Advertisements

Thursday, May 26, 2016

TEMEKE YAPIGA MARUFUKU UFANYAJI WA MAZOEZI BARABARA KUU

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imepiga marufuku vikundi vya mazoezi vinavyofanya mazoezi kwenye barabara kuu ya uwanja wa Taifa ili kuzuia foleni na ajali za barabarani.

Tamko hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Habari wa Halmashauri hiyo, Joyce Msumba alipokua akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu foleni ya magari inayosababishwa na wachezaji wanaotumia barabara kuu ya Temeke kuelekea uwanja wa Taifa.

“Halmashauri yetu imepiga marufuku wachezaji wote wanaokimbia kuelekea uwanja wa Taifa kupitia barabara kuu na badala yake wanatakiwa kutumia njia za waendao kwa miguu (service road) zilizopo pembezoni mwa barabara kuu”,alisema Joyce.


Joyce aliongeza kuwa kila kundi la wachezaji wana viongozi wao ambao walishapewa maelekezo na Halmashauri juu ya suala hilo kwahiyo,viongozi hao wana wajibu wa kuwasimamia wanamichezo wao.

Kwa upande wake Afisa Utamaduni wa Halmashauri hiyo, Emmanuel Ndumukwa amewaomba wanamichezo hao kuzingatia sheria za barabarani ili kuepusha ajali.

“Mara nyingi tunawaeleza wanamichezo wazingatie sana sheria za barabarani pamoja na kutumia bendera nyekundu kama alama ya kuashiria uwepo wao katika barabara ili kuzuia ajali”,alisema Ndumukwa.

No comments: