hata hivyo, Infosys imenukuliwa ikidai kuwa Kitwanga alishajiondoa kwenye uendeshaji wa kampuni hiyo mwaka 2010 na tangu wakati huo hajakanyaga kwenye ofisi zao.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment